Monday, September 10, 2012

SERENGETI BOYS YAENDELEA KUJINOA MBEYA


Timu ya Taifa ya vijana wenye umri chini ya miaka 17 (Serengeti Boys) inaendelea vizuri na kambi ya mazoezi mkoani Mbeya ambapo tayari imecheza mechi moja ya kujipima nguvu.
 
Ilicheza mechi hiyo jana (Septemba 8 mwaka huu) dhidi ya Tanzania Prisons iliyoko Ligi Kuu ya Vodacom kwenye mji wa Nakonde ulioko mpakani mwa Tanzania na Zambia. Timu hizo zilitoka sare ya 1-1 huku bao la Serengeti Boys likifungwa na Miraji Selemani.
 
Serengeti Boys leo jioni (Septemba 9 mwaka huu) inatarajia kucheza mechi nyingine wilayani Mbozi dhidi ya Mbozi United. Itacheza mechi ya tatu Jumanne (Septemba 11 mwaka huu) jijini Mbeya dhidi ya timu ya daraja la kwanza ya Mbeya City.
 
Kwa mujibu wa Kocha wa timu hiyo, Jakob Michelsen kambi hiyo inaendelea vizuri, na anatarajia kupata mechi moja ya kirafiki ya kimataifa kabla ya kucheza mechi ya mashindano na Misri, Oktoba 13 mwaka huu Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
 
PONGEZI KWA UONGOZI MPYA IRFA
Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) linatoa pongezi kwa uongozi mpya wa Chama cha Mpira wa Miguu Mkoa wa Iringa (IRFA) uliochaguliwa katika uchaguzi uliofanyika jana (Septemba 9 mwaka huu) mjini Iringa.
 
Ushindi waliopata viongozi waliochaguliwa kuongoza chama hicho unaonesha jinsi wajumbe wa Mkutano Mkuu wa IRFA walivyo na imani kubwa kwao katika kusimamia mchezo huo mkoani Iringa.
 
TFF inaahidi kuendeleza ushirikiano wake kwa Kamati ya Utendaji ya IRFA chini ya uenyekiti wa Cyprian Kuyava ambaye amechaguliwa kuongoza chama hicho kwa mara ya kwanza.
 
Uongozi huo mpya una changamoto nyingi, kubwa ikiwa ni kuhakikisha unaendesha shughuli za mpira wa miguu mkoani Iringa kwa kuzingatia katiba ya IRFA pamoja na vyombo vya mpira wa miguu vilivyo juu yake.
 
Pia tunatoa pongezi kwa Kamati ya Uchaguzi ya IRFA na Kamati ya Uchaguzi ya TFF kwa kuhakikisha uchaguzi huo unaendeshwa kwa mujibu wa kanuni za uchaguzi za wanachama wa TFF.
 
Viongozi waliochaguliwa katika uchaguzi huo ni Cyprian Kuyava (Mwenyekiti), Stanford Mwakasala (Makamu Mwenyekiti), Eliud Mvella (Katibu) na John Ambwene (Katibu Msaidizi).
 
Wengine ni Ramadhan Mahano (Mjumbe wa Mkutano Mkuu TFF), Coaster Magoloso (Mwakilishi wa Klabu TFF), Abdallah Kiyumbo (Mhazini), wakati wajumbe wa Kamati ya Utendaji ni Maulid Tofi na David Mwamalekela.
 

No comments: