Na Juma
Mohamed.
MGOMBEA
Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Chama cha Ukombozi wa Umma
(CHAUMMA), Hashim Rungwe, amesema serikali ya Chama Cha Mapinduzi (CCM)
imechoka kiasi cha kushindwa kuinua hali duni walizonazo wananchi kwa kipindi
cha zaidi ya miaka 50.
Akizungumza
juzi mkoani hapa katika mkutano wa hadhara wa kunadi sera za chama na kuomba
kura kwa wananchi, alisema CCM ni sawa na betri iliyoisha ‘chaji’ kutokana na kukosa
nguvu na mbinu za kuwafanya wananchi waishi maisha bora huku kukiwa na
rasilimali nyingi za kuinua uchumi.
Alisema,
iwapo wananchi watamchagua kuwa Rais, atahakikisha kunajengwa viwanda vya
kusindika nyama, kutengeneza nguo ambazo zitawafanya watu waache kuvaa mitumba
pamoja na viwanda vya kutengeneza magari.
“Jamaa
mwingine alikuwa ananiuliza mimi eti nitajenga viwanda hela nitapata wapi,
nikamwambia muulize mzee aliyetangulia ela alitoa wapi..hela ipo wasiwadanganye
mbona wananunua mabaluni yale..mimi nauza magari, si mnajua kuwa biashara yangu
ni kuuza magari..leo mnawafundisha watanzania kuuza magari haya yaliyotumiwa na
wenzetu sisi hatuna uwezo wa kutengeneza magari, ila mkinipa mimi tunatengeza
magari hapa..” alisema.
Hashim Rungwe |
Alisema,
Tanzania kuna watu wenye uwezo mkubwa na vipaji ambavyo vinaweza kuwafanya waunde bidhaa mbalimbali yakiwemo magari, na kwamba hawana tofauti na watu wa
Japani ambako ni maarufu kwa utengenezaji wa magari.
Aliwataka
wananchi kumpigia kura za Urais na kuachana na kuichagua CCM huku kura za
Udiwani na Ubunge wawapigie vyama vingine vya upinzani na kuwasihi kuto pigia
chama kimoja na baadala yake wachaguwe wabunge wa vyama mbalimbali ili kutoa
ushindani wa kweli bungeni.
“Msije
mkakipa chama kimoja wabunge wote, timu lazima iwe ‘combine’..tumeona jeuri ya
CCM kule bungeni wakati mimi nagombea bunge la katiba, walinibana huku na huku
wanatumia uwingi..hakuna mbunge wa chama kimoja akake pekeake bungeni
hatutaki..nataka mchanganyiko, CHADEMA kidogo, NCCR kidogo, CUF kidogo, CHAUMMA
kidogo tunataka mchanganyiko..” alisema.
Hashim Rungwe |
Awali,
mwenyekiti wa chama hicho mkoa wa Mtwara, Fatuma Selemani, alisema wameacha
kusimamisha wagombea wa Udiwani na Ubunge kwasababu wanaunga mkono muungano wa
vyama vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (UKAWA).
Alisema,
kutokana na adha waliyoipata Wanamtwara wakati wa vurugu za gesi, ambazo
CHAUMMA wanaamini zilichangiwa kwa kiasi kikubwa na serikali iliyopo madarakani
ya CCM, wameona kuna haja ya kuungana UKAWA kuweza kuwaondoa madarakani.
“Kwahiyo
sisi CHAUMMA pamoja na viongozi wangu wa kitaifa wameliona hilo pamoja na
kukumbuka adha ya Mtwara..walikuwa wanaona tulivyokimbia lakini viongozi hawa
mmoja alikuja lakini alishindwa kufanya mkutano kwasababu ya kufukuzwa na watu
hawajatulia wakangoja mpaka watulie..” alisema.
Naye,
mgombea mwenza wa chama hicho, Issa Habasi Hussein, alitaja vipaumbele vya
chama hicho kuwa ni pamoja na ajira, afya kutolewa bure kwa wananchi, kutoa
mikopo kwa wafanya biashara wadogo ambayo haitakuwa na riba, pamoja na kutoa elimu
bure kuanzia darasa la kwanza mpaka chuo.
No comments:
Post a Comment