Thursday, September 10, 2015

Kundi la mashabiki kutoka Dar kuwasili kesho kuishangilia Ndanda Sc.


Wachezaji wa timu ya Ndanda Sc ya mkoani Mtwara, wakipokea maelekezo kutoka kwa makocha wao, Hamimu Mawazo (Kocha Mkuu) na Ngawina Ngawina (Msaidizi) baada ya kumaliza mazoezi ya mwisho kabla ya kuingia uwanjani kesho kupambana na Mgambo Shooting ya Tanga katika mchezo wa ligi kuu ya Tanzania Bara.



Mlinda mlango namba moja wa timu ya Ndanda Sc,Nahodha, Wilbert Mweta, akizungumza na waandishi wa habari juu ya walivyojipanga kuelekea katika mchezo wao na Mgambo Shooting.



Msemaji wa mashabiki wa Ndanda Sc, George Wena, akizungumza na waandishi wa habari.


Na Juma Mohamed.

MASHABIKI wapatao 50 wa Ndanda Sc wanatarajiwa kuwasili mkoani Mtwara kesho wakitokea jijini Dar es Salaam na kuungana na wenzao wa mkoani humo kwa ajili ya kuishangilia timu hiyo siku ya Jumamosi itakapoteremka dimbani kuvaana na Mgambo Shooting ya Tanga, katika mchezo wa ligi kuu ya Tanzania Bara.
Akizungumza na East Africa Radio, msemaji wa mashabiki wa Ndanda mkoani humo, George Wena, amesema wanatarajia kuwapokea wenzao katika kijiji cha Hiyari, ambapo wanakuja kwa ajili ya kuongeza nguvu katika ushangiliaji ili kufanikisha ushindi kwa timu hiyo.
“Tunawaomba wadau na wakazi wote wa mkoa wa Mtwara, tunaomba waisapoti timu yetu kwasababi ni timu ambayo tunaitegemea kutupatia burudani katika mkoa wetu..na tujitolee kuhusu timu ili matatizo madogomadogo tuyamalize sisi wenyewe, na tusichanganye na mambomengine ya kisiasa..” alisema.
Alisema, wamejipanga vizuri kushangilia katika mchezo huo utakaopigwa katika uwanja wa Nangwana Sijaona, na wanaimani kubwa na timu yao kuibuka na ushindi hapo kesho kutokana na usajili uliofanywa chini ya kocha mkuu, Hamimu Mawazo.
Aidha, kocha Hamimu Mawazo alisema, kitu kikubwa kinachompa matumaini ya kuibuka na ushindi katika mchezo huo ni kuimarika katika idara zote, zaidi katika safu ya ulinzi na ushambuliaji ambazo msimu uliopita ndio zilikua na tatizo kubwa kiasi cha kuchangia kupata matokeo mabovu.
Alisema timu ikiwa na safu imara ya ulinzi inasaidia kuto ruhusu idadi kubwa ya magoli na kutoa nafasi kubwa kwa washambuliaji kupata morali ya kufumania nyavu za timu pinzani.
“Mwaka huu tunabahati kwamba maeneo yale yamepta marekebisho mazuri kwenye timu, ninaamini tutakuwa na timu nzuri ambayo itakuwa na uwezo wa kufunga na ninaamini ninamabeki wazuri wenye uwezo wa kuzuia kwenye upande wetu wa timu ya Ndanda..kwahiyo hayo mawili yakifanikiwa tutapata ushindi, na mimi naamini kwasababu wachezaji ambao wana uwezo wa kutuletea ushindi kwenye hiyo mechi ya Jumamosi..” alisema Mawazo.

Kocha mkuu wa timu ya Ndanda Sc, Hamimu Mawazo, akizungumza na waandishi wa habari, juu ya namna alivyokiandaa kikosi chake kwa ajili ya kuikabili Mgambo Shooting ya Tanga.

Alisema, kuhusu changamoto zingine za nje ya uwanja wanazokumbana nazo wachezaji, amekaa nao na kuzungumza nao ambapo wameonyesha kukubali na wote kuwa na lengo moja la ushindi kuelekea katika mchezo huo ambao ni miongoni mwa michezo saba ya ligi kuu itakayochezwa siku ya Jumamosi.
Kwa upande wake, Nahodha wa timu hiyo, Wilbert Mweta, aliwataka wachezaji wenzake kucheza kwa ushirikiano na kujituma zaidi huku wakifuata maelekezo ya mwalimu wao ili kufanikisha hadhma yao ya kuondoka na poiti tatu katika mchezo huo.
“Wachezaji wenyewe tujitume na tushirikiane uwanjani, tufuate maelekezo ya walimu wetu na ninaamini tutayafuata kwasababu tumejiandaa muda mrefu..jambo lingine la msingi ni kwamba mashabiki wetu wajitokeze waje kutusapoti kwasababu tupo katika uwanja wetu wa nyumbani ili tupate hamasa kubwa..” alisema.

No comments: