AZAM FC WAJA NA UZI UPYA MKALI WA 2012/2013
Jezi za msimu ujao za Azam, ya kwanza kushoto itatumika ugenini, ya pili yake nyumbani Chamazi |
KLABU ya Azam FC ipo kwenye
mchakato wa kutoa jezi mpya za msimu ujao- ambazo watatumia katika Ligi Kuu ya
Bara na michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika.
Washindi hao wa Medali ya
Fedha Ligi Kuu Bara, kwa msimu wa tatu mfululizo wameweza kuendana na mfumo wa
kisasa wa utumiaji wa vifaa vya michezo, yaani kila baada ya msimu wanaibua
mzigo mpya- zoezi ambalo bado linavishinda vigogo wa soka nchini, Simba na Yanga
japo wanadhaminiwa na kampuni kubwa, TBL.
Azam FC, kama ilivyokuwa kwa
Mtibwa Sugar, nayo ilianzishwa na kikundi cha wafanyakazi wa kampuni ya Mzizima
Flour Mill, kampuni tanzu ya Bakhresa, makao yake makuu yakiwa Barabara ya
Nyerere, Dar es Salaam.
Lengo la wafanyakazi hao wa
kampuni inayomilikiwa na Said Salim Bakhresa, awali ilikuwa ni kucheza kwa ajili
ya kujiburudisha, baada ya kazi.
Lakini baada ya kuona wana
timu nzuri, Oktoba 16, mwaka 2004, waliisajili rasmi kwa ajili ya kushiriki Ligi
Daraja la Nne, wakitumia jina la Mzizima FC.
Baadaye Mkurugenzi Mkuu wa
makampuni ya Bakhresa, Abubakar Bakhresa, aliona ni vyema timu hiyo ihusishe
wafanyakazi wa kampuni zote za Bakhresa, na kutumia jina la moja ya bidhaa zao
kubwa, Azam.
Kampuni nyingine za Bakhresa
ni Food Products Ltd, Azam Bakeries Ltd, Omar Packaging Industries Ltd na
kadhalika.
John Bocco na jezi ya Azam msimu wa 2010/2011 |
Wazo lake lilikubaliwa na
wafanyakazi wa kampuni hiyo, ndipo timu hiyo ikaanza kuitwa Azam SC, badala ya
Mzizima. Lakini baadaye Juni 11, mwaka 2007, ilibadilishwa jina tena na kuwa
Azam FC.
Azam ilikwenda kwa kasi nzuri
kuanzia Daraja la Nne na hadi mwaka 2008, ilifanikiwa kucheza Ligi Kuu,
ikipandishwa na makocha King, aliyekuwa akisaidiwa na Habib Kondo. Baada ya
kupanda, Azam ilimuajiri kocha wa zamani wa Simba SC, Mbrazil Neider dos Santos,
aliyekuwa akisaidiwa na Sylvester Marsh na Juma Pondamali upande wa kuwanoa
makipa.
Baadaye ilimuongeza kocha wa
viungo, Itamar Amorin kutoka Brazil pia, ambaye awali ya hapo alikuwa msaidizi
wa Marcio Maximo katika timu ya taifa ya Tanzania, Taifa
Stars.
Ilisajili pia wachezaji nyota,
wazoefu, wakiwamo kutoka nje ya Tanzania, ambao walichanganywa na chipukizi
wachache walioipandisha timu hiyo, kama John Bocco
‘Adebayor’.
Wakati Azam inapigana kwenye
Ligi Daraja la kwanza ili kupanda Ligi Kuu, kikosini ilikuwa ina wakongwe kama
Shekhan Rashid na Suleiman Matola, viungo wa zamani wa klabu ya
Simba.
Malengo makuu ya Azam ni
kuifanya timu iwe ya kulipwa, wachezaji wakihudumiwa vizuri, chini ya makocha
bora, nao waweze kufanya vizuri na kuitangaza kimataifa timu hiyo na soka ya
Tanzania kwa ujumla.
Aidha, kwa kuwa inataka
kutambulika kimataifa, ina kitengo maalumu cha soka ya vijana, kilicholenga
kuibua vipaji vya chipukizi wa soka na kuwakuza katika misingi na maadili ya
mchezo wenyewe, ili baadaye wauzwe Ulaya.
Mmoja kati ya mabosi wa Azam,
Yussuf Bakhresa, ni wakala wa wachezaji anayetambuliwa na Shirikisho la Soka la
Kimataifa (FIFA), ambaye anaweza kuwafanya yosso wa klabu hiyo waende Ulaya moja
kwa moja.
John Bocco na jezi ya msimu
uliopita ya Azam, iliyowapa nafasi ya pili Ligi Kuu, wakiipikua Yanga |
Kikosi cha kwanza cha Azam
Ligi Kuu kilikuwa kinaundwa na wafuatao; Kassim Kilungo, Said Bakar Nachikongo,
Abdul Azizi Hamza, Shaaban Abdallah Kisiga ‘Malone’, Ally Suleiman Alawy, John
Raphael Bocco ‘Adebayor’, Salum Machaku, Shekan Rashid Abdallah, Jamal Simba
Mnyate, Yussuf Juma Gogo, Zuberi Ubwa, Yahaya Said Tumbo, Said Khamis Sued,
Salum Abubakar Salum, Luckson Jonathan Kakolaki, Adam Shomari Ngido, Abdulhalim
Chilumbe, Ngoy-Pichou Botwetwe, Mussa Khalid Kipao, Iddi Abubakar Mwinchumu,
John Faustin Mabula, James Adriano Kilongola, Malika Philipo Ndeule, Paulo John
Nyangwe, Abubakar Pawasa na Vladimir Niyonkuru.
Azam pamoja na kumilikiwa na
kampuni ya bilionea, zaidi ya basi lake ‘kali’, haina uwanja wake, Azam Complex,
uliopo Chamazi, Mbagala, Dar es Salaam, ambao kwa msimu huu imeshuhudiwa hadi
vigogo, Simba na Yanga wakiutumia kwa mechi zao za Ligi Kuu.
Kwa
sasa Kocha Mkuu wa Azam, Muingereza Stewart Hal. Naam, hao ndiyo Azam FC, wana
Lamba Lamba.
Hivi karibuni, Azam watafanya
ziara ya kujiandaa na msimu mpya Falme za Kiarabu na inawezekana wakaondoka
baada tu ya michuano ya Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati, Kombe la Kagame
itakayofanyika Julai mjini Dar es Salaam.
Malengo ya Azam ni kutwaa
Kombe la Kagame na kuhakikisha mwakani wanacheza hatua ya makundi ya Kombe la
Shirikisho- pamoja na kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu ya Bara. Hao ndio Azam
No comments:
Post a Comment