Mateka Yondan |
Na Mahmoud Zubeiry
WAKATI leo Kamati ya Sheria, Maadili na
Hadhi za Wachezaji ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), chini ya Mwenyekiti
wake, Alex Mgongolwa inatarajiwa kutoa uamuzi kuhusu kesi za mabeki wawili wa
Yanga, Mbuyu Twite na Kevin Yondan, ambao usajili wao unapingwa na Simba, sakata
hilo limechukua sura mpya jana.
Inadaiwa Yondan jana alitekwa na klabu
yake ya zamani, Simba SC katika kile kinachoelezwa jitihada za kumrudisha
nyumbani, lakini dili hilo likakwama baada ya mchezaji mwenyewe kuwatoroka
viongozi wa Simba.
Akizungumza na BIN ZUBEIRY jana usiku,
Mjumbe wa Kamati ya Utendaji ya Yanga, Abdallah Ahmad Bin Kleb alisema kwamba
mchezaji wa zamani wa Simba, ambaye aliwahi kukutwa na kashfa ya kutaka
kumhonga mchezaji wa timu pinzani akitumiwa na klabu yake hiyo, ndiye
aliyemuingiza Yondan kwenye mtego.
“……..alikwenda kwa Yondan, akasema
amekwenda kumsalimia na kwa kuwa wanafahamiana wamewahi kucheza wote wa Simba,
Yondan hakuwa na tatizo. Baada ya mazungumzo akaaga anaondoka, akaomba
asindikizwe hadi mjini, kufika mbele kidogo, yule mchezaji akaomba aendeshe
gari la Yondan. Yondan akampa.
Yule jamaa akapeleka lile gari moja kwa
moja hadi kwa…………..(kiongozi wa juu wa Simba), kufika wakaingia ndani, Yondan
anamuuliza huku wapi tena, ooh naenda kuchukua mpunga (fedha) kidogo kwa…..(huyo
kiongozi). Walipofika, akamshawishi Yondan waingie naye ndani, na kwa kuwa
Yondan alikuwa anajiamini, akashuka wakaingia.
Kufika, jamaa (kiongozi) akamtolea (Yondan)
Sh. Milioni 20 ili asaini fomu za Simba na muda ule ule azungumze na Radio
Clouds kutangaza kwamba yeye ni mchezaji halali wa Simba, Yondan akakataa. Jamaa
akaongeza burungutu la fedha, bado mchezaji akakataa. Alipoona anazidi kubanwa,
akaomba aende chooni mara moja. Ndipo alipotoka akampigia simu Seif (Ahmad ‘Magari’)
kumuambia haraka haraka kinachoendelea.
Seif akamuambia ajitahidi atoke nje ya jengo
hilo na gari lake aliache tu humo ndani, kwa kuwa ufunguo wa gari lake alikuwa
nao huyo mchezaji aliyetumwa, wale kule wakajiamini atarudi tu. Yondan
akafanikiwa kutoka na anafika tu nje ya geti, tayari mtu kafika kumchukua na
baada ya muda Seif naye akafika.
Kule ndani walipoona Yondan harudi, yule
mchezaji akatumwa kutoka kumfuatilia, akatoka nje akakutana na Seif, akamkamata
akampakia kwenye gari akaondoka nao wote.
Sema naye yule (mchezaji aliyetumwa) kule
mbele akafanikiwa kumtoroka Seif, ila kesi imefunguliwa Polisi dhidi ya huyo
kiongozi wa Simba na huyo mchezaji. Na aliyefungua ni Yondan mwenyewe. Sasa hii
ndio picha halisi,”alidai Bin Kleb.
Ikumbukwe, mapema Jumatatu wiki
iliyopita, kikao cha baina ya klabu hizo mbele ya Kamati ya Sheria, Maadili na
Hadhi za Wachezaji ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), chini ya Mwenyekiti
wake, Alex Mgongolwa, kilivunjika bila kufikia makubaliano kuhusu pingamizi za
Simba dhidi ya Yanga.
Katika kikao hicho kilichoanza majira ya
saa 7:00 mchana, hoja ya kwanza kuwasilishwa mezani ilikuwa ni suala la beki
Twite na upande wa Yanga uliwakilishwa na Sanga na Katibu, Celestine Mwesigwa
wakati kwa Simba walikuwepo Makamu Mwenyekiti, Geoffrey Nyange ‘Kaburu’ na
Mwenyekiti wa Kamati ya Usajili, Kapteni wa zamani wa Jeshi la Wananchi
Tanzania (JWTZ), Zacharia Hans Poppe.
Ikumbukwe, Simba iliwasilisha malalamiko
ya kufanyiwa mchezo usio wa kiungwana na Yanga kwa Twite. Ilidai Twite alisaini
mkataba na klabu yao Agosti 1, mwaka huu mbele yao, viongozi wa Shirikisho la
Soka Rwanda (FERWAFA) na APR na kulipwa dola za Kimarekani 30,000 na nyingine
2,000 za nauli ya kuja Dar es Salaam kujiunga na klabu hiyo. Hata hivyo,
mchezaji huyo akahamia Yanga.
Katika mjadala huo, Simba ilikubali
kurudishiwa fedha zao, lakini viongozi wa Yanga wakasema hawawezi kutoa hadi
waombwe radhi na Mwenyekiti wa Simba, Alhaj Ismail Aden Rage, ambaye alisema
viongozi wa klabu hiyo yenye maskani yake makutano ya mitaa ya Twiga na
Jangwani wana ‘fedha chafu za EPA’.
Simba wakasema kauli yake ya Rage
ilikuwa sehemu ya utani wa jadi, kama ambavyo Yanga walimvalisha jezi Twite
yenye jina la Rage.
Kufikia hapo, Simba wakasema hawawezi
hata kujadili suala la Kevin Yondan na Kamati ya Mgongolwa ikasema itapitia
maelezo ya pande zote, watatoa majibu kwa mujibu wa kanuni na sheria Septemba
10, mwaka huu, yaani leo.
Katika kesi ya Yondan, walalamikaji ni
Simba, ambao wanadai beki huyo alisaini Yanga akiwa bado ana mkataba na klabu
yao.
Awali, Kamati ya Mgongolwa ilikutana
Jumapili iliyopita asubuhi hadi usiku, bila kupata suluhisho la pingamizi hizo
na kuamua kutumia busara ya kuzikutanisha pande zinazopingana kujaribu kupata
suluhu siku iliyofuata.
Pingamizi nyingine zilikuwa ni, Azam inayopinga
usajili wa Ramadhan Chombo ‘Redondo’ kwenda Simba kwa maelezo bado ina mkataba
naye unaomalizika Juni 11 mwakani na inaelezwa tayari klabu hizo
zimekwishamalizana juu ya kiungo huyo.
Yanga inapinga Simba kuwaacha wachezaji
Dan Mrwanda, Haruna Shamte, Kanu Mbiyavanga na Lino Masombo kwa maelezo
walishapatiwa leseni za kucheza Ligi ya Tanzania walizozitumia kwenye
mashindano ya Kombe la Kagame. Pia inapinga Ramadhan Chombo ‘Redondo’ kujiunga
Simba kwa vile ana leseni ya kuchezea Azam kwa msimu wa 2012/2013.
Pingamizi lingine la Yanga kwa Simba ni
kuwa imezidisha idadi ya wachezaji wa kigeni wanaotakiwa kusajiliwa kwa maelezo
inao wanane wakati wanaoruhusiwa ni watano. Imewataja wachezaji hao kuwa ni
Lino Masombo, Felix Sunzu, Emmanuel Okwi, Mussa Mude, Kanu Mbiyavanga, Pascal
Ochieng, Komalmbil Keita na Daniel Akuffor.
Pingamizi nyingine ambazo jumla zinahusu
wachezaji 17 walioombewa usajili katika timu za Ligi Kuu ni Toto Africans ya
Mwanza imewawekea pingamizi wachezaji Enyinna Darlington aliyeombewa usajili
Kagera Sugar, na Mohamed Soud anayekwenda Coastal Union kwa maelezo kuwa bado
ina mikataba na wachezaji hao.
Pia Flamingo ya Arusha inapinga usajili
wa wachezaji wake Kelvin Friday Iddy katika timu za Azam na Salim Walii (Polisi
Mara) kwa vile taratibu za kuwahamisha bado hazijafanywa. Nayo Kagera Sugar
inapinga usajili wa beki David Charles Luhende kwenda Yanga kwa vile ada ya uhamisho
haijalipwa.
Super Falcon ya Chanjamjawiri,
Chakechake, Pemba inapinga wachezaji wake wanne; Edward Christopher Shija,
Samir Said Luhava (Simba), Robert Joseph Mkhotya (African Lyon) na Sultan Juma
Shija (Coastal Union) kusajiliwa katika timu hizo kwa maelezo taratibu halali
za uhamisho hazikufuatwa.
Mchezaji Othman Hassan aliyeombewa
usajili Coastal Union anapingwa na Oljoro JKT kwa vile bado ana mkataba na timu
hiyo unaomalizika Mei 24, 2013. Nayo Rollingstone Multipurpose Ateclass
Foundation ya Arusha inapinga usajili wa Kigi Makassy kutoka Yanga kwenda Simba
hadi itakapolipwa fidia ya kumlea mchezaji huyo kwa vile bado hajafikisha umri
wa miaka 23. Pingamizi zote zitatolewa majibu leo na Kamati ya Mgongolwa.SOURCE:BIN ZUBEIRY
No comments:
Post a Comment