Thursday, December 4, 2014

DAR WAPELEKA KILIO TANGA




Dar Port


 
Tanga Port
                                                                         





Na Juma Mohamed, Mtwara

Timu ya soka ya Bandari ya Dar Es Salaam, Dar Port juzi ilifanikiwa kujipatia ushindi wake wa kwanza katika michuano ya nane ya Bandari Inter-Ports Games inayoendelea hapa mkoani Mtwara, baada ya kuichapa Tanga Port kwa jumla ya magoli matatu kwa sifuri katika mchezo uliofanyika Uwanja wa Nangwanda Sijaona.

Magoli ya washindi yalifungwa na Ramadhani Madebe na Selemani Muikwabe katika kipindi cha kwanza, kabla ya Selemani Muikwabe tena kupachika goli la tatu katika kipindi cha lala salama.

Akizungumza baada ya mchezo huo, kocha wa Dar Port, Elu Teli amesema mchezo huo ulionekana kuwa ni wa upande mmoja kutokana na wao kuutawala mchezo kwa kiasi kikubwa, na kuwafanya wapinzani wao wacheze nusu uwanja.

“Alafu kingine kilichofanya tuwazidi wapinzani wetu, ni kwamba wao ni wakongwe sana kuliko sisi”. Aliongeza.

Kwa upande wake kocha wa Tanga Port, Hamisi Rasi amesema wameathirika sana kwenye mchezo huo kutokana na wacezaji wake wengi kuwa majeruhi.

“Tuna wachezaji wanne ambao ni majeruhi..na wanacheza hasa katika nafasi ya kiungo, ndio sababu umeona leo tumezidiwa pale katikati. Lakini nina imani mchezo wa mwisho ambao tutacheza na Ziwa tutajitahidi tushinde angalau tupate nafasi ya tatu”. Alisema Rasi.

Mchezo huo ulitanguliwa na mchezo kati ya wenyeji Mtwara Port waliokipiga na Maziwa, ambapo wenyeji walifanikiwa kupata usindi wa goli 1-0, goli ambalo lilifungwa na Amphley Kachamile. Kwa matokeo hayo, Mtwara wamefanikiwa kufikisha alama saba baada ya kucheza michezo mitatu ambapo wameshinda miwili na kutoa suluhu mchezo mmoja na kufanikiwa kuongoza, wakifuatiwa na Dar Port waliocheza michezo miwili, wakishinda mmoja na kwenda sare mmoja, ambapo wamefikisha alama 4.

Maziwa wao wanakamata nafasi ya tatu wakiwa na alama 3 baada ya kuteremka dimbani mara mbili, ambapo wameshinda mchezo mmoja na kupoteza mmoja.

Michuano hiyo inayofanyika kila mwaka nakushirikisha timu zote tano za Bandari za Tanzania Bara, ilianza kutimua vumbi Jumatatu ya Desemba 1, mwaka mwaka huu na inataraji kufikia Tamati siku ya Ijumaa, Desemba 05, mwaka huu.





No comments: