KAMATI
ya Utendaji ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) imeridhia mapendekezo ya Kamati
ya Mashindano ya kutaka Ligi Daraja la Kwanza (FDL) kuwa na timu 20 badala ya 18
za sasa.
Ofisa Habari wa Shirikisho la
Soka Tanzania (TFF), Boniface Wambura Mgoyo ameiambia BIN
ZUBEIRY jioni hii kwamba, lengo la mabadiliko hayo ni Ligi ya Taifa (NL)
kuchezwa kwa kanda, hivyo msimu huu timu mbili zaidi (ukiondoa tatu ambazo
zimeshapanda kutoka NL) zitaongezwa ili kufikisha idadi ya timu 20 katika
FDL.
Amesema timu ambazo zimepanda
kutoka NL iliyochezwa katika vituo vitatu ni; Kanembwa JKT ya Kigoma iliyoongoza
Kituo cha Kigoma, Ndanda SC ya Mtwara iliyoibuka kinara Kituo cha Mtwara na
Polisi Mara iliyokamata usukani katika Kituo cha Musoma.
Amesema Kamati ya Utendaji pia
imepitisha mapendekezo ya kuchezwa play off ili kupata timu mbili zaidi za
kucheza FDL msimu huu.
Amesema timu zitakazocheza
play off katika utaratibu utakaotangazwa baadaye na Kamati ya Mashindano ni tatu
zilizoshuka kutoka FDL na tatu nyingine zilizoshika nafasi za pili katika NL
kutoka vituo vya Kigoma, Mtwara na Musoma.
Amezitaja timu tatu
zilizoshuka FDL ni AFC ya Arusha, Samaria ya Singida na Temeke United ya Dar es
Salaam wakati zilizoshika nafasi za pili katika NL na vituo vyao kwenye mabano
ni Kurugenzi ya Iringa (Mtwara), Mwadui ya Shinyanga (Kigoma) na Tessema ya Dar
es Salaam (Musoma).
Hata hivyo, timu zitakazoshuka
kutoka Ligi Kuu bado zitaendelea kuwa tatu kama ilivyo kwa
zitakazopandwa.
USAJILI BARA KUFUNGWA AGOSTI 10, SIMBA AZAM KUCHEZA NGAO AGOSTI 25
Danny Mrwanda amesaini Simba SC |
KIPINDI
cha kwanza cha usajili wa wachezaji kwa ajili ya msimu wa 2012/2013 kitamalizika
Agosti 10 mwaka huu kulingana na kalenda ya Matukio ya Shirikisho la Mpira wa
Miguu Tanzania (TFF) ya 2012/2013.
Ofisa Habari wa Shirikisho la
Soka Tanzania (TFF), Boniface Wambura Mgoyo ameiambia BIN
ZUBEIRY jioni hii kwamba, uhamisho wa wachezaji unafanyika kuanzia Juni
15 hadi Julai 30 mwaka huu wakati kipindi cha kuacha wachezaji (sio wa Ligi Kuu.
Wachezaji wa Ligi Kuu wanacheza kwa mikataba) ni kuanzia Juni 15- 30 mwaka
huu.
Amezitaka klabu za Ligi Kuu
kutangaza wachezaji watakaositishiwa mikataba yao ni kuanzia Juni 15-30 mwaka
huu na usajili wa wachezaji unafanyika kuanzia Juni 15 hadi Agosti 10 mwaka
huu.
Frank Damayo amesaini Yanga SC |
“Tunasisitiza kipindi cha
usajili kiheshimiwe na mikoa yote kwa sababu usajili huo huo ndiyo utakaotumika
katika michuano ya Kombe la FA. Kwa maana nyingine hakutakuwa na kipindi kingine
cha usajili wa wachezaji kwa klabu zote nchini hadi hapo litakapofunguliwa
dirisha dogo,”amesema.
Mechi ya kufungua msimu ya
Ngao ya Jamii (Community Shield) kati ya mabingwa wa Ligi Kuu, timu ya Simba na
makamu bingwa Azam itachezwa Agosti 25 mwaka huu wakati Ligi Kuu itaanza
Septemba Mosi mwaka huu, na Ligi Daraja la Kwanza (FDL) yenyewe itaanza Septemba
15 mwaka huu.
Ratiba ya Ligi Kuu itatolewa
Julai 23 mwaka huu.
MAFARAO WADOGO WAOMBEWA MECHI NA NGORONGORO
Thomas Ulimwengu, mshambuliaji wa Ngorongro |
CHAMA
cha Soka Misri (EFA) kimeomba mechi mbili za kirafiki kwa timu yao ya vijana na
timu ya vijana wenye umri chini ya miaka 20 ya Tanzania (Ngorongoro
Heroes).
Ofisa Habari wa Shirikisho la
Soka Tanzania (TFF), Boniface Wambura Mgoyo ameiambia BIN ZUBEIRY
jioni hii kwamba, EFA imeomba mechi hizo zichezwe Julai 3 na Julai 5 mwaka huu
kwa masharti maalumu. Ikiwa zitachezwa Misri, mwenyeji (EFA) atagharamia
Ngorongoro Heroes kwa malazi, chakula, usafiri wa ndani na sehemu ya kufanyia
mazoezi.
Amesema ikiwa mechi hizo
zitachezwa Dar es Salaam, Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF)
litaigharamia timu ya Misri kwa malazi, chakula, usafiri wa ndani na sehemu ya
mazoezi. Hivyo, amesema kila timu itajigharamia kwa usafiri wa ndege na posho
kwa timu yake.
“Sekretarieti ya TFF inafanya
uchambuzi wa gharama ili kujua ipi ni nafuu kabla ya kufanya uamuzi wa wapi
mechi hizo zichezwe”amesema.
Ngorongoro Heroes imeingia
raundi ya pili ya michuano ya Afrika ambayo fainali zake zitafanyika mwakani
nchini Algeria baada ya kuitoa Sudan katika raundi ya
kwanza.
Itacheza mechi ya kwanza ya
raundi ya pili Julai 28 mwaka huu jijini Dar es Salaam wakati ya marudiano
itakuwa Agosti 11 mwaka huu nchini Nigeria
No comments:
Post a Comment