Monday, September 10, 2012

KIIZA AREJEA JANGWANI KUIONGEZEA NGUVU YANGA


Kiiza baada ya kutua Uwanja Ndege akiwa amepokewa na watoto wa rafiki yake, Abdulsamad
  
Kiiza akiwa na rafiki yake Abdulsamad aliympokea Uwanja wa Ndege.

Na Mahmoud Zubeiry
HAMISI Kiiza ‘Diego’ amerejea jioni hii mjini Dar es Salaam, akitokea kwao, Uganda ambako alikuwa ana majukumu ya kitaifa na tayari amejiunga na wenzake kwa ajili ya mchezo wa kwanza wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara, dhidi ya Prisons mjini Mbeya mwishoni mwa wiki.
Kiiza hakuwa na Yanga kwa takriban wiki mbili, akiwa kwao kwa ajili ya kuichezea timu yake ya taifa, The Cranes mechi ya kuwania tiketi ya kucheza Fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika mwakani nchini Afrika Kusini.
Katika mechi hiyo iliyochezwa Jumamosi mjini Lusaka dhidi ya wenyeji, Zambia, Koronga wa Uganda alifungwa 1-0 na sasa anahitaji ushindi wa 2-0 katika mchezo wa marudiano nyumbani, ili kusonga mbele.   
Kiiza ni mmoja kati ya wapachika mabao hodari, ambao kocha Mkuu wa Yanga, Mbelgiji Tom Saintfiet ‘Mtakatifu Tom’ anajivunia na amesema kwamba anatarajia mvua ya mabao katika mechi za Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara, kutokana na uwezo mkubwa wa kufunga wa wachezaji wake, kuanzia mabeki, viungo hadi washambuliaji.
Akizungumza na BIN ZUBEIRY jana, Mtakatifu Tom alisema kwamba mbali na washambuliaji kufunga, pia mabeki wake na viungo wanafunga pia, na hilo linampa faraja sana.
Jana Yanga ilicheza mechi ya mwisho ya kujipima nguvu kabla ya kuanza kwa Ligi Kuu na kushinda mabao 4-0 dhidi ya Moro united, Mrundi Didier Kavumbangu akifunga mawili, mengine beki Juma Abdul na kiungo Shamte Ally. 
“Kavumbangu aliwahi kufunga pia tulipocheza na Sinza Stars, ninafurahia hilo, ni muhimu kwa klabu kubwa, lakini pia wachezaji wengine wanaweza kufunga, Stefano Mwasyika, Nadir Haroub ‘Cannavaro’, Juma Abdul…tumecheza mechi 14 kabla ya ligi, zikiwemo dhidi ya Sinza Stars na Kijitonyama Stars, tumefunga mabao 42 na tumefungwa sita tu,”alisema Mtakatifu Tom.
Saintfiet alitaka mechi moja dhidi ya timu inayocheza kama wapinzani wao wa kwanza katika Ligi Kuu, Prisons na pia katika Uwanja mbaya kama ambao atachezea mechi ya kwanza ya ligi hiyo, Sokoine mjini Mbeya na ndiyo maana timu hiyo ikacheza na Moro United juzi kwenye Uwanja wa Shule ya Msingi Kijitonyama.
Saintfiet ameridhika na kiwango cha timu na sasa anasema timu iko tayari kwa Ligi Kuu, akianza na Prisons iliyorejea Ligi Kuu msimu huu kwenye Uwanja wa Sokoine, Septemba 15.
Hiyo ilikuwa mechi ya 11, Saintfiet anashinda Yanga katika mechi 12 tangu ajiunge nayo miezi miwili iliyopita, mbali ya ziwe za mazoezini dhidi ya Sinza Stars na Kijitonyama Stars.
Ndani ya mechi hizo kuna mechi sita za Klabu Bingwa ya soka Afrika Mashariki na Kati, Kombe la Kagame, ambalo aliiwezesha Yanga kutwaa ubingwa wa tano wa michuano hiyo, ikipoteza mechi moja tu ya kwanza dhidi ya Atletico ya Burundi, kwa kufungwa 2-0, mabao yote ya Kavumbangu, ambaye baadaye ikamsajili.  
REKODI YA SAINTFIET YANGA
1.                      Yanga Vs JKT Ruvu 2-0
2.                      Yanga Vs Atletico (Burundi) 0-2
3.                      Yanga Vs Waw Salam (Sudan Kusini) 7-1
4.                      Yanga Vs APR (Rwanda) 2-0
5.                      Yanga Vs Mafunzo (Z’bar) 1-1 (5-3penalti)
6.                      Yanga Vs APR (Rwanda) 1-0
7.                      Yanga Vs Azam 2-0
8.                      Yanga Vs African Lyon 4-0
9.                      Yanga Vs Rayon (Rwanda) 2-0
10.             Yanga Vs Polisi (Rwanda) 2-1
11.             Yanga Vs Coastal Union 2-1
12.             Yanga Vs Moro United 4-0

SOURCE:BIN ZUBEIRY

No comments: