Tuesday, December 22, 2015

Serikali Mtwara kuwachukulia hatua watakaoshindwa kuwapeleka watoto wao Kidato cha kwanza.


Katibu Tawala wa Mkoa wa Mtwara, Alfred Luanda, akifungua Kikao cha Uchaguzi wa wanafunzi watakaojiunga na kidato cha kwanza kwa mwaka 2016, katika ukumbi wa Montesori-Mtwara





Wajumbe wa kikao cha uchaguzi wa wanafunzi watakaojiunga na kidato cha kwanza mwaka 2016, ambao ni maafisa elimu wa halmashauri zote za mkoa wa Mtwara, baadhi ya wakuu wa shule, wakurugenzi wa halmashauri na wadau wengine, katika ukumbi wa Montesori-Mtwara


 Na Juma Mohamed

SERIKALI mkoani hapa imesema itawakamata na kuwafikisha kwenye vyombo vya sheria wazazi na walezi watakaobainika kutowaandikisha watoto wao kujiunga na elimu ya sekondari, kwani hawana kisingizio kutokana na elimu kutolewa bure kwanzia darasa la kwanza hadi kidato cha nne.
Akizungumza katika kikao cha uchaguzi wa wanafunzi watakaojiunga na kidato cha kwanza mwaka 2016, katibu tawala wa mkoa wa Mtwara, Alfred Luanda, aliwaagiza viongozi wa idara mbalimbali za elimu katika halmashauri ikiwa ni pamoja na maafisa elimu na wakurugenzi, kuhakikisha kila mototo aliyechaguliwa kujiunga na kidato cha kwanza naripoti shuleni katika tarehe husika.

Katibu Tawala wa Mkoa wa Mtwara, Alfred Luanda, akifungua Kikao cha Uchaguzi wa wanafunzi watakaojiunga na kidato cha kwanza kwa mwaka 2016, mbele ya wajumbe ambao ni maafisa elimu wa halmashauri zote za mkoa wa Mtwara, baadhi ya wakuu wa shule, wakurugenzi wa halmashauri na wadau wengine, katika ukumbi wa Montesori-Mtwara

Alisema, viongozi hao watakua na hoja za kujibu iwapo kutatokea baadhi ya watoto kati ya 15,670 ambao wanatarajiwa kujiunga na kidato cha kwanza mwakani, watashindwa kuandikishwa kwasababu wazazi na walezi hawana sababu za kutowaandikisha.
Pia alionya baadhi ya wazazi kuwaachisha masomo watoto wao hasa wakike kwa ajili ya kuwapeleka Jando na Unyago kisha kuwaozesha, ambapo amewataka viongozi wa ngazi husika kulidhibiti suala hilo na kuwachukulia hatua watakaobainika.
“Lakini kuna tabia ya watu kuwachukua watoto wao kwa ajili ya kuwacheza ngoma na kuwaoza wakiwa bado wadogo hasa watoto wakike, kuwaachisha shule mapema, tunaomba tutoe onyo kama serikali, hiyo tabia kwakweli haikubaliki..tunaomba viongozi mkienda mkafuatilie, mototo amechaguliwa kidato cha kwanza na hajaripoti hatua zichukuliwe, mzazi achukuliwe hatua aseme Yule mototo amempeleka wapi..” alisema.
Alisema, wapo baadhi ya wazazi ambao wanakatisha masomo kwa watoto wao kwa makusudi kwa lengo la kutaka wawasaidie katika shughuli zao za kilimo na wengine kuwashinikiza waingie katika shughuli za ujaasiliamali, jambo ambalo ameliita ni hujuma kwa watoto hao na ni vitendo ambavyo havikubaliki.

Awali akiwasilisha taarifa ya uchaguzi wa wanafunzi watakaojiunga na kidato cha kwanza mwaka 2016, afisa elimu wa mkoa, Fatuma Kilimia, alisema katika mwaka 2015 jumla ya wanafunzi 22,902 wakiwemo wavula 10,304 na wasichana 12,598 walifanya mtihani wa kumaliza elimu ya msingi, ambapo kati yao waliofaulu ni 15,670 wakiwemo wavulana 7,215 na wasichana 8,455.
“Ufaulu huo ni sawa na asilimia 68.42, ufaulu wa mwaka huu ukilinganisha na ule wa mwaka 2014 umepanda, kwani mwaka 2014 ufaulu ulikua sawa na asilimia 62.0, hivyo mkoa umepanda kwa asilimia 6.42..” alisema.
Licha ya ufaulu kimkoa kuonekana kupanda kwa asilimia 6.42, mkoa wa Mtwara Kitaifa umekuwa katika nafasi ya 12 na kuonekana kurudi nyuma kwa nafasi mbili kutoka katika nafasi ya 10 mwaka 2014, huku halmashauri ya Mtwara vijijini ikifanya vizuri na kuwa yakwanza kimkoa kwa kufaulisha kwa asilimia 86.84 na Kitaifa kushika nafasi ya 16.
Kutokana na takwimu hizo, halmasahuri hiyo imepanda ukilinganisha na takwimu za matokeo ya mwaka 2014 ambapo ilifaulisha kwa asilimia 71 na kuwa yapili kimkoa na kitaifa kuwa katika nafasi ya 31.

Wajumbe wa kikao cha uchaguzi wa wanafunzi watakaojiunga na kidato cha kwanza mwaka 2016, ambao ni maafisa elimu wa halmashauri zote za mkoa wa Mtwara, baadhi ya wakuu wa shule, wakurugenzi wa halmashauri na wadau wengine, katika ukumbi wa Montesori-Mtwara

Halmashauri ambazo zimeonekana kufanya vibaya katika mtihani huo ni za Masasi na Nanyumbu, ambapo Masasi vijijini imefaulisha kwa asilimia 53.2 nakuwa katika nafasi ya sita kimkoa na kitaifa kuwa nafasi ya 141, na kwamba ukilinganisha na ufaulu wa mwaka 2014, imepanda kwa asilimia 0.2 kwasababu mwaka 2014 ilifaulisha kwa asilimia 53.
Masasi miji yenyewe imekuwa katika nafasi ya saba kimkoa na nafasi ya 142 kitaifa kutokana na kufaulisha kwa asilimia 53.09, hivyo kurudi nyuma kwa nafasi mbili kutokana na kuwa katika nafasi ya tano mwaka 2014.
Nanyumbu ambayo imeshika nafasi ya tano kimkoa na nafasi ya 132 kwa kufaulisha kwa asilimia 55.07, yenyewe imeshuka ukilinganisha na ufaulu wa mwaka 2014 ambapo kimkoa ilikuwa nafasi ya 4 huku kitaifa ikiwa nafasi ya 77.
”Ufaulu katika halmashauri zote umepanda, tatizo bado lipo Masasi (V) ambayo imebaki palepale, Nanyumbu imerudi nyuma hatua 2.5 na Masasi mji imerudi hatua 2.9. Tunazipongeza halmashauri zote kwa juhudi walizoziweka hadi kufanikiwa kuinua taaluma..pongezi kubwa ni kwa halmashauri ya Mtwara kwa kuchukua nafasi ya 16 kitaifa na Mtwara Manispaa kwa kupanda kwa hatua 22.8 ikilinganishwa na mwaka 2014.” Aliongeza Kilimia.
Kufuatia kufanya vibaya kwa halmasahuri hizo, katibu tawala alitoa onyo kwa maafisa elimu na kuwataka kuhakikisha wanainua hali ya ufaulu katika mitihani ijayo, na kama hali itaendelea kuwa hifyo hatua kali zitachukiliwa dhidi yao.
Aidha, akitolea maelezo sababu za kufanya vibaya katika halmashauri yake, mkurugenzi mtendaji wa halmashauri ya Nanyumbu, Idris Mtande, alisema sababu kubwa ni wazazi kukosa muitikio mzuri kielimu na ukosefu wa vitendea kazi ikiwa ni pamoja magari katika idara ya elimu.

No comments: