Saturday, October 10, 2015

JK aitaka TPDC kutatua kero za maji Madimba-Mtwara



RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Jakaya Kikwete, akihutubia katika zoezi la uzinduzi wa miundombinu ya kuchakata na kusafirisha gesi asilia, iliyopo Madimba-Mtwara na Songosongo-Lindi. Zoezi ambalo lilifanyika Madimba mkoani Mtwara.




Baadhi ya wageni waalikwa waliojitokeza Madimba, katika uzinduzi wa miundombinu ya kuchakata na kusafirisha gesi asilia ya Madimba-Mtwara na Songosongo-Lindi, lililofanywa leo na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Jakaya Kikwete.



Na Juma Mohamed.

RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Jakaya Kikwete, amelitaka Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC) kutekeleza wajibu wao wa kufikisha huduma za maji kwa wananchi wanaoishi katika vijiji vinavyozunguka mradi wa miundombinu ya gesi asilia, uliyopo Madimba, mkoani hapa.
Akizungumza juzi mkoani hapa katika uzinduzi wa mradi huo, alisema ni wajibu wa shirika hilo kuboresha huduma za kijamii ambazo zitawanufaisha wananchi wanaoishi katika vijiji jirani na mradi huo.
“Maji mliokuwa nayo hapa, chukuweni yale mnayoweza kutumia nyie lakini mchangie na jirani, lakini kwa jirani zenu wanaowazunguka tafuteni mitambo na wataalam wa kutafuta kaji chini ya ardhi chimbeni visima..wachimbieni visima virefu wapate maji ya kutosha ili wasiwe tena wananung’unika kwamba wale jamaa wanachukua gesi lakini sisi wanatuacha bila maji..” alisema.

Mhe. Dkt. Jakaya Kikwete.


Alisema, kwa kufanya hivyo itasaidia kwa kiasi kikubwa kuondoa migogoro baina yao na wananchi wanaowazunguka, na kwamba huo ni wajibu wao kwasababu moja ya kero kubwa kwa wananchi waishio vijijini ni upatikanaji wa maji.
Aliwataka viongozi wa shirika hilo kutoishia katika kutatua kero ya maji pekee, kwani kuna kero nyingine za kijamii zinazowakabili wananchi hao ambazo ni miundombinu ya elimu, afya na barabara.
“Lakini msiishie kwenye maji, wana mahitaji mengi, shule zao watoto hawana madawati, zahanati zao ziko hali mbaya, jimeni muwasaidie..saidieni zahanati, saidieni shule zao, msaidie kujenga nyumba za walimu..ni ghara lakini wala sio kubwa ukilinganisha na mapato mtakayoyapata kwenye gesi hii katika miaka miamoja inayokuja..” alisema.
Rais aliyasema hayo kufuatia ombi lililotolewa na mbunge wa jimbo la Mtwara vijijini na Waziri wa Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) Mhe. Hawa Ghasia, kwamba wananchi hao wanapata shida katika kutafuta maji huku wakilazimika kusafiri umbali mrefu kufuata huduma hiyo.
Alisema, mbali na maji tatizo linguine ambalo linahitaji utatuzi na kuondoa malalamiko kwa wananchi ni kusambazwa kwa umeme, ambapo yapo maeneo ambayo bado hayajafikiwa na huduma hiyo huku hata yale ambayo yamefikiwa baadhi ya wananchi wanalalamikia gharama wanazolipia na kuitaka serikali kuwaondolea kabisa gharama ili watumie bure.
Aliwapa pole Shirika la Umeme Tanzania (TANECCO) kutokana na matatizo ya kukatika kwa umeme ambayo yanaendelea katika baadhi ya mikoa hapa nchini yanayotokana na upungufu wa maji katika mabwawa yanayotegemewa kuzalisha umeme kwa kiasi kikubwa.
Alimtaka mkurugenzi wa shirika hilo Mhandisi Felchesmi Mramba, kuwa na uvumilivu kwasababu anakumbana na changamoto nyingi kwa wakati huu ambapo baadhi ya wanasiasa wanaliingiza swala hilo katika siasa.
“Poleni sana, lakini ndio mambo katika kazi hizi kuna wakati Fulani ikitokea watu wanakutilia shaka lakini msife moyo na endeleeleni kuchapa kazi, nyinyi hakikisheni tu kwamba umeme unapatikana haraka ili maneno hayo yaishe..wala mistake kubishana na watu kikubwa watu wanataka umeme, ukiwapatia umeme ukiwauliza bwana vipi Mramba, watesema Mramba ‘bombaa’ sasa we Mramba kazana tuu.” Aliongeza.
Kwa upande wake, waziri wa nishati na madini, Mhe. George Simbachawene, alisema suala la upungufu wa maji ya kuzalisha umeme limesababisha kushuka kwa kiasi kikubwa kiwango cha kuzalisha umeme kutoka MGW 591 mpaka kufikia MGW 80.
Alisema, suluhisho la changamoto hiyo ni uwepo wa gesi asilia ambapo kupitia mradi huo, unaifanya nchi isimame katika uchumi wa kati ambao ungeweza kuporomoka kama jitihada za ujenzi wa bomba la gesi zisingefanyika na kukamilika kwa wakati.
“Mhe. Rais, dhamira ya serikali ni kuhakikisha kwamba gesi asilia inapatikana kwa ajili ya kuzalisha umeme, na wananchi wengi zaidi kupata gesi kwa matumizi ya majumbani na viwandani..ni wazi kwamba matumizi haya ya gesi asilia yataongeza kasi ya ukuwaji uchumi kwa mtu mmoja mmoja na serikali kwa ujumla..” alisema.
Awali akitoa taarifa ya mradi huo, mkurugenzi wa TPDC, James Mataragio, alisema utekelezaji wa mradi huo ulianza miaka mine iliyopita na ujenzi wake ulitokana na mkopo wa masharti nafuu kutoka benki ya Exim ya nchini China, ambapo mpaka unakamilika umegharimu fedha kiasi cha dola za kimarekani bilioni 1.33 ambazo ni sawa na sh. Trilioni 2.926 za kitanzania.

“Kazi za ujenzi zimeendelea kwa kasi kubwa, na mpaka unazindua mradi huu wa miundombinu hii ya Madimba na bomba la kutoka Mtwara hadi Dar es Salaam umekamilika kwa asilimia 100 na tayari majaribio yamekwishafanyika na sasa gesi inasafirishwa kwenda Kinyerezi tayari kwa kuzalisha umeme..” alisema.

No comments: