Thursday, May 31, 2012

LIVERPOOL IMECHEZA BONGE LA KAMARI KWA BRENDAN RODGERS


Brendan Rodgers, applauding
31 May 2012Last updated at 06:49 GMT

Hayo ni maneno ya beki wa zamani Liverpool, Mark Lawrenson

BEKI wa zamani wa Liverpool, Mark Lawrenson anaamini kuajiriwa kwa kocha Brendan Rodgers katika Uwanja wa Anfield ni bonge la kamari.
Rodgers, ambaye aliiongoza Swansea kushika nafasi ya 11 kwenye Ligi Kuu msimu uliopita, anasaini mkataba wa miaka mitatu Liverpool.
"Ni bonge la kamari kwa kuteuliwa kwake na kamari kubwa ambayo klabu haijawahi kucheza kwa muda mrefu," alisema Lawrenson.
"Mashabiki wa Liverpool watampa nafasi. watampa muda. Lakini kama timu haitamaliza ndani ya nne bora, wamiliki watafanyeje?"
Rodgers amewahi kuzifundisha Reading na Chelsea kabla ya kwenda Watford Novemba mwaka 2008.
Alipoulizwa kuhusu sifa za kocha huyo mwenye umri wa miaka 39, Lawrenson alisema: "Rodgers amefanya kazi nzuri akiwa Swansea, kila mmoja anapenda jinsi wanavyocheza soka yao.
"Nafasi ya Brendan kuongoza klabu ambayo ipo ndani ya 10 bora nchini ipo juu ya uwezo wake. Ni changamoto tofauti kwake, klabu itatarajia kushinda kila mechi.
"Liverpool ilitumia fedha nyingi katika usajili msimu uliopita, hakuna shaka watatumia fedha nyingi zaidi. Ni kazi kubwa kwa Rodgers, kwa sababu atawajibika kwa kila kitu kama ilivyo hakuna Mkurugenzi wa Michezo,"alisema.

INGEKUWA VIPI NYOSSO, JABU, MWAIKIMBA NA REDONDO BILA ASHANTI, JE WANGETOKA?

Hapa ndio makao makuu ya klabu ya Ashanti inayopigania kurejea Ligi Kuu. Hii ni klabu ambayo imeibua wachezaji wengi wanaotamba katika Ligi Kuu hivi sasa kama Juma Nyosso, Ramadhan Chombo 'Redondo', Gaudence Mwaikimba, Juma Jabu, Ally Mustafa 'Barthez' na wengineo.


WABUNGE WA CHADEMA WAAGWA KWA MTANANGE WA BRAZIL NA MAREKANI


Baaada ya kazi kubwa ya kuzindua na kuimarisha tawi la chadema Washington Dc Maryland na Virginia,Wabunge wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA)Mhe. Peter Msigwa na Mhe. Nassari Joshua, Al-Marufu Dogo janja, Usiku wa Jana Jumatano Mei 30,2011 waagwa rasmi kwa kuangalia mpambano wa kimataifa kati ya US na Brazil ndani ya uwanja wa Fedex, uliopo Landover Maryland Nchini marekani
Wabunge wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) Mhe, Peter Msigwa na Mhe. Nassari Joshua, Al-Marufu Dogo janja, wakiwa na uwongozi wa tawi la Chadema Washington Dc Libe Mwangombe, wanne, Mjomba a.k.a Cosmas, Mzee wa swahilivilla Aboh Shatry wa pili kulia, pamoja na mashabiki wa US, wakiiunga mkono bendera ya taifa. (Picha maelezo na swahilivilla.blog spot.com)

Idadi ya wapenzi waliohudhuria katika mpambano huo ni 67,656 wakiwemo Mhe. Nassari Joshua pamoja na Mhe, Peter Msigwa. (Picha maelezo na swahilivilla.blog spot.com)

Wabunge wa chama cha Chadema wakipata flash ya pamoja na warembo wa Kibrazil ndani ya uwanja wa FedexField, uliopo Landover Maryland Nchini marekani. (Picha maelezo na swahilivilla.blog spot.com)

Picha ya pamoja na viongozi wa juu wa Chadema kwenye mpambano wa US na Brazil Usiku wa kuamkia leo Alhamis Mei 31,2012 ndani ya ndani ya uwanja wa Fedex, uliopo Landover Maryland Nchini marekani
Nabendera ya Taifa wakishangilia Bao la kwanza la Brazil lilifungwa kwa Penalti na mchezaji Neymar
Wachezaji wa Brazil wakilinda ngome yao kwa kuwadhibiti timu ya US kwenye mechi hiyo ya kirafiki ambapo timu ya Brazil waliweza kuwabamiza US bao 4-1 nyumbani kwao.
US. hoi kwa Brazil baada ya kubamizwa bao nne bao la kwanza lilifungwa na Neymar, na lapili na Thiago mnamo wa dakika ya 11, kipindi cha kwanza. bao la US lilifungwa na Hercules Gomes dakika ya 44 kipindi chakwanza hadi mapumziko Brazil 2 US 1 kwenye mchezo wa kirafiki. (Picha maelezo na swahilivilla.blog spot.com)
Landon Donovan
Forward wa United States Landon Donovan, akipandisha majeshi juu huku alidhibitiwa na Brazil defender Marcelo wa Brazi katika mpambano wa kirafiki.
Hivyo ndivyo ilivyo katika uwanja wa FedexFeild, uliopo Landover Maryland Nchini Marekani (Picha maelezo na swahilivilla.blog spot.com).

TETESI ZA USAJILI BARA: MTIBWA, COASTAL ZAMGOMBEA KIUNGO FUNDI WA AZAM


KIUNGO wa Azam FC aliyecheza kwa mkopo msimu huu, African Lyon ya Dar es Salaam, Suleiman Kassim ‘Selembe’ amesema kwamba Coastal Union ya Tanga na Mtibwa Sugar ya Morogoro, ndizo ambazo hadi sasa zimeonyesha nia ya kumsajili, ila anapenda kukabiliana na changamoto kubwa zaidi, kama za Simba au Yanga.
Akizungumza na BIN ZUBEIRY visiwani Zanzibar leo asubuhi, Selembe (pichani kushoto) alisema kwamba klabu yake, Azam FC imeonyesha nia ya kumuacha aende klabu yoyote itakayomtaka na sasa naye anasikilizia timu ambayo itamalizana naye.
“Kwa kweli hadi sasa naweza kusema Coastal Union na Mtibwa ndizo ambazo zimeonyesha nia haswa ya kunisajili, ila mimi mwenyewe niko tayari kukabiliana na changamoto zozote, hasa zile kubwa kubwa, kama Simba au Yanga hivi, niko tayari,”alisema.
Selembe ni kati ya viungo wazuri kwa sasa nchini, ambaye ameyumba kidogo baada ya Azam kumpeleka kwa mkopo Lyon, kiasi cha kufikia kutemwa katika kikosi cha timu ya taifa ya Tanzania, Taifa Stars.
Kwa sasa, fundi huyo wa soka yuko kwenye kambi ya timu ya Zanzibar, inayojiandaa na michuano ya Kombe la Dunia ya nchi zisizo wanachama wa FIFA nchini Uzbekistan, michuano itakayoanza Juni 4, mwaka huu na Zanzibar Heroes inatarajiwa kuondoka Juni 2 nchini.
 

DROO YA TANO YA VUMBUA HAZINA CHINI YA KIZIBO YA SBL YAFANYIKA DAR LEO


Meneja wa kinywaji cha Serengeti Premium Lager Bw. Allan Chonjo akizungumza wakati wa kutangaza washindi wa Genereta na Bajaj katika bahati nasibu ya promosheni ya Vumbua Hazina chini ya Kizibo iliyofanyika kwenye ofisi za Kampuni hiyo Oysterbay jijini Dar es salaam kulia ni Tumainiel Malisa kutoka PWC.
Menejwa mawasiliano wa kampun i ya bia ya Serengeti Imani Lwinga akizungumza wakati wa kuchezesha bahati nasibu hiyo katikati ni Meneja wa bia ya bia ya Serengeti Premium Lager na kulia ni Tumainiel Malisa kutoka PWC
Meneja wa kinywaji cha Serengeti Premium Lager Bw. Allan Chonjo akizungumza wakati wa kutangaza washindi wa Genereta na Bajaj katika bahati nasibu ya promosheni ya Vumbua Hazina chini ya Kizibo iliyofanyika kwenye ofisi za Kampuni hiyo Oysterbay jijini Dar es salaam katikati ni Tumainiel Malisa kutoka PWC na kulia ni Abdallah Hemed kutoka bodi ya mchezo ya kubahatisha.

SOURCE: FULL SHANGWE
Zoezi la kukabidhi zawadi kwa washindi waliojitokeza kushiriki na kushinda zawadi zinazotolewa katika promosheni ya kipekee ‘VUMBUA HAZINA CHINI YA KIZIBO’ inayoendeshwa na kampuni ya bia ya Serengeti limeendelea wiki iliyopita katika mikoa ya Iringa na Mwanza ambapo mshindi wa jenereta na yule wa bajaj walikabidhiwa zawadi zao katika sherehe zilizohudhuriwa na umati mkubwa wa watu na kushuhudia SBL ikikabidhi zawadi hizo na kuamsha hamasa kubwa kwa wapenzi na watumiaji wa biadhaa za SBL.
Asubuhi ya leo droo ya tano ya promosheni hiyo ‘VUMBUA HAZINA CHINI YA KIZIBO’ imechezeshwa katika ofisi za kampuni ya bia ya Serengeti zilizopo maeneo ya Oysterbay jijini na kupata kuhudhuriwa na waandishi wa habari, wasimamizi kutoka Bodi ya Bahati Nasibu Tanzania, wadau kutoka ndani na nje ya kampuni hiyo, wakiwemo kampuni ya kuendesha Bahati Nasibu ya PUSH MOBILE na wahakiki na wakaguzi kutoka PWC-Price Water House Coopers.
Akiongea katika mkutano na waandishi wa habari wakati wa kuchezeshwa kwa droo ya tano ya promosheni hiyo, Mkurugenzi wa Masoko wa kampuni hiyo bw. Ephraim Mafuru, amesema “Tumeshakabidhi jereta nne kwa washindi mbalimbali na zawadi ya pikipiki, bajaj mbili na gari moja aina ya FORD FIGO ambapo zawadi zote zimeshakabidhiwa kwa washindi wetu . Hivi karibuni tutasafiri kwenda Mfinga Mkoani Iringa kukabidhi Bajaj”.
“Naendelea kuwashauri jamii na watanzania kwa ujumla kwamba promosheni hii ni kwa ajili ya kila mtanzania mwenye vigezo vya kushiriki kwa hiyo wajitokeze k kwa wingi kushiriki ili kujaribu bahati kama wenzetu ambao wamejaribu na kupata zawadi kubwa ambazo hawakutarajia katika maisha yao.” Alisema Mafuru.
Aliongeza kuwa zawadi zinazoshindaniwa gharama yake ni jumla fedha za kitanzania milioni 780 ikiwemo pesa taslimu ambazo mshindi anapata papo hapo kupitia matandao wa simu za mikononi M- pesa. Ikumbukwe kuwa zawadi hizi zinapelekwa hadi pale mshindi wetu alipo bila yeye kuchangia chochote walakugharamia chochote ikiwemo usafiri.
Katika droo hii ya tano mshindi ni Isaya Charles kutoka Igoma mkoani Mwanza ambaye amejishindia Jenereta, wakati mshindi mwingine Mariam Karumba mwanafunzi wa mwaka wa tatu Chuo Kikuu cha Saint Agustin pia anatoka mkoani Mwanza amejishindia Bajaj

Kampuni ya bia ya Serengeti kupitia bidhaa yake bora kabisa ya Serengeti Premium Lager, Tusker Lager and Pilsner inaendesha promosheni hii kwa wiki 16 ikiwa na lengo la kuinua na kuboresha maisha ya wateja wake na watanzania kwa ujumla

DK TAMBA AOMBWA KUGOMBEA UENYEKITI YANGA


Dk Tamba

WANACHAMA wa klabu ya Yanga, wakiwemo wazee kadhaa wa Dar es Salaam wamemuomba, mwanachama mwenzao maarufu, Dk. Maneno Tamba kujitokeza kuwania nafasi ya Uenyekiti wa klabu hiyo katika uchaguzi wa klabu hiyo, uliopangwa kufanyika Julai 15, mwaka huu.
Habari ambazo BIN ZUBEIRY imezipata kutoka kwa mtu wa karibu wa Dk. Tamba, zimesema kwamba wanachama wa klabu hiyo, walifika mapema Jumatatu wiki hii ofisini kwa Dk. Tamba, Magomeni Mikumi, Dar es Salaam na kumuomba agombee, wakimpa moyo ana sifa na uwezo.
“Walikuwa kama wanane hivi, kati yao watatu walikuwa wazee kabisa, walifika hapa. Wakaomba kumuona Dk Tamba, msaidizi wa Dk Tamba akaenda kumuambia. Dk akawaambia waingie, walipoingia sasa, nasikia yule msaidizi wake wakati anawapelekea kahawa, ndio akasikia hayo mazungumzo,”kilisema chanzo hicho.
BIN ZUBEIRY iliwasiliana na Dk. Tamba juu ya habari hizo na uamuzi wake, lakini akasema ni mapema mno kwa sasa kuzungumzia chochote juu ya hilo, kwa sababu hakuwahi kufikiria suala hilo hata siku moja, hivyo inabidi naye alifanyie kazi kwanza.
“Sheikh haya mambo mazito, wewe umepata habari hizi? Wewe naye hatari sana,” alisema Dk. Tamba na kuanguka kicheko kabla ya kuendelea; “Wamekuja wiki hii kweli, lakini inabidi nipate muda kwanza wa kulitafakari hili jambo na kuwasiliana na wadau wangu kushauriana nao, klabu kubwa ile kaka,”alisema.
Kama kweli Dk Tamba ataamua kugombea Uenyekiti wa Yanga, anaweza akapita kutokana na sifa zake.
Pamoja na kuucheza mpira wa miguu, kuwa na elimu nzuri, pia Dk. Tamba ni mtu anayeheshimika mno na watu mbalimbali nchini, wakiwemo viongozi wakubwa wa serikali, kutokana na shughuli za utabibu.
Ni mwadilifu na muumini safi wa dini ya Kiislamu, ambaye anasali sala tano. Ana hekima, busara na anaijua soka kindakindaki- kwa sababu ni mpenzi haswa wa mchezo huo. Dk Tamba anamiliki timu ya mpira wa miguu ya wanawake ya Mburahati Queens, inayotoa wachezaji wengi timu ya taifa.
Sifa za ziada za Dk Tamba ni mbunifu, kwani pamoja na shughuli zake za tiba za kijadi, ambazo humfanya aende kutoa huduma hadi nje ya nchi, pia ni mfanyabiashara na ni miongoni mwa watu wa awali kabisa nchini kutayarisha filamu ya Kitanzania na kuziingiza sokoni, ambazo zilifanya vizuri mno, kama Nsyuka na Soka la Bongo.

POULSEN AWATEMA NYOTA WAWILI SIMBA SAFARI YA IVORY COAST

Wachezaji wa Taifa Stars wakiingia ndani ya Uwanja wa Ndege wa Mwalimu Julius Nyerere, Dar es Salaam alfajiri ya leo tayari kwa safari ya Ivory Coast.

NYOTA wa klabu ya Simba, beki Said Nassor 'Chollo' na kiungo Haruna Moshi 'Boban' wameondolewa kwenye kikosi cha wachezaji 23 cha timu ya taifa ya soka ya taifa ya Tanzania, Taifa Stars kilichoondoka alfajiri ya leo Dar es Salaam kwa ndege ya Kenya Airways kwenda Abidjan, Ivory Coast kwa ajili ya mechi ya mchujo ya Kombe la Dunia itakayochezwa Juni 2 mwaka huu.
Kocha Kim Poulsen alisema wakati timu hiyo ikiondoka wachezaji hao ni majeruhi ndio maana kawaacha. Wachezaji walioondoka na timu i Nahodha Juma Kaseja, Nahodha msaidizi Aggrey Morris, Mwadini Ally, Deogratius Munishi, Amir Maftah, Erasto Nyoni, Kelvin Yondani, Waziri Salum, Shomari Kapombe, Juma Nyoso, Jonas Mkude, Mwinyi Kazimoto, Salum Abubakar, Shabani Nditi, Edward Christopher, Mrisho Ngasa, Frank Domayo, Mbwana Samata, Ramadhan Singano, Simon Msuva na John Bocco.
Boban na Chollo wanaungana na wachezaji wengine wawili, waliobaki kutokana na kuwa majeruhi, mshambuliaji Thomas Ulimwengu anayecheza timu ya TP Mazembe ya Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo na kiungo wa Yanga, Nurdin Bakari.
Nahodha wa Ivory Coast, Didier Drogba
Viongozi waliofuatana na timu hiyo ni Kocha Mkuu Kim Poulsen, Sylvester Marsh (Kocha Msaidizi), Juma Pondamali (Kocha wa makipa), Leopold Mukebezi (Meneja wa timu), Juma Mwankemwa (Daktari wa timu), Frank Mhonda (Physiotherapist) na Alfred Chimela (Mtunza vifaa).
Msafara huo unaongozwa na Mjumbe wa Kamati ya Utendaji ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) Crescentius Magori wakati naibu kiongozi wa msafara ni Makamu wa Rais wa Chama cha Mpira wa Miguu Zanzibar (ZFA) Haji Ameir Haji.
Timu hiyo inayodhaminiwa na Kilimanjaro Premium Lager iliagwa leo (Mei 30 mwaka huu) na Naibu Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo, Amos Makala ambaye aliwataka wachezaji hao kwenda kuiwakilisha vizuri Tanzania kwenye mechi hiyo.
Hafla hiyo ya kukabidhi Bendera ya Taifa pia ilihudhuriwa na Mwenyekiti wa Baraza la Michezo la Taifa (BMT), Dioniz Malinzi, Rais wa TFF, Leodegar Tenga na Meneja wa bia ya Kilimanjaro, George Kavishe.
Mechi itachezwa kwenye Uwanja wa Felix Houphouet-Boigny jijini Abijan kuanzia saa 11 kamili kwa saa za Ivory Coast.
Kiungo Haruna Boban, enzi zake akicheza Ulaya, Geffle FF ya
Ligi Kuu Sweden, kabla ya kurejea kwenye soka ya madafu
Mwamuzi atakuwa Slim Jedidi wakati mwamuzi msaidizi namba moja ni Bechir Hassani, wote kutoka Tunisia. Mwamuzi msaidizi namba mbili ni Sherif Hassan kutoka Misri. Mwamuzi wa akiba ni Youssef Essrayri pia kutoka Tunisia.
Mtathmini wa waamuzi ni Rachid Medjiba kutoka Algeria wakati Kamishna wa pambano hilo atakuwa Saleh Issa Mahamat kutoka Chad.
Stars itarajea nyumbani Juni 5 mwaka huu saa 1.40 asubuhi na kuingia moja kwa moja kambini kujiandaa kwa mechi dhidi ya Gambia itakayofanyika Juni 10 mwaka huu kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
 

Wednesday, May 30, 2012

PSG YAMTAKA ROONEY KWA BEI AMBAYO HAJAWAHI KUNUNULIWA MCHEZAJI YEYOTE DUNIANI


Rooney

Gossip logo
30 May 2012Last updated at 22:56 GMT

Tetesi za Alhamisi magazeti Ulaya

ROONEY ATAKIWA KWA EURO MILIONI 150 UFARANSA

KLABU ya Paris Saint-Germain ya Ufaransa inajiandaa kufanya kufuru mbaya- kutoa dau la Euro Milioni 150 kwa ajili ya kumnunua mshambuliaji wa Manchester United, Wayne Rooney.
KLABU za Tottenham na Chelsea zinajiandaa kumnunua mshambuliaji wa Newcastle, Demba Ba, ambaye amepewa ruhusa binafsi ya kuhama kwa dau la pauni la Milioni 7.
KLABU ya Chelsea ipo karibuni kumnasa kwa dau la pauni Milioni 40, mshambuliaji wa Porto, Hulk, mwenye umri wa miaka 25, huku mazungumzo yakitarajiwa kuendelea baadaye wiki hii.
KLABUA za Manchester United, Chelsea na Arsenal zinamfuatilia kinda wa umri wa miaka 22 wa Ukraine, kiungo wa Dnipro, Yevhen Konoplyanka.
Rafael Van der Vaart
Rafael van der Vaart.
MSHAMBULIAJI wa Tottenham, Rafael van der Vaart anatazamiwa kuondoka White Hart Lane baada ya Schalke kuonyesha nia ya kumchukua Mholanzi huyo kwa dau la pauni Milioni 10.
KLABU za Tottenham na Newcastle zimeingia kwenye mbio za kuwania saini ya kiungo wa Manchester City, Adam Johnson.
WAPINZANI wa Kaskazini kwa London, Arsenal na Tottenham zina mpango wa kumsajili kiungo wa Sochaux, Marvin Martin baada ya mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 24 kusema anataka kuondoka Ufaransa.
KLABU ya Arsenal inataka kumpa ofa Salomon Kalou kubaki katika Ligi Kuu ya England, baada ya kutemwa na klabu yake ya sasa, Chelsea, huku kukiwa kuna habari anataka kwenda Schalke.
KLABU ya Newcastle imeripotiwa kutenga dau la kati ya pauni 500,000 na Milioni 1 kumnasa kinda wa Coventry, Gael Bigirimana, mwenye umri wa miaka 18.
KOCHA wa Sunderland, Martin O'Neill yuko tayari kumnasa Msenegali wa Wigan, kiungo nyota Mohamed Diame, mwenye umri wa miaka 24.

ATEMWA KIKOSI CHA EURO KWA KUSHINDWA WIMBO WA TAIFA

KOCHA Mserbia, Sinisa Mihajlovic amemtema Adem Ljajic baada ya mshambuliaji huyo kushindwa kuimba wimbo wa taifa kabla ya mechi waliyofungwa 2-0 na Hispania Jumamosi.
 

KAMBI TIMU YA TAIFA ZANZIBAR MATATIZO MATUPU HADI MISOSI MIGOGORO


Wachezaji mazoeini jioni ya leo, Uwanja wa Amaan jioni ya jana
KAMBI ya timu ya taifa ya Zanzibar, inayojiandaa na michuano ya Kombe la dunia kwa nchi zisizo wanachama wa FIFA (Shirikisho la Soka la Kimataifa), inakabiliwa na hali ngumu mno na zaidi inaendelea kwa sababu ya uzalendo wa wachezaji pekee.
BIN ZUBEIRY jana imetembelea kambi hiyo visiwani hapa na kufanya mahojiano na Kocha Mkuu, Ahmad Morocco, ambaye amesema kama si uzalendo wa wachezaji, basi safari ya Uzbekistan kwenye mashindano hayo yanayoanza Juni 4, mwaka huu ingekufa.
Morocco amesema vijana wapo kambini Bwawani Hotel, lakini hata chakula ni cha matatizo. “Hawapati chakula cha kutosha, yaani wanapewa chakula kwa kiwango ambacho wamepanga wenye hoteli, si lishe ya kula mchezaji, lakini tutafanyeje na hiyo ndio hali halisi,”amesema Morocco.

CHANZO CHA MATATIZO:
Nikiwa kwenye mazungumzo na kocha Morocco
Morocco anasema kwamba chanzo cha matatizo ni timu kutokuwa na mdhamini wala wafadhili na anasikitika japo Zanzibar kuna wafanyabiashara wakubwa na maarufu, lakini wote wamekaa kimya kipindi hiki na hawajitokezi kusaidia timu.
“Wao wanasubiri matokeo mabaya waje kulaumu tu, lakini katika hali kama hii, ukifanya vizuri basi unastahili sifa sana, mimi nakuambia hata dawa tu hapa ni tatizo, timu haina dawa wala nini,”amesema.
Morocco anasikitika kwamba hata wachezaji wa timu hiyo wapo kambini kwa zaidi ya siku 10, lakini hawapati posho na anaamini Chama cha Soka Zanzibar (ZFA) hakina uwezo kwa sababu hakina wafadhili zaidi ya kutegemea serikali.
“ZFA wanasema wamekwishapeleka bajeti yao Wizarani, lakini ajabu hadi sasa wanasema hawajajibiwa chochote, na hali inazidi kuwa mbaya kambini, maana yake wachezaji wanatumia chao cha mfukoni hadi wanaishiwa, sasa hata familia zao watazisaidiaje,”amesema.

SMZ IMEISUSA TIMU?
Selembe kushoto na Gulam kulia wakijiandaa kuingia mazoezini
Lakini katika hali ya kustaajabisha zaidi, wachezaji wa timu hiyo wanastaajbu Serikali ya Mapinduzi Zanzibar imekaa kimya kabisa na wala haijaonyesha dalili za kusaidia timu. “Sisi tunashangaa, kwa sababu matatizo yetu yanajulikana, lakini serikali imekaa kimya, yaani kila siku mazoezini ni kama unavyotuona, sisi na makocha wetu tu na daktari wetu. Hatumuoni hata kiongozi wa ZFA wala serikali, ila sisi tutakwenda kupigana na tutaleta Kikombe hapa wao washerehekee,”alisema Nadir Haroub ‘Cannavaro’, beki wa timu hiyo.

PAMOJA NA YOTE, VIJANA UZALENDO MBELE:
Abdi Kassim kushoto na Abdulhalim Humud kulia wakipasha
Pamoja na matatizo yote, kocha Morocco amesema wachezaji wana morali kutokana na hali yao ya uzalendo. “Wachezaji wako vizuri na wanaendelea vizuri na wako tayari kwa mashindano. Wameonyesha uzalendo wa hali ya juu kwa kweli.
Morocco amesema timu itaondoka Juni 2, kupitia Dar es Salaam tayari kwa mchezo wa kwanza dhidi ya Tehran na anasema kwa ujumla wamepania kurejea na Kombe hilo. “Sisi kwa pamoja, azma yetu ni kurejea na Kombe, ili tuwadhihirishie wananchi wa Zanzibar uzalendo wetu,”amesema.

SABRI, FAROUK WATEMWA SAFARINI, CANNAVARO CHUPUCHUPU
Cannavaro na mkewa wakiwa jukwaani wanaangalia mazoezi
Katika kikosi cha wachezaji 18 wanaoondoka na timu, wachezaji wawili tegemeo, kipa namba moja Farouk Ramadhan Mzee na kiungo Sabri Ramadhan ‘China’ wametemwa kutokana na kuchelewa kuwasilisha pasipoti zao kwa ajili ya kuombewa viza.
Bado kikosini watakuwepo wachezaji wengine hodari tu wakiongozwa na nyota wa Azam FC, viungo Abdi Kassim ‘Babbi’, Abdulhalim Humud ‘Gaucho’, Suleiman Kassim ‘Selembe’, beki wa Yanga, Cannavaro, ambaye naye chupuchupu akose safari kutokana na majeruhi na mshambuliaji wa Canal Suez ya Misri, Ally Badru.
Cannavaro ameshindwa kufanya mazoezi leo kutokana na kufanyiwa upasuaji mdogo wa jipu kwenye goti, lakini daktari wa timu amethibitisha anaendelea vizuri na kesho ataaanza tena mazoezi.
Katika kikosi hicho atakosekana pia beki Aggrey Morris Ambroce, ambaye yuko kwenye kikosi cha timu ya taifa ya Tanzania, Taifa Stars kinachokwenda kucheza na Ivory Coast mwishoni mwa wiki, kikiondoka alfajiri ya kesho Dar es Salaam.
Morocco amesema pengo la Morris limezibwa vema na beki Salum Tall anayecheza soka ya kulipwa Oman, ambaye alicheza soka nzuri mno katika mechi ya kujipima nguvu na Malawi jana iliyoisha kwa sare ya 1-1. Malawi pia ilicheza na Taifa Stars Jumamosi wakatoka 0-0.
 

STARS YAONDOKA ALFAJIRI KUWAFUATA AKINA DROGBA, YAYA TOURE


Mbwana Samatta katikati akimtoka Juma Nyosso mazoezini wiki iliyopita

KIKOSI cha wachezaji 23 na viongozi tisa kinatarajia kuondoka kesho (Mei 31 mwaka huu) saa 11.10 alfajiri kwa ndege ya Kenya Airways kwenda Abidjan, Ivory Coast kwa ajili ya mechi ya mchujo ya Kombe la Dunia itakayochezwa Juni 2 mwaka huu.
Wachezaji wanaoondoka ni nahodha Juma Kaseja, nahodha msaidizi Aggrey Morris, Mwadini Ally, Deogratius Munishi, Nassor Masoud Cholo, Amir Maftah, Erasto Nyoni, Kelvin Yondani, Waziri Salum, Shomari Kapombe na Juma Nyoso.
Wengine ni Jonas Mkude, Mwinyi Kazimoto, Salum Abubakar, Shabani Nditi, Edward Christopher, Mrisho Ngasa, Frank Domayo, Mbwana Samata, Ramadhan Singano, Simon Msuva, Haruna Moshi na John Bocco.
Wachezaji waliobaki kutokana na kuwa majeruhi ni mshambuliaji Thomas Ulimwengu anayecheza timu ya TP Mazembe ya Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo na kiungo wa Yanga, Nurdin Bakari.
Nahodha wa Ivory Coast, Didier Drogba
Viongozi wanaofuatana na timu hiyo ni Kocha Mkuu Kim Poulsen, Sylvester Marsh (Kocha Msaidizi), Juma Pondamali (Kocha wa makipa), Leopold Mukebezi (Meneja wa timu), Juma Mwankemwa (Daktari wa timu), Frank Mhonda (Physiotherapist) na Alfred Chimela (Mtunza vifaa).
Msafara huo unaongozwa na Mjumbe wa Kamati ya Utendaji ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) Crescentius Magori wakati naibu kiongozi wa msafara ni Makamu wa Rais wa Chama cha Mpira wa Miguu Zanzibar (ZFA) Haji Ameir Haji.
Timu hiyo inayodhaminiwa na Kilimanjaro Premium Lager imeagwa leo (Mei 30 mwaka huu) na Naibu Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo, Amos Makala ambaye aliwataka wachezaji hao kwenda kuiwakilisha vizuri Tanzania kwenye mechi hiyo.
Hafla hiyo ya kukabidhi Bendera ya Taifa pia ilihudhuriwa na Mwenyekiti wa Baraza la Michezo la Taifa (BMT), Dioniz Malinzi, Rais wa TFF, Leodegar Tenga na Meneja wa bia ya Kilimanjaro, George Kavishe.
Mechi itachezwa kwenye Uwanja wa Felix Houphouet-Boigny jijini Abijan kuanzia saa 11 kamili kwa saa za Ivory Coast.
Mwamuzi atakuwa Slim Jedidi wakati mwamuzi msaidizi namba moja ni Bechir Hassani, wote kutoka Tunisia. Mwamuzi msaidizi namba mbili ni Sherif Hassan kutoka Misri. Mwamuzi wa akiba ni Youssef Essrayri pia kutoka Tunisia.
Mtathmini wa waamuzi ni Rachid Medjiba kutoka Algeria wakati Kamishna wa pambano hilo atakuwa Saleh Issa Mahamat kutoka Chad.
Stars itarajea nyumbani Juni 5 mwaka huu saa 1.40 asubuhi na kuingia moja kwa moja kambini kujiandaa kwa mechi dhidi ya Gambia itakayofanyika Juni 10 mwaka huu kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam

No comments: