
Na Juma
Mohamed, Mtwara.
CHAMA cha
Walimu Tanzania (CWT) mkoani hapa kimeendesha mafunzo ya siku tatu kwa viongozi
wa chama hicho kutoka katika ngazi ya mkoa, wilaya na vitengo vya wanawake, kwa
lengo la kuwajengea uwezo juu ya masuala mbalimbali yakiuongozi.
Mafunzo hayo
yaliyoratibiwa na baraza kuu la CWT Taifa na kuhusisha viongozi kutoka katika
wilaya zote za mkoa wa Mtwara, ndio yakwanza tangu kufanyika kwa uchaguzi mkuu
wa chama hicho mwezi Mei mwaka huu.
Wakizungumza
baada ya kufungwa kwa mafunzo hayo, baadhi ya walimu wamesema awali walikuwa
wakikabiliwa na changamoto nyingi za kiuongozi zaidi ikiwa ni juu ya matumizi
ya fedha za chama ambazo walishindwa kupanga mlolongo mzuri.
Mariam
Makubomula, kutoka halmashauri ya Mtwara vijijini, alisema alikuwa katika
wakati mgumu kuweza kujibu maswali ya wanachama ambao wengi wao walikuwa
wakihoji kuhusu asilimia zinazokatwa kutoka katika fedha za wanachama, ambapo
baada ya kupata mafunzo hayo atakua na majibu.
Mwenyekiti
wa Kitengo cha Walimu Wanawake (KE) Manispaa ya Mtwara Mikindani, Graceana
Nyoni, alisema miongoni mwa changamoto zinazowakabili walimu wanawake ni kipato
duni ambacho hakikidhi mahitaji yao kwa kila mwezi jambo linalopelekea kuwa na
maendeleo hafifu.
“Walimu
mishahara yao ni midogo, ukilingalisha na maisha ya hapa Mtwara mjini
haviendani kabisa..maisha hapa yapo juu sana, sasa mwalimu akisema aangaike na
mshahara tu ule hauwezi kutosha, anakuwa na majukumu mengi mwalimu utakuta
anakuwa na mikopo na mambo mengine mengi, lakini kwa msaada wa mafunzo haya
hapa tukienda kuwaelimisha wanachama wetu au walimu wanawake, tunaweza
tukatengeneza miradi mingi..” alisema.
Naye, Mgreth
Kalage, mwakilishi kutoka kitengo KE Manispaa ya Mtwara, alisema walimu wanawake
wengi wanapata changamoto ya walezi wa watoto wao inapotokea wamejifungua, na
kutakiwa kurudi kazini baada ya miezi mitatu kiasi cha kulazimika kuwaacha
watoto wao ambao ni wachanga wakilelewa na wasaidizi wa kazi.
Alisema,
itakuwa ni fursa kwa walimu hao iwapo wataamua kuanzisha kituo cha kulelea
watoto ambacho waaajiri wasichana maalum kwa ajili ya kazi hiyo ambao watakuwa
wapatiwa mafunzo ya shughuli hiyo.
Katibu wa
chama hicho, Fratten Kwahison, alisema kupitia mafunzo haoyo, walimu wameweza kupata
ufumbuzi wa mambo mbalimbali ambayo yalikuwa ni kikwazo kwao katika utendaji wa
kazi zao pamoja na mifumo dume ambayo ilikuwa ni changamoto kwa walimu wakike.
“Sisi kina
baba siku zote hatuwapi nafasi kina mama, utakuta anakua kiongozi lakini inapofikia
katika masuala ya maamuzi hatuwashirikishi vyakutosha..sasa kwenye semina hii
wameelimishwa na wamejua ni namna gani na wao wanaweza wakafanya yale majukumu
ambayo wanaume wanafanya..” alisema.
No comments:
Post a Comment