Friday, August 28, 2015

Kushuhudia kipute cha Ndanda Sc vs Azam Fc ni buku 5..huku waandishi wa habari za michezo wakiahidiwa vitambulisho


Mwenyekiti wa Chama cha Soka Mkoa wa Mtwara (MTWAREFA), Athumani Kambi, akizungumza na waandishi wa habari leo juu ya maswala ya Ndanda Fc na maandalizi ya mchezo wa kirafiki wa kuadhimisha siku ya Ndanda (Ndanda Day).




Athumani Kambi na waandishi wa habari wa mkoa wa Mtwara, baada ya kumaliza mazungumzo juu ya maswala ya Ndanda Sc.

Na Juma Mohamed, Mtwara

Mashabiki wa soka mkoani Mtwara na mikoa jirani wametakiwa kujitokeza kwa wingi uwanjani katika mchezo wa kirafiki kati ya Ndanda Sc na Azam Fc utakaopigwa kesho katika uwanja wa Nangwanda Sijaona.
Akizungumza na waandishi wa habari leo, mwenyekiti wa Chama cha Soka mkoani humo Athumani Kambi, amesema mchezo huo ni sehemu ya maadhimisho ya siku ya Ndanda ( Ndanda Day), lengo likiwa ni kuwatambulisha wachezaji wapya ambapo viingilio vitakuwa ni sh. 10,000, 7,000 na 5,000.
“Lakini dhumuni la pili tunaichukulia Ndanda Day kama sehemu mojawapo ya kuichangia timu yetu ya Ndanda, kwahiyo tungeoma watu wajitokeze kwa wingi mjini na sehemu nyingine..hivyo viingilio labda watu watasema tumeweka hela nyingi lakini sio hivyo, tumeweka hivyo kwasababu tunataka watu wachangie timu yetu ya Ndanda, kwahiyo watu wajue kwamba wataangalia mpira huku wanachangia timu..” alisema.
Aliongeza kwa kuendelea kusisitiza juu ya wadau kujitokeza kuisaidia timu hiyo ambayo ndio timu pekee inayowakilisha mkoa wa Mtwara katika ligi kuu, ambapo alisema kila mtu mchango wake unahitajika na utapokelewa kwa kile atakachotoa akisisitiza kwamba hata wanasiasa wanakaribishwa.
Alisema timu hiyo siyo ya wanasiasa lakini wanasiasa hawazuiliwi kuisaidia kwasababu wapo ambao tayari walishatoa misaada yao huku akisisitiza pia kwa wafanyabiashara na hata serikali ya mkoa na kampuni zilizopo mkoani hapa.
Aidha, amesema juhudi zinafanyika ili kuhakikisha kuanzia msimu huu wa ligi kuu itakapoanza wawakilishi wa vilabu hawatoruhusiwi kukusanya mapato mlangoni katika uwanja huo na baadala yake kutakuwa na utaratibu mwingine ambao utatangazwa, ili kudhibiti upotevu wa mapato.
“Tutakapoanza ligi nadhani kutakuwa na aina nyingine na sio ile ya mwaka jana ya kuweka vilabu kukusanya mapato, wao watakuwa wanakaa pale kuangalia tu kama mambo yanaenda sawa lakini mtu wa klabu hatutaruhusu kusimama mlangoni, iwe Yanga au Simba..kwasababu tumeona watu wengi wa vilabu wanaokaa pale wanachangia kuvujisha mapato..” alisema.

 Wakati huo huo Kambi amewaahidi waandishi wa habari za michezo wa mkoani hapa  kutengenezewa vitambulisho maalumu watakavyovitumia katika kutekeleza majukumu yao ya kutafuta na kuandika habari za michezo na kuingilia uwanjani wakati wa michezo ya ligi kuu ya Tanzania Bara itakayochezwa katika uwanja wa Nangwanda Sijaona.
Alisema, maamuzi hayo ni kuwaondolea usumbufu wanahabari hao hasa katika michezo ya Ligi Kuu ambapo kumekuwa na malalamiko ya kuzuiwa milangoni wanapohitaji kuingia uwanjani hasa kutoka kwa wafuasi wa timu ngeni ambao hawawatambui waandishi wa Mtwara.
Aliwataka waandishi hao kuwasilisha picha ndogo (Passport Size) kwa ajili ya kutengeneza vitambulisho hivyo.



No comments: