Thursday, September 3, 2015

Nanauka: UKAWA watoe tamko haraka jimbo la Mtwara mjini ili kulinusuru.

Mgombea ubunge jimbo la Mtwara mjini kupitia Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Joel Nanauka, akiongea na waandishi wa habari leo, kuelezea misimamo na mapendekezo yake juu ya jimbo hilo.




Na Juma Mohamed.

MGOMBEA ubunge katika jimbo la Mtwara mjini kupitia Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Joel Nanauka, amewataka viongozi wakuu wa vyama vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (UKAWA), kutoa tamko haraka juu ya hatma ya jimbo la Mtwara mjini ili kuhepuka kuwagawa wananchi.
Alisema kama tayari mgombea ameshapatikana basi ni vyema akatangazwa ili aungwe mkono na wagombea wengine wa Umpja huo, na kwamba kitendo cha kukaa kimya huku muda unazidi kwenda, ni kuto watendea haki wananchi ambao wanakiu kubwa ya kutaka kumjua mgombea wao.
“Kama amepatikana, hakuna haja ya kuendelea na migogoro wala majadiliano, tamko litolewe na mtu atangazwe ili tupate kumuunga mkono..na ningependa kutoa wito kwa wagombea wanaowakilisha CUF (Chama cha Wananchi) na NCCR, hakuna sababu ya kuendelea majadiliano kwenye swala la kuamua nani anataka kufanya, na ningependa kuwaomba viongozi wa kitaifa walisimamie na watoe tamko kwa haraka ili wasiendelee kuwagawanya watu, na kuwakosesha yale matumaini ambayo walikuwa nayo kwa muda mrefu..” alisema.
Alisema anapopita mitaani anaona kuwa matumaini ya wananchi yanazidi kufifia na wanakata tamaa kwa kuona kama watu wanagombea vyeo, jambo ambalo ni kinyume na falsafa ya umoja huo ambao una lengo la kuwa na kiongozi mahiri atakae wawakilisha vyema wananchi.
Aidha, aliwataka wananchi kuendelea kuwa na matumaini na umoja huo na kuendelea kutunza vitambulisho vyao kwa ajili kupiga kula mwezi Oktoba wakati wa uchaguzi, huku akiendelea kusisitiza msimamo wake wa kumuunga mkono mgombea yeyote atakaeidhinishwa na UKAWA.
“Nataka nione Wanamtwara wananufaika, na ili wanufaike ni lazima tuweke masilahi yetu bianfsi pembeni..kwahiyo mimi kama mgombea CHADEMA nimesema wazi kwamba kama ikionekana mgombea wa CUF ndio anakubalika na ana uwezo nitamuunga mkono na ni hivyo hivyo kwa NCCR…mimi siko tayari kufanya kampeni kwa vyama vitatu, yani CHADEMA, NCCR na CUF, ikitokea hivyo msimamo wangu ni kwamba sito gombea na nitaendelea kutoa mchango wangu nikiwa nje..” alisema.
Aliongeza kuwa, bado ataendelea kubaki na misimamo yake hata ikitokea inaenda tofauti na matakwa na viongozi wake wa wilaya na hata mkoa japo bado hajasikia tamko lolote kutoka kwao, huku akiwasisitiza wananchi kupiga kura ya mabadiliko uchaguzi ukifika.

No comments: