Thursday, September 3, 2015

Wachezaji Ndanda Sc wagomea mazoezi kudai mishahara.


Kikosi cha timu ya Ndanda Sc msimu wa 2014/2015


Msemaji wa timu ya Ndanda Sc ya mkoani Mtwara, Idrissa Bandari akizungumza na waandishi wa habari juu ya ukata unaoukabili timu hiyo kiasi cha kushindwa kuwalipa mishahara wachezaji ambao wameamua kugomea mazoezi jana kushinikiza kulipwa mishahara yao.


Idrissa Bandari


Na Juma Mohamed.

Wachezaji wa timu ya soka ya Ndanda Sc ya mkoani hapa wamegomea kufanya mazoezi kutokana na kuto lipwa mishahara yao, ikiwa ni wiki moja kabla ya kuanza kwa michuano ya ligi kuu ya Tanzania Bara.
Akizungumza na waandishi wa habari jana, msemaji wa timu hiyo, Idrissa Bandari, amesema hali hiyo inatokana na timu kukumbwa na ukosefu wa fedha ambapo wapo wachezaji wanaodai mishahara ya miezi miwili na wengine mwezi mmoja.
“Tumeanza ukata huu mapema sana msimu huu..kwasababu timu haina hela na leo vijana hawajafanya mazoezi asubuhi na jioni hatuna mazoezi, vijana wale wanadai mishahara yao na sisi hatuna fedha, lazima tuwe wakweli..sasa tuwaomba, tunapokwenda kupeleka barua sehemu za kuomba udhamini, ni ngumu sana kuenda Idrissa au kiongozi wa Ndanda akapata zile fedha, lazima tupate ‘support’ ya mtu ambaye anaweza akaenda hiyo sehemu na akazungumza na wale watu wakakubali kutokana na hadhi yake..” alisema.
Alisema benchi la ufundi limejitahidi kusajili wachezaji wazuri msimu huu ukilinganisha na msimu uliopita, lakini iwapo hali hiyo itaendelea, wananchi wa Mtwara wasitarajie makubwa kutoka kwa timu hiyo ambayo bajeti yake ni sh. Bilioni 1 kwa msimu nzima huku hata ikipatikanai kiasi cha sh. Milioni 500 inaweza kuwasaidia kuiendesha.
“Swala la mshahara ni swala kubwa sana na ni haki yao kudai, sisi kama tunapata Milioni 500 leo tunaweza kuiendesha ile timu vizuri kabisa kwasababu tutakuwa tumeweza kutatuwa mahitaji yote muhimu..wachezaji asubuhi walieleza tu ukweli na kama binaadamu au kama kiongozi inafikia hatua unaguswa na hoja zao..wana matatizo watayalizaje nyumbni kwao.” Alisema.


Mlinzi wa Ndanda, Azizi Sibo, akijaribu kuwadhibiti washambuliaji wa timu ya Azam, katika mechi ya kirafiki ya tamasha la siku ya Ndanda (Ndanda Day). Mchezo ulimalizika kwa kufungana bao 1-1

Idrissa alisema, amelazimika kuzungumza hayo na vyombo vya habari ili wananchi wa Mtwara wafahamu kwamba bado timu yao ina matatizo na kwamba hawapaswi kulaumiwa kwa namna yeyote kwa matokeo au mwenendo nzima wa timu hiyo ukiwa tofauti na matarajio yao pindi ligi itakapoanza.
Aidha, ametowa wito kwa serikali ya mkoa na wadau wengine kujitolea kwa hali na mali kuweza kuisaidia timu, kwa kushawishi kampuni na mashirika mbalimbali yaliyopo mkoani humo kama ambavyo inafanyika katika mikoa ambayo ina kampuni za uwekezaji.

“Niwaombe sana watu wa Mtwara wenye nia na mapenzi mema na timu ya Ndanda..hali ya timu ni mbaya, na tusidanganyane kuiendesha timu kwa kuomba michango, timu ya Ligi haiendeshwi hivyo, inaendeshwa kwa udhamini pamoja na bajeti yake ambayo inatengwa, lakini sisi hatuna hiyo fedha..hali ya Mtwara inajulikana, tuna makampuni mengi kama watu wanajitolea kutusaidia wale ambao wananguvu na sauti zao zina nguvu, wakaenda kwa hawa watu kuwaona tunaweza tukapata msaada mkubwa sana..” alisema.

No comments: