Wednesday, October 14, 2015

Uchaguzi Marekani-Clinton na Sanders wakosoana kwenye mdahalo

Bernie Sanders na Hillary Clinton

Hillary Clinton amemkosoa mpinzani wake mkuu Bernie Sanders kuhusu sheria za umiliki wa bunduki Marekani katika mdahalo wa wanaotaka kuwania urais kwa tiketi ya chama cha Democrats nchini humo.
Alipoulizwa iwapo seneta huyo wa Vermont anatosha katika kukabiliana na tatizo hilo, Bi Clinton alisema “la hasha” kabla ya kuapa kuwa atawaandama wanaotengeneza bunduki zinazotumiwa kupiga watu risasi akichaguliwa rais.
Bw Sanders naye alimshutumu Bi Clinton, akisema hatua yake ya kuunga mkono agizo la ndege kutopaa anga ya Syria inaweza kusababisha “matatizo chungu nzima”.
Mikutano ya kampeni ya Sanders imekuwa ikivutia watu wengi na amekuwa akitishia umaarufu wa Bi Clinton katika majimbo mengi muhimu.
Majibizano makali kati ya wawili hao yalitawala mdahalo huo Las Vegas na wagombea wengine watatu wanaosaka tiketi ya chama hicho hawakusikika sana.
Wagombea hao wengine ni aliyekuwa gavana wa Maryland Martin O'Malley, aliyekuwa seneta wa Virginia Jim Webb na aliyekuwa seneta wa Rhode Island Lincoln Chafee.
Moja ya mambo waliyotofautiana sana Sanders na Clinton yalikuwa kuhusu sharia ya udhibiti wa bunduki.
Suala hilo tata lilirejea baada ya ufyatuaji wa risasi katika bewa la chuo kimoja Oregon.
Bi Clinton aliposema mpinzani wake hajaonyesha uthabiti wa kutosha, akirejelea hatua ya Sanders ya kupigia kura hatua ya kukinga watengenezaji wa silaha hizo 2005.
Wawili hao pia walijadiliana kuhusu manufaa ya mfumo wa ubepari, Bi Clinton akisema litakuwa “kosa kubwa” kwa taifa hilo kukataa ubepari.
Makamu wa rais Joe Biden bado anatafakari uwezekano wake wa kujitosa katika kinyang’anyiro hicho ingawa hakujitokeza dakika za mwisho jukwaani, kama walivyotarajia wengi wa wafuasi wake.
Bi Clinton amekuwa akipoteza umaarufu kutokana na kufichuka kwa habari kwamba alitumia anwani yake ya kibinafsi ya barua pepe kwa shughuli za kiserikali alipokuwa waziri wa mashauri ya nje wa Marekani. Ametaja hilo kuwa kosa.
Hata hivyo, alikaa imara Bw Chafee alipotilia shaka kuaminika kwake, na alikataa kujibu hilo alipotakiwa kulizungumzia.
Wagombea hao walijaribu kutenganisha mdhahalo wao na midahalo Republican, ambapo muda mwingi ulitumiwa kujadili masuala ya kijamii kama vile utoaji mimba na ndoa za jinsia moja.
Bw O'Malley alitumia hotuba yake fupi ya dakika 90 ya kufunga mchango wake kusema midahalo ya Republican iliangazia sana chuki.
Lakini mgombea wa Republican Jeb Bush alisema hakuona chochote cha kumpendeza katika mdahalo huo uliofanyika Las Vegas.
Uchaguzi mkuu nchini Marekani utafanyika Novemba 2016.

SOURCE: BBC SWAHILI

No comments: