Na Juma Mohamed.
HALMASHAURI
ya Manispaa ya Mtwara Mikindani imewataka wananchi wanaotafuta ajira kuwa
makini na vitendo vya kitapeli vinavyofanywa na baadhi ya watu wanaojifanya
maafisa utumishi wa halmashauri, wakiwa na lengo la kujipatia fedha kwa njia ya
rushwa.
Akizungumza na
waandishi wa habari jana, Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri hiyo, Donald Nssoko,
alisema kumekuwa na utapeli unaofanywa na watu wasiojulikana ambao wanawapigia
simu watu ambao waliwahi kufanyiwa usaili katika halmashauri hiyo kwa kuwaambia
wanahitajika ofisini kwa ajili ya kupatiwa ajira.
Alisema,
jumla ya watu watatu kutoka maeneo tofauti hapa nchini wametapeliwa kiasi
tofauti cha fedha, baada ya kupigiwa simu na watu wanaojitambulisha kuwa wao ni
maafisa utumishi wa halmashauri hiyo, na kwamba wanahitaji fedha ili waweze
kuwapatia ajira walizoomba, kwani hakuna kitu kinachopatikana bure.
“Ni vizuri
kuweka taadhari kwa umma ili wananchi wetu wasiweze kupata hasara, na ndio
maana leo nimewaita ili tuwa taarifu wananchi kwamba wajihepushe wanapopigiwa
simu na watu wasiowafahamu ambao ni matapeli wakiwaeleza kwamba kuna nafasi
ambazo ziko wazi hapa manispaa ya Mtwara Mikindani..na sio watu wa mkoa wa
Mtwara iwe ni kwa nchi nzima, kwasababu kuna dada mmoja alipigiwa simu akiwa
yuko Kigoma..” alisema.
Alisema waliotapeliwa
ni Christina Rutayega mkazi wa Kigoma ambaye alitapeliwa kiasi cha sh. 120,000,
Glory Valentine mkazi wa Tanga sh. 200,000 na Maimuna Mohamed sh. 250,000.
Aidha, alisema
halmashauri hiyo ilipata kibali cha kuajiri watumishi wanane wa vitengo viwili
tofauti February 18 mwaka huu chenye kumbukumbu namba CB 170/362/01/C/63,
ambapo waliohitajika kuajiriwa ni watunzaji wa kumbukumbu wasaidizi wa daraja
la pili (4) na madereva wa daraja la pili (4).
Alisema halmashauri
ilifuata taratibu zote za kuendesha usaili na kwamba usaili wa mchujo
ulifanyika Mei 19 mwaka huu kwa nafasi zote, baada ya kupitia maombi ya 36 ya
waombaji.
“Kwa mantiki
hiyo, nafasi zote za waajiriwa kwa maana ya watunza kumbukumbu wasaidizi daraja
la pili nafasi nne na madereva wasaidizi daraja la pili nafasi nne..nafasi zote
hizo baada ya kukamilisha mchakato wa usaili, watahiniwa wote hao waliajiriwa..”
aliongeza.
Kwa upande
wake, Glory Valentine, ambaye alitapeliwa kiasi cha sh. 200,000 alisema,
alipigiwa simu na mtu ambaye alijitambulisha kama aifisa utumishi na kumuambia
kuwa kutokana na kwamba aliomba nafasi ya kuajiriwa katika manispaa ya Mtwara
Mikindani, anatakiwa amtumie kiasi hicho cha fedha ili aweze kupata ajira.
Alisema,
baada ya kuambiwa atume fedha hiyo, alifanya jitihada za kuipata na kisha
kumtumia ambapo aliambiwa atapigiwa simu na watu wa manispaa hiyo siku moja
baadae, lakini haikuwa hivyo na kwamba siku iliyofuata alipompigia simu kutaka
kumuuliza kwanini hajapigiwa, simu yake haikupokelewa.
“Siku ya nne
akanipigia simu na kuniuliza kama nilipigiwa, nikamjibu hapana..akanitafuta
tena siku iliyofuata akataka nimuongeze ten ash. 500,00, nikamuambua baba yangu
ameniambia mpaka atakapoiona hiyo barua ya kazi atakuongeza hata zaidi ya
hiyo..akataka nimpe namba ya baba, nikampa na akawasiliana naye..” alisema.
Na kuongeza “alivyowasiliana
naye akamwambia yeye aje tu kesho Mtwara, na barua yake nimemwambia mkurugenzi
asiende sehemu yeyote aje kuchukua kwangu alafu aje na hiyo hela..” aliongeza.
Alisema,
kabla ya kufunga safari ya Mtwara aliamua kuwasiliana na mtu aliyekuwa mkoani
hapa na kumuulizia kuhusu suala la ajira akamjibu kuwa swala hilo halipo,
ambapo hakuweza tena kusafiri na kuacha kuwasiliana naye tena kwa kujua tayari
ni tapeli.
Naye,
Christina Rutayega mkazi wa Kigoma, alisema alipigiwa simu na baba yake
akimweleza kuwa amepata kazi mkoani Mtwara na anatakiwa kuripoti kazini ndani
ya siku tatu, huku akisema amepewa taarifa hizo kwa njia ya simu na mtu aliejitambulisha
kwa jina la Mrisho.
Alisema baada
ya kuambiwa hivyo, alilazimika kusafiri siku ya pili yake mpaka Dar es Salaam
ambako alilala kabla ya kufika Mtwara siku iliyofuata na kupokelewa na rafiki
yake ambaye anafahamiana na afisa utumishi wa Manispaa hiyo.
“Nilivyomwambia
akasema ngoja kwanza niwasiliane na afisa utumishi wa pale, baada ya
kuwasiliana naye akaambiwa kwamba hakuna kitu kama hicho..tukampigia simu tena yule
mtu tukamwambia, na ilikuwa Jumapili, akasema wewe njoo kesho saa nne maana
asubuhi nitakuwa kwenye kikao..mimi nikaenda ile Jumatatu saa nne nikampigia
simu baada ya kufika, akaniambia ni subiri yupo sokoni.” Alisema
Na kuongeza “nikamwambia
sasa mboni unanisumbua hivi kaka, akasema wewe subiri, nikasubiri mpaka saa sita
ikabidi niondoke nikarudi nyumbani..” aliongeza.
Alisema,
ilikuwa rahisi kumuamini mtu huyo kwasababu aliyepigiwa simu ni mzazi wake na
kwamba namba ya simu aliyoitumia ilikuwa katika wasifu wake (CV) kwahiyo sio
kitu rahisi kwa mtu kuweza kuipata.
Wakati huo
huo kamanda wa Polisi mkoani hapa, Henry Mwaibambe, alisema matukio ya utapeli
ya aina hiyo yamekuwa mengi na kuwataka wananchi kutokubali wanapopigiwa simu
wakitakiwa kutoa pesa kwa ajili ya kutafutiwa kazi viandani au mahali sehemu
zingine.
Alisema,
alipgiwa simu na mtu kutoka wilayani Mkuranga akimweleza kuwa alipigiwa simu na
mtu ambaye yuko mkoani hapa na kumwambia kuwa amtumie fedha sh. 500,000 ili
apate kazi katika kiwanda cha Saruji cha Dangote, na kwamba tayari ameshamtumia
sh. 200,000.
No comments:
Post a Comment