Monday, October 12, 2015

Jeshi la polisi Mtwara ladai kupata shida upelelezi wa mgombea CHADEMA aliyetekwa.

Kamanda wa polisi mkoa wa Mtwara ASP Henry Mwaibambe, akizungumza na viongozi wa vyama vya siasa, kuhusu matukio ya uvunjifu wa amani yanayofanywa na baadhi ya wafuasi wa vyama hivyo katika mikutano ya kampeni inayoendelea katika maeneo mbalimbali mkoani hapa. 



Kamanda wa polisi mkoa wa Mtwara ASP Henry Mwaibambe, akizungumza na viongozi wa vyama vya siasa, kuhusu matukio ya uvunjifu wa amani yanayofanywa na baadhi ya wafuasi wa vyama hivyo katika mikutano ya kampeni inayoendelea katika maeneo mbalimbali mkoani hapa. 

Henry Mwaibambe


Viongozi wa vyama vya siasa mkoa wa Mtwara wakiwa katika kikao cha pamoja na kamanda wa polisi mkoani hapa Henry Mwaibambe, kuhusu hali ya uvunjifu wa amani inayofanywa na baadhi ya wafuasi wa vyama hivyo katika mikutano ya kampeni inayoendelea katika maeneo mbalimbali

Na Juma Mohamed.

Jeshi la polisi mkoa wa Mtwara limesema tukio la kutekwa mgombea ubunge wa Mtwara mjini kupitia Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Joel Nanauka, linawapa shida katika kulifuatilia kutokana na mwenyewe kutotoa ushirikiano nzuri kwa jeshi hilo.
Akizungumza katika mkutano na viongozi wa vyama vya siasa, kamanda wa polisi mkoani humo, Henry Mwaibambe, alisema maelezo yaliyotolewa na mgombea huyo hayakuwa katika mlolongo mzuri kiasi cha kuwapa urahisi wa kujua pakuanzia kufanya upelelezi.

Mgombea Ubunge jimbo la Mtwara mjini kupitia Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Joel Nanauka, akiwa wodini katika hospitali ya rufaa ya Ligula mkoani Mtwara, alikopelekwa kwa ajili ya kupata matibabu kutokana na maumivu aliyoyapata kwa kipindi amabcho alikuwa haonekani

“Mgombea wa CHADEMA mwenyewe hajatusaidia, ametunyima sisi fursa ya kupata njia ya kupitia, kuna vitu vitatu hapa, cha kwanza ni maelezo yake ametoa maelezo mara mbili, kwanza anasema amepigiwa simu na mtu asiye mfahamu maeneo ya Mnarani kwamba akakutane naye alipofika akaambiwa apande kwenye gari wakaenda mpaka Mikindani wakamshusha wakampulizia dawa usoni, akashtukia asubuhi yupo mahakama ya mwanzo..” alisema.

Henry Mwaibambe

Na kuongeza “hayo ni maelezo ambayo ameandika ya kwanza lakini baadae akiwa Ligula (Hospitali ya rufaa ya mkoa) akasema anataka kukutana na maofisa wa polisi lakini kusiwe na mtu mwingine yeyote, kule akatoa maelezo tofauti kwamba alipanda bajaji akaenda sijui Guest akatoka akakaa pale akataka kutoka watu  wakamzuia..kwahiyo maelezo kama haya tunashindwa tuanzie wapi.” Alisema.
Aidha, alisema jeshi hilo limevumilia vya kutosha vitendo vya uvunjifu wa amani vinavyofanywa na baahi ya wafuasi wa vyama vya siasa katika mikutano ya kampeni, na sasa litaanza kuchukua hatua dhidi ya watakao bainika kufanya hivyo.
Alisema kumekuwa na matukio ya kuashiria uvunjifu wa amani ambayo yamekuwa yakifanyika katika mikutano ya kampeni na wafuasi wa vyama hivyo huku wengine wakifanya mbele ya askari polisi.

Henry Mwaibambe na wanasiasa

Aliwakumbusha baadhi ya mambo ambayo kwa mujibu wa sheria ya maadili ya uchaguzi, hayapaswi kufanyika kuwa ni pamoja na kufanya fujo katika mikutano ya vyama vingine, kutoa lugha za matusi, kejeli, kashfa, udhalilishaji au vitisho vinavyoashiria uvunjufu wa amani katika mikutano ya kampeni.
“Hairuhusiwi kubeba sanamu, kinyago au kitu chochote kinachoonesha kudhalilisha, kukebehi au kufedheesha chama kingine cha siasa au kiongozi wake au serikali katika mkutano wowote wakisiasa..haya yanafanyika na nyie mnafahamu kuwa ni kosa la jinai, kuanzia tarehe 12 ya leo (jana) hatutavumilia kitu kama hicho..” alisema.

Henry Mwaibambe na wanasiasa

Aliwataka kuacha kutumia vipaza sauti kwa ajili ya kutangaza ratiba za mikutano yao kuanzia saa 2 usiku jambo ambalo linafanyika kila siku katika kipindi hiki cha kampeni na ni kwa vyama vyote ambavyo vina wagombea.
Alitoa wito kwa wananchi na wanasiasa kutoa ushirikiano kwa jeshi la polisi juu ya viashiria vyovyote vya uvunjifu wa amani na kwamba kwa kuliachia jeshi hilo pekee haliwezi kujua kila kitu kinachotokea au kutarajia kutokea kwasababu wao sio malaika kwamba wanajua kila kitu.
Kwa upande wao, viongozi wa vyama ambao walihudhuria kikao hicho walikiri kutokea kwa vitendo hivyo kwa wafuasi wao na kuahidi kwenda kuzungumza nao ili waweze kuacha na kuhepusha kukamatwa na kushitakiwa jambo ambalo litawakosesha kura wagombea wao iwapo watapatikana na hatia na kuhukumiwa.
Mgombea na mwenyekiti wa chama cha NCCR-Mageuzi mkoa wa Mtwara, Uledi Hassan, alisema aliwahi kufuatwa na wafuasi wa CUF akiwa nymbani kwake usiku ambao walifanya fujo pasipo kujua sababu ya wao kufanya hivyo.

Viongozi wa vyama vya siasa mkoa wa Mtwara wakiwa katika kikao cha pamoja na kamanda wa polisi mkoani hapa Henry Mwaibambe, kuhusu hali ya uvunjifu wa amani inayofanywa na baadhi ya wafuasi wa vyama hivyo katika mikutano ya kampeni inayoendelea katika maeneo mbalimbali


Alimshukuru kamanda kwa kuwaita na kuzungumza nao kirafiki huku akiahidi kuwaita wafuasi wake na kuzungumza nao juu ya kufanya kampeni za kistaarabu katika muda mchache uliobaki kabla ya tarehe ya kupiga kura.
Naye mwenyekiti wa CHADEMA mkoa wa Mtwara, Kasim Bingwe, alisema kutokana na kikao hicho amebaini kuwa vipo vyama ambavyo havifanyi siasa za kweli na kusema kuwa wananchi kwa sasa wanahitaji mabadiliko kutokana na kuchoshwa na utawala wa chama kimoja cha CCM ambacho hata hivyo hakikuwa na mwakilishi yeyote katika kikao hicho.
Aliwataka wananchi kuacha kufanya maandamano kiholela wakati wanapotoka katika mikutano ya kampeni ambapo wanasababisha kufunga barabara na watumiaji kukosa nafasi za kupita huku akinukuu kauli ya kamanda kwamba “maandamano yanayotakiwa ni ya kwenye karatasi za kupigia kura ifikapo Oktoba 25”.


No comments: