Sunday, January 10, 2016

Wananchi Mtwara wachangamkia fursa ya kujiendeleza kielimu.

Mbunge wa Mtwara mjini (CUF) Maftaha Nachuma, akiwa darasani kuwafundisha baadhi ya wananchi wa jimbo hilo waliojiandikisha katika programu yake ya Maftaha English Leaning yenye lengo la kuwaendeleza wananchi hao kielimu na kuwawezesha kujua lugha ya kiingereza ili waweze kunufaka kwa kupata ajira katika kampuni mbalimbali za uwekezaji mkoani Mtwara.


Baadhi ya wananchi wa manispaa ya Mtwara wakiwa katika foleni ya kusubiri kujiandikisha katika programu ya kujiendeleza kielimu ya Maftaha English Leaning iliyoandaliwa na mbunge wa jimbo la Mtwara mjini (CUF), Maftaha Nachuma



Baadhi ya wananchi wa manispaa ya Mtwara mikindani wakiwa darasani kuhudhuria masomo kupitia programu ya kuwaendeleza kielimu ya Maftaha English Leaning inayotekelezwa na mbunge wa Mtwara mjini (CUF), Maftaha Nachuma, inayofanyika katika shule ya msingi Lilungu. 

Na Juma Mohamed, Mtwara.

WANANCHI wa manispaa ya Mtwara Mikindani wamehamasika kwa kiasi kikubwa na kujitokeza katika program maalumu ya kuwaendeleza kielimu iliyoanzishwa na mbunge wa jimbo la Mtwara mjini (CUF) Maftaha Nachuma, kwa lengo la kuinua kiwango cha elimu kwa wananchi hao ambao wanalalamikia ukosefu wa ajira.
 Wakizungumza wakati wa kujiandikisha kwa ajili ya kuanza masomo programu hiyo inayofahamika kama Maftaha English Leaning Program, baadhi yao walisema wameshawishika kujiunga kwasababu wanaamini ukosefu wa ajira wanaokabiliana nao kwa sasa ni kutokana na kutokuwa na elimu ya kutosha ikiwa ni pamoja na kutojua lugha ya kiingereza.
Walisema, miongoni mwa changamoto wanazokabiliana nazo kutokana na kukosa elimu ni kuaibika wanapotembea katika sehemu mbalimbali hapa nchini kwa kuambiwa wakazi wa Mtwara hawana elimu, huku wengine wakidai kuwa hali hiyo inachangia umasikini kwa baadhi yao.
“Kwakweli hamasa ambayo imenifanya mimi kuja mahali hapa kwanza nikiangalia sikuizi ni tofauti na zamani, sasahivi utandawazi ni mwingi, yani nikiangalia huu ni mwaka 2016 sasa mpaka kufikia 2020 kwa sisi ambao hatujui hii lugha ya kiingereza yani tutakuwa tupo chini na ukiangalia huu mkoa wetu sasahivi ajira zipo nyingi, tukishazembea kusoma itaonekana hata wabaki kutoka huko nchi za nje watakuja kupata ajira..” alisema Zuhura Abeid.
Naye, Ahmadani Nahembe, ambaye anashughulika na sanaa za maigizo, alisema suala la kutojua lugha ya kiingereza limekuwa ni changamoto kubwa kwake kutokana na kukosa kazi anapotakiwa kufanyiwa usaili kwa lugha hiyo ambayo ndio itakayoanza kufundishwa katika program hiyo kwa muda wa miezi sita kabla ya kuanza masomo ya elimu ya sekondari.
Kwa upande wake, mbunge huyo alisema alibaini kuwepo kwa changamoto hiyo kutokana na kuzunguka katika ofisi na kampuni mbalimbali za serikali na watu binafsi ambapo aligundua kuwa kuna uhaba wa wananchi wa Kusini walioajiriwa katika ofisi hizo huku alipouliza sababu za uhaba wao alijibiwa kuwa wananchi wengi hawana elimu.
“Kwahiyi nikaona kwamba kuna haja ya kuwatangazia Wanamtwara, niazishe hii program maalumu, kwanza waweze kujua kiingereza na ndio maana tumesema wasome kwa miezi mitatu kwanza ‘then’ wafanye mtihani wasome tena miezi mitatu mingine wafanye mtihani kwa maana kwamba ni miezi sita, ‘then’ tuaanze masomo ya sekondari kwasababu masomo ya sekondari yanafundishwa kwa lugha ya kiingereza kwahiyo tukaona ni vema wanafunzi wakajua kiingereza kwanza ili watakapojisomea vitabu vya kiingereza waweze kufahamu kile kilichoandikwa..” alisema Maftaha.
Alisema, amefurahishwa na muitikio wa watu ambao ni zaidi ya 500 walijitokeza kujiandikisha huku akiwataka wananchi hao wazidi kujituma ili waweze kufikia malengo kwasababu kusoma hakuna umri, ambapo alisema mpango huo anaugharamia mwenyewe kupitia mshahara wake na tayari walimu wameshapatikana kwa ajili ya kuanza kufundisha.

No comments: