Tuesday, October 16, 2012

MBAGA AZICHEZESHA KENYA, BAFANA BAFANA


Mwamuzi Oden Mbaga wa Tanzania anayetambuliwa na Shirikisho la Kimataifa la Mpira wa Miguu (FIFA) ndiye anayechezesha mechi ya kirafiki kati ya Kenya (Harambee Stars) na Afrika Kusini (Bafana Bafana).
 
Mechi hiyo inachezwa leo Uwanja wa Kimataifa wa Moi Kasarani jijini Nairobi. Mbaga anasaidiwa na waamuzi wasaidizi wa FIFA, John Kanyenye kutoka Mbeya na Erasmo Jesse wa Morogoro.
 
TFF imeteua waamuzi hao baada ya kupata maombi kutoka kwa Shirikisho la Mpira wa Miguu la Kenya (FKF) ambao ndiyo waandaaji wa mechi hiyo ambayo ni moja ya vipimo kwa kocha mpya wa Harambee Stars, Henry Michel kutoka Ufaransa.
 
TAFCA YAONGEZA MUDA WA KUCHUKUA FOMU
Kamati ya Uchaguzi ya Chama cha Makocha wa Mpira wa Miguu Tanzania (TAFCA) imeongeza muda kwa wagombea kuchukua fomu kwa ajili ya uchaguzi wa chama hicho ambao sasa utafanyika Novemba 25 mwaka huu.
 
Kwa mujibu wa Mwenyekiti wa Kamati ya Uchaguzi ya TAFCA, Ramadhan Mambosasa, jana ndiyo ilikuwa mwisho wa kuchukua fomu lakini mwitikio wa wagombea bado umekuwa mdogo ambapo ni watano tu waliojitokeza.
 
Hivyo, amesema wameongeza muda wa kuchukua na kurudisha fomu ambapo mwisho itakuwa ni Oktoba 19 mwaka huu saa 10 kamili alasiri. Fomu zinapatikana ofisi za TAFCA ambazo ziko Uwanja wa Kumbukumbu ya Karume, Dar es Salaam.
 
Nafasi zinazogombewa ni Mwenyekiti, Makamu Mwenyekiti, Katibu Mkuu, Katibu Msaidizi, Mjumbe wa Mkutano Mkuu wa TFF, Mhazini na wajumbe watatu wa Kamati ya Utendaji.
 

No comments: