Mgombea Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Mhe. Edward Lowassa, akihutubia maelfu ya wakazi wa Mbeya. |
Mgombea urais kupitia Chama cha
Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Edward Lowassa, amesema akiingia madarakani
baada ya uchaguzi mkuu Jumapili ijayo atafuta misamaha yote ya kodi isiyokuwa
na tija ili fedha zitakazopatikana zitumike kusomesha bure kila mtoto kuanzia
chekechea hadi chuo kikuu.
Akizungumza katika mkutano wake wa kampeni uliovutia maelfu ya
watu kwenye viwanja vya Luandanzovwe jijini Mbeya, jana, Lowassa anayeungwa
mkono pia na vyama vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) vya Chama
cha Wananchi (CUF), NLD na NCCR-Mageuzi, alisema mwaka jana peke yake, serikali
ilisamehe kodi yenye thamani ya zaidi ya Sh. trilioni 1.6 huku bajeti ya elimu
nchini kote ikiwa ni Sh. trilioni 1.4.
Alisema akichaguliwa na kuingia madarakani, atahakikisha kodi
hiyo inakusanywa na kutumika kwa maendeleo ya Watanzania.
"Serikali ikusanye hizo kodi halafu inipe mimi Sh. trilioni
1.4 ili niendeshe elimu nchini,"alisema.
Kadhalika, Lowassa alisema kupitia makusanyo mazuri ya kodi na
pia kutumia vyema rasilimali zilizopo nchini, atazibadilisha hospitali za
wilaya zote kuwa za rufaa ili kuboresha afya na pia kumaliza kero wanayoipata
sasa kina mama kwa kutembea umbali mrefu kwa ajili ya kutafuta huduma hizo.
MAPOKEZI MAKUBWA
Kabla ya mkutano wake jijini Mbeya, Lowassa alipata mapokezi ya
kifalme huku baadhi ya wananchi wakijitolea kufagia na kudeki barabara kama
ilivyokuwa Musoma, mkoani Mara wiki iliyopita.
Msafara wa mgombea huyo ulianzia kwenye uwanja wa ndege wa
zamani hadi kwenye viwanja vya Luandanzovwe vilivyopo Ilomba. Msafara huo wa
Lowassa ulivutia maelfu ya watu na kusababisha barabara kuu itokayo Iringa hadi
Mbeya kufungwa kwa muda huku polisi wakiwa na kazi kubwa ya kuwapanga vyema
wananchi barabarani ili msafara huo upate nafasi ya kusogea.
Aidha, wakati mkutano wa Lowassa ukiendelea, zaidi ya watu 10
walionekana kuzimia kutokana na kukosa hewa na kusaidiwa na madaktari kadhaa,
wakiwamo waliokuwa katika msafara wa Lowassa.
SUGU ATAKA MAJI, UMEME
Mgombea ubunge wa Mbeya Mjini, Joseph Mbilinyi, alimuomba
Lowassa kutatua suala la maji na umeme iwapo atachaguliwa kuwa rais. Pia,
alisema Mbeya inahitaji hospitali yake kuwa na kipimo cha CT Scan ili wananchi
wasihangaike kuifuata huduma hiyo mbali.
Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe, alisema iwapo serikali ya
awamu ya tano itaingia madarakani, watahakikisha katiba mpya inayoridhiwa na
Watanzania inapatikana baada ya serikali ya CCM kushindwa kutimiza dhamira
hiyi.
Aidha, aliwataka wananchi kusimamia na kulinda kura zao
kwa sababu tume ya uchaguzi iliyopo siyo huru na ya haki.
Alisema sheria nyingine zimepitwa na wakati kwa sababu vituo
vingine vipo kwenye makazi ya wananchi.
Pia, aliwaomba askari na vyombo vya usalama kusimamia uchaguzi
huo kwa amani.
"Askari wetu tunawapenda na kuwaheshimu, simamieni haki...
na mimi nawaambia wananchi hakuna sababu ya kufanya fujo ila simamieni
haki," alisema na kuongeza.
Alisema wizi wa kura unaanza kuanzia mkesha wa siku ya uchaguzi
kwani CCM watakuwa wanazunguka mitaani kugawa fedha.
KINGUNGE
Aliyekuwa kada mkongwe wa CCM, Kingunge Ngombali Mwiru, alisema
CCM aliyoshiriki yeye (Kingunge) kuiasisi siyo CCM ya sasa.
"Viongozi wa CCM wa sasa wamevunja katiba, hawaheshimu
katiba yao wenyewe, hawaheshimu taratibu zao wenyewe, wameamua kubinafsisha
chama chao wenyewe.
"Sasa hivi CCM imekuwa ni mali ya viongozi wachache,
wanafanya wanayoyataka wenyewe, wanawadhalilisha wenzao,"alisema.
Alisema anaijua CCM na ameitumikia vya kutosha lakini ilibidi
aachane nayo kwa sababu si chombo cha kuleta maendeleo kwa Watanzania kwani
sasa imechoka.
"Unaposhindwa mzigo inabidi uwaachie wenye nguvu waubebe
ambao ni Ukawa chini ya Lowassa,"alisema.
SUMAYE
Waziri Mkuu Mstaafu, Frederick Sumaye alisema CCM lazima iondoke
madarakani kwa sababu imevunja mkataba na wananchi.
"CCM walitakiwa wajiulize kama wamewatimizia watanzania
yale waliyowaahidi kuliko kuendeleea kupiga kelele,"alisema.
Alisema CCM wanatakiwa kujibu hoja na wala si kupanda majukwaani
na kuanza kumtukana Lowassa.
Jana, Lowassa alifanya mikutano Mbarali, Chunya, Songwe na Mbeya
mjini.
SOURCE: NIPASHE
No comments:
Post a Comment