Na Juma
Mohamed, Mtwara.
SERIKALI
itaokoa kiasi cha dola za kimarekani bilioni 1 kwa mwaka zinazotumika kwa
kuagiza mafuta kutoka nje baada ya kuanza kuzalisha umeme kwa kutumia gesi
asilia kutoka katika kiwanda cha kuchakata rasilimali hiyo cha Madimba, mkoani
hapa.
Hayo
yamezungumzwa juzi na meneja mradi wa kiwanda hicho Leonce Mrosso, alipokuwa
akizungumza na waandishi wa habari wa mikoa ya Mtwara, Lindi na Dar es Salaam
baada ya kutembelea kiwandani hapo kama sehemu ya somo wakiwa katika mafunzo ya
siku mbili ya kujifunza kuandika habari za rasilimali za mafuta na gesi
yaliyoandaliwa na Baraza la Habari Tanzania (MCT).
Alisema
licha ya kuokoa kiasi hicho cha fedha kupitia rasilimali hiyo ambayo uzalishaji
wake unakadiriwa kuanza kati ya Septemba 15-20 mwaka huu,kutakuwa na faida
nyingine kwa taifa ambazo ni kuwa na umeme wa uhakika na kuongezeka kwa viwanda
ambavyo vitaliingizia taifa mapato.
“Faida za
rasilimali hii ni nyingi sana..kwasababu hiki kiwanda baada ya kuchakata gesi
sasa kutakuwa na mabaki yale ambayo yenyewe ni faida vilevile kwasababu
yatatumika kwa kutengeza vitu vingine kama plastiki..lakini nchi yetu haitakuwa
na tatizo tena la umeme na hata viwanda vitaongezeka kwasababu watu watakuja
kuwekeza zaidi kwa ajili ya kufuata umeme wa uhakika..” alisema.
Aliongeza
kuwa, upatikanaji wa maji kwa wakazi wa eneo linalozunguka mradi ni faida
nyingine inayotokana na rasilimali hiyo huku akisema mpaka sasa ni kijiji cha
Madimba pekee kinachopata maji na kwamba juhudi ya kuvifikia vijiji vingine
zinafanyika.
Aidha,
alisema zoezi linaloendelea sasa kiwandani hapo ni kuijaribu mitambo kabla ya
kuanza kuisukuma gesi kuipeleka Kinyerezi, ikiwa ni wiki moja baada ya kufungua
gesi hiyo kutoka katika visima viwili kati ya vitano vilivyopo Msimbati.
Alisema
kiwanda hicho kinauwezo wa kuzalisha gesi futi za ujazo milioni 210 kwa siku
huku bomba linalotoka kiwandani hapo kwenda Kinyerezi lenye urefu wa km 487 na
inchi 36, linauwezo wa kusafirisha gesi yenye futi za ujazo 784 kwa siku, hivyo
hakuna uwezekano wa gesi kuisha kwenye bomba.
Alisema
asilimia 95 za fedha za ujenzi wa mradi huo ambao umegharimu kiasi cha dola za
kimarekano bilioni 1.33 ni za mkopo kutoka katika benki ya Exim ya nchini China
huku fedha za serikali ikiwa ni asilimia 5 iliyobaki.
Awali
akizungumza katika ufunguzi wa mafunzo, katibu wa MCT, Kajubi Mukajanga,
aliwataka waandishi wa habari kubadilika katika uandishi hasa katika kuandika
habari zinazohusu masuala ya uziduaji, na kuuliza maswali kwa ajili ya kupata
undani wa jambo na kuepuka kuandika taarifa kama inavyotolewa na mtoaji.
“Kila nyumba
itakuwa na mabomba mawili, moja la maji lingihe la gesi..na sisi tunaandika tu
hivyo hivyo hatuulizi nini kitatakiwa ili hali hiyo iweze kutokea, hatuulizi
itawezekanaje katika mazingira ambayo Tandale hata hilo bomba la maji lenyewe kupitisha
mpaka kufika nyumbani kwako ni mbinde..” alisema.
Alisema
lengo la mafunzo hayo ni kumfanya mwandishi aweze kuuliza maswali ya nyongeza
kwa chanzo chake na kuto ridhika na maelezo yanayotolewa kwa kuamini kuwa
yamejitosheleza.
No comments:
Post a Comment