Tuesday, October 13, 2015

Samatta kuwania tuzo CAF

Mbwana Samatta

Mshambuliaji matata Mbwana Aly Samatta anayeichezea klabu ya TP Mazembe ametajwa miongoni mwa wachezaji 24 watakaowania tuzo ya mchezaji bora Afrika anayecheza ligi ya barani Afrika.
Uteuzi wake umetokea siku chache tu baada yake kuisaidia Taifa Stars kufika raundi ya pili ya mechi za kufuzu kwa Kombe la Dunia.
Magoli yake matano katika awamu za robo fainali na nusu fainali yaliiwezesha TP Mazembe kufika fainali ya kombe la kilabu bingwa barani Afrika kwa mara yake ya kwanza tangu mwaka wa 2010.
Mwaka jana, tuzo hiyo ilitwaliwa na raia wa Congo Firmin Ndombe Mubele.
Katika hatua ya robo fainali, Samata alifunga magoli matatu walipoicharaza Moghreb Tetouan kwa magoli 5-0 na kufuzu kwa nusu fainali.
Licha ya kupoteza mechi ya mkondo wa kwanza wa nusu fainali kwa magoli 2-1 dhidi Al Merreikh ya Sudan, Mazembe iliibuka na ushindi wa 3-0 baada ya Samatta kufunga magoli mawili katika dakika za 53 na 70.
Raia wa Ivory Coast, Roger Assale alifunga kazi dakika ya 72 na kuiwezesha Mazembe kuondoka na ushindi wa 4-2 na kuingia fainali ambapo itachuana na USM Alger Oktoba 30.
Mwaka jana, Samatta alitambulika na klabu yake ya TP Mazembe kwa kutunukiwa mchezaji bora wa klabu mwaka wa 2013.
Uteuzi huo huenda ukampiga jeki mshambuliaji huyo wa zamani wa klabu ya Simba kwani tayari amefichua hamu yake ya kucheza soka barani Ulaya.
SOURCE: BBC SWAHILI

No comments: