Sunday, October 11, 2015

Wawili CUF Mtwara watekwa na kupewa kibano.

Mwanachama wa Chama cha Wananchi (CUF) mkazi wa Magomeni Kagera, manispaa ya Mtwara mikindani, Kissa Mwaya, akiwa amelazwa katika wodi namba 8 katika hospitali ya rufaa ya mkoa wa Mtwara, Ligula, kutokana na kuumizwa na watu wasiojulikana baada ya kutekwa na kupewa kipigo.


Kisa Mwaya

Mwanachama wa Chama cha Wananchi (CUF) mkazi wa manispaa ya Mtwara mikindani, Haji Bakari, akiwa amelazwa katika wodi namba 8 katika hospitali ya rufaa ya mkoa wa Mtwara, Ligula, kutokana na kuumizwa na watu wasiojulikana baada ya kutekwa na kupewa kipigo


 Na Juma Mohamed.

WANACHAMA wawili wa Chama cha Wananchi (CUF) manispaa ya Mtwara Mikindani, wamelazwa katika hospitali ya rufaa ya Ligula, huku wakiugulia maumivu waliyoyapata baada ya kutekwa na kuteswa na watu waiojulikana usiku wa Oktoba 9 kuamkia juzi Oktoba 10.
Wakizungumza hospitalini hapo leo, walisema mazingira yakutekwa kwao yanafanana kwasababu wote walitekwa siku moja ambapo ilikuwa ni usiku huku kila mtu akifuatwa nyumbani kwake na watu ambao walijifanya ni askari.
Haji Bakari alisema alikuwa tayari ameshaingia ndani kulala kabla ya muda mfupi baadae kusikia sauti ikimuita kwa jina lake, ambapo aliitika na kuambiwa asogee upande wa dirishani na kumuambi atoke nje bila kutambua anaitwa na nani akatoka.
“kwahiyo nilivyofungua tu mlango nikatokea nje nikakutana na watu watatu ambao walinikamata na kuniewka chini ya ulinzi na kuniambia bwana uko chini ya ulinzi, nikawauliza kwa kosa gani waksema twende utaenda kujieleza kituoni..nikawaambia basi wasubiri nichukuwe hata fulana nivae wakasema sio rahisi kukuruhusu uingie ndani tena na wakati huo walikuwa tayari wameshanikamata.” Alisema.

Haji Bakari


Na kuongeza “baada ya kukamatwa nikawa nimechukuliwa na nikigeuka nyuma naona wanatokea watu wawili tena na kufanya jumla kuwa watu watano..wakaniingiza kwenye gari Toyota Landa Cruiser nyeupe, wakanifunga mikono na usoni nikafungwa kitambaa wakanilazisha nilale chini niinamishe kichwa..” aliongeza.
Alisema baada ya hapo haikusikika sauti yoyote hadi pale ambapo alisikia sauti ikisema “mlete huyo dogo” kasha kusafiri kwa umbali mrefu huku hawafahamu wapi wanakopelekwa na tayari ilikuwa ni usiku sana.
Alisema, walipofika huko ambako walikusudia walianza kumshusha mmoja kasha kuanza kumshushia kipigo wakipiga zaidi katika magoti kwa kutumia kitu ambacho hakuweza kukifahamu ni nini.
Naye, Kissa Kasim Mwaya, ambaye ni mkazi wa Magomeni Kagera mjini hapa, aliezea tukio la kukamatwa kwake na kupelekwa huko ambapo mazingira yake hayana tofauti na namna alivyokamatwa mwenzie.
Alisema, alisikia ikitoka amri ikisema “mpige zipu huyo” ambapo alijikuta akifungwa kitambaa usoni na kusafirishwa kwa umbali mrefu tofauti na alivyodhani kwamba anaelekea kituo cha polisi.

Kisa Mwaya

 Alisema baada ya kufikishwa walikokusudia, walianza kumpa kipigo kikali kilichopelekea kushindwa hata kusimama kwa muda flani ambapo baadaye walipoamua kuwaacha wakawafungua vitambaa kabla ya kuwasha gari na kuondoka wakiwaacha huko ambako wenyewe wanasema ni katikati ya kijiji cha Libobe na Utende.
“Baada ya kupata nguvu kidogo tukajaribu kwenda kwa mwenyekiti kumuulizia kama kuna kituo cha afya au zahanati, akasema hapa kupata huduma itakuwa vigumu sana usiku huu kwasababu daktari halali hapa kijijini anaishi Naliendele..chamsingi ni kuangalia jinsi gani mnaweza kufika nyumbani.” Alisema.
Alisema, msaada amabao waliupata kupitia kwa mwenyekiti huyo ambaye hakumtaja jina ni kuwatafutia usafiri wa pikipiki ambao uliwawezesha kuwafikisha mjini Mtwara.
Aidha, alihusisha tukio hilo moja kwa moja na siasa kutokana na yeye kuwa ni mwanachama wa CUF ambaye pia ni muhamasishaji hasa katika kipindi hiki cha kampeni ambaye hata akitetea hoja zake anapokuwa na watu wa Chama cha Mapinduzi (CCM) mara nyingi anashinda.
Alisema, kuna baadhi ya maneno ambayo walikua wakitamkiwa wakiwa njiani kuelekea huko huku zaidi wakiwatamkia kwamba “nyie hamtaki CCM, mtaona..”.
Hata hivyo, walisema kuwa tukio hilo haliwezi kuwakatisha tama ya kuendeleza harakati zao za uhamasishaji, na kwamba ndio watazidi kuongeza juhudi kwasababu siasa za Tanzania ni laini na hazina changamoto kama zilivyo katika nchi nyingine.
“Huko South Africa mpaka sasaivi kuna pendeza, wakombozi wao wengi wamefungwa sio chini ya miaka 25, wengi wamedai mapambano ili nchi yao iwe huru..kwahiyo hili bado na tena ndio limenipa hamasa zaidi ya kujua haki haipatikani kirahisi..” alisema Kissa.
Mganga mfawidhi wa hospitali hiyo, Dkt. Mhuza Mdoe, hakuzungumzia hali zao na namna walivyoathirika ndani ya miili yao lakini alikiri kuwapokea.
Naye, mkurugenzi wa siasa wa CUF mkoa wa Mtwara, Saidi Mtunduima, alisema bado chama hakijafanya uchunguzi wowote juu ya tukio hilo huku wakisubiri wenyewe wapate nafuu na kuweza kueleza vizuri pengine watawakumbuka waliowafanyia kitendo hicho.
Kamanda wa polisi mkoani hapa, Henry Mwaibambe, alipoulizwa juu ya tukio hilo, alisema halijui kwasababu bado halijafika ofisini kwake, hivyo hawezi kuzungumza lolote.

Tukio hilo linakuja wiki moja baada ya kutokea tukio la kutekwa na kuteswa kwa mgombea ubunge wa jimbo la Mtwara mjini kupitia Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) Joel Nanauka, ambaye hata hivyo watu waliofanya hivyo bado hawajafahamika.

No comments: