Tuesday, June 14, 2016

Tandahimba wakamilisha madawati shule za msingi kwa asilimia 100


Mkuu wa wilaya ya Tandahimba, Emmanuel Luhahula.





Fundi akiendelea na ujenzi wa jengo la maabara, sekondari ya Tandahimba



Juma Mohamed, Mtwara.

Ikiwa zimebaki wiki mbili kabla ya kufikia mwisho wa muda uliotelewa na serikali kwa halmashauri zote nchini juu ya utatuzi wa uhaba wa madawati kwa shule za msingi na sekondari, halmashauri ya wilaya ya Tandahimba mkoani Mtwara imekamilisha agizo hilo kwa asilimia 100 kwa shule za msingi.
Mkuu wa wilaya hiyo, Emmanuel Luhahula alisema awali halmashauri hiyo ilikuwa ikikabiliwa na uhaba wa madawati 7,453 kwa shule zote za msingi na sekondari ambapo tayari ya shule za msingi yamekamilika huku wakibawa na zoezi la kukamilisha madawati zaidi ya 500 kwa shule za sekondari.
“Mpaka hapa sasa hivi tunapoongea madawati kwa shule za msingi tulishakamilisha yote, hakuna dawati hata moja ambalo tunadaiwa kilichobaki ni kuanza kuyasambaza kwa shule husika..kwa sekondari bado madawati sina takwimu sahihi hapa lakini ni kama Miatano na kitu au miasaba hivi..” alisema.
Alisema, madawati yaliyobaki kwa sekondari yapo katika hatua za mwsho ili yakamilike ambapo licha kukabiliwa na uhaba wa mbao lakini aliahidi kukamilisha kabla ya June 30 mwaka huu.
Sambamba na utatuzi wa changamoto ya madawati, halmashauri hiyo inaendelea na utekelezaji wa agizo la Rais wa awamu ya Nne Dkt. Jakaya Kikwete, la ujenzi wa Maabara ya Sayansi kwa shule za sekondari ambapo wanafunzi walielezea adha wanayoipata kwa kukosa Maabara.
“Masomo yapo matatu, na yote yanahitaji ‘practical’ (Mafunzo kwa vitendo) kwahiyo wanafunzi wanapoingia Maabara kufanya ‘practical’ vipindi vinagongana kwahiyo inawapa tabu sana walimu kwasababu mwalimu wa Physics anataka kufanya ‘prctical’ katika ‘laboratory’ hiyohiyo na mwalimu wa Kemia anataka afanye hivyo hivyo kwahiyo inatupa changamoto sana wanafunzi pale tunaposoma..” alisema Mwanahawa Hussein, mwanafunzi wa Sekondari ya Tandahimba.

Mwanafunzi wa shule ya sekondari ya Tandahimba, Mwanahawa Hussein.



Kwa upande wake, mkurugenzi wa halmashauri hiyo, Mzega Twalib, alisema ujenzi wa Maabara unaendelea katika halmashauri yake ikiwa ni utekelezaji wa agizo la serikali ya awamu ya Nne huku akiahidi kukamilisha ifikapo mwezi Septemba mwaka huu.
“Vikao vya halmashauri vilitenga fedha sh. Milioni 300 kwa ajili ya kupeleka kwenye Maabara kwahiyo tulipeleka kwenye shule zote 28 ili kufanya ‘finishing’ ya angalau chumba kimoja ili viweze kutumika kwahiyo ndio ujenzi ambao unaendelea..lakini pia halmashauri inampango wa kupeleka fedha nyingine takribani sh. Milioni 600 katika mwaka huu wa fedha unaoanzia Julai ili kwa vyovyote itakavyokuwa ifikapo mwezi Septemba tuwe tumekamilisha zoezi la ukamilishaji wa ujenzi wa Maabara..” alisema.
Halmashauri hiyo inatarajia kutumia kiasi cha sh. Bilioni 2.1 ili kukamilisha ujenzi huo kwa maabara zote katika shule zote 28 za sekondari.

Mkurugenzi wa halmashauri ya wilaya ya Tandahimba, Mzega Twalib






No comments: