Monday, October 24, 2016

Bei ya Korosho kuchangia ongezeko la Ndoa holela Nanyamba Mtwara.


Baadhi wa wakulima wa korosho wa halmashauri ya mji wa Nanyamba, Mtwara wakifuatilia mnada wa ununuzi wa zao hilo.




Meneja mkuu wa chama kikuu cha ushirika cha Mtwara, Masasi Co operative Union-MAMCU, Kelvin Rajabu akitoa maelekezo kwa  wakulima wa korosho wakati wa mnada wa ununuzi wa zao hilo, katika ghala la Dinyecha, Nanyamba.


Juma Mohamed, Mtwara

Baadhi ya wakulima wa zao la korosho katika halmashauri ya mji wa Nanyamba mkoani Mtwara, wameahidi kuongeza kasi ya kufunga ndoa ikiwa ni sehemu ya matumizi ya pesa wanazozipata kupitia mauzo ya zao hilo
Wakizungumza na Juma News nje ya ghala la chama cha msingi cha Dinyecha baada ya kufanyika kwa mnada wa ununuzi wa korosho, wamesema kupanda kwa bei ya zao hilo kutachangia ongezeko la ndoa holela maarufu kama Ndoa za Msimu.
“Mimi nasema nashukuru kwa bei ya korosho…hii bei ya korosho itatufanya sisi wakulima wadogowadogo sisi kwanza tuwe na fursa ya kupata hela nyingi na kutusaidia mambo ya Ndoa, tutaoa wanawake tutafanya shughuli zile za kilimo..kwahiyo na ndoa zenyewe kama zilikua kwa mwaka zinakua 10 au 20 na zaidi na mpaka hata 50..tunamuomba tu rahisi ili aliweke kipaumbele..” alisema Said Ngalile mkazi wa Nanyamba.

Baadhi wa wakulima wa korosho wa halmashauri ya mji wa Nanyamba, Mtwara wakifuatilia mnada wa ununuzi wa zao hilo.



Said Selemani anasema ndoa hizo hupatikana zaidi msimu wa mauzo ya korosho kutokana na wakulima wengi kupata pesa na kwamba katika msimu huu ambao korosho inaonekana kuwa na bei nzuri ndoa hizo zitakuwa kwa wingi zaidi.
Asha Salum, anaeleza namna ndoa hizo zilivyokithiri katika halmashari hiyo pamoja na kueleza athari ambazo wanawake wanazipata baada ya kuachika kutoka kwa waume zao.
“Tunatelekezwa sana sisi akina mama katika ndoa hizo, kwasababu anakuachia familia unahangaika sana na inakuwa hata watoto hawajali..msimu huu korosho ziko juu sana kwahiyo nategemea hizi ndoa zitakuwa nyingi sana kwasababu pesa zitakuwepo.” Alisema Asha Salum

Meneja mkuu wa chama kikuu cha ushirika cha Mtwara, Masasi Co operative Union-MAMCU, Kelvin Rajabu akitoa maelekezo kwa  wakulima wa korosho wakati wa mnada wa ununuzi wa zao hilo, katika ghala la Dinyecha, Nanyamba.



Meneja mkuu wa chama kikuu cha ushirika cha Mtwara, Masasi Co operative Union MAMCU Kelvin Rajabu, anaeleza namna minada ilivyofanyika na kampuni zilizoshinda ununuzi.
“Wakulima wa Masasi wameuza korosho zao kwa bei ya chini ya shilingi 3,760 na bei ya juu ni 3,805 lakini kwa upande wa wakulima wa Mtwara kwa upande wa ghala la Olam kampuni ya B Southern Trading imeweza kuchukua korosho kwa bei ya 3, 805 japokua ni tani chache tani 230..” alisema
Naye mkuu wa mkoa wa Mtwara Halima Dendego anawakumbusha wakulima matumizi bora ya fedha wanazozipata baada ya mauzo, huku akisisitiza wajiwekee akiba kwa ajili ya ununuzi wa pembejeo mara baada ya msimu kumalizika.
Ndoa za msimu zimeshamiri zaidi katika maeneo yanayolimwa korosho kwa wingi mikoa ya Lindi na Mtwara na hufungwa zaidi wakati huu wa mauzo ya zao hilo na kuachana mara baada ya wakulima kuishiwa pesa.

No comments: