Tuesday, September 4, 2012

SAKATA LA TWITE NA YONDANI BADO ZITO KWA MGONGOLWA

 


 
Mbuyu Twite

 
KLABU za Simba na Yanga zimeshindwa kufikia suluhu mbele ya Kamati ya Sheria, Maadili na Hadhi za Wachezaji ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), chini ya Mwenyekiti wake Alex Mgongolwa, katika kikao cha leo, juu ya wachezaji Kevin Yondan na Mbuyu Twite.
Katika kikao hicho kilichoanza majira ya saa 7:00 mchana, hoja ya kwanza kuwasilishwa mezani ilikuwa ni suala la beki Twite na upande wa Yanga uliwakilishwa na Makamu Mwenyekiti, Clement Sanga na Katibu, Celestine Mwesigwa wakati kwa Simba walikuwepo Makamu Mwenyekiti, Geoffrey Nyange ‘Kaburu’ na Mwenyekiti wa Kamati ya Usajili, Kapteni wa zamani wa Jeshi la Wananchi Tanzania (JWTZ), Zacharia Hans Poppe.
Ikumbukwe, Simba iliwasilisha malalamiko ya kufanyiwa mchezo usio wa kiungwana na Yanga kwa Twite. Ilidai Twite alisaini mkataba na klabu yao Agosti 1, mwaka huu mbele yao, viongozi wa Shirikisho la Soka Rwanda (FERWAFA) na APR na kulipwa dola za Kimarekani 30,000 na nyingine 2,000 za nauli ya kuja Dar es Salaam kujiunga na klabu hiyo. Hata hivyo, mchezaji huyo akahamia Yanga.
Katika mjadala huo, Simba ilikubali kurudishiwa fedha zao, lakini viongozi wa Yanga wakasema hawawezi kutoa hadi waombwe radhi na Mwenyekiti wa Simba, Alhaj Ismail Aden Rage, ambaye alisema viongozi wa klabu hiyo yenye maskani yake makutano ya mitaa ya Twiga na Jangwani wana ‘fedha chafu za EPA’.
Simba wakasema kauli yake ya Rage ilikuwa sehemu ya utani wa jadi, kama ambavyo Yanga walimvalisha jezi Twite yenye jina la Rage.
Kufikia hapo, Simba wakasema hawawezi hata kujadili suala la Kevin Yondan na Kamati ya Mgongolwa ikasema itapitia maelezo ya pande zote, watatoa majibu kwa mujibu wa kanuni na sheria Septemba 10, mwaka huu.
Katika kesi ya Yondan, walalamikaji ni Simba, ambao wanadai beki huyo alisaini Yanga akiwa bado ana mkataba na klabu yao.
Awali, Kamati ya Mgongolwa ilikutana Jumapili asubuhi hadi usiku, bila kupata suluhisho la pingamizi hizo na kuamua kutumia busara ya kuzikutanisha pande zinazopingana kujaribu kupata suluhu leo.
Pingamizi nyingine zilikuwa ni, Azam inayopinga usajili wa Ramadhan Chombo ‘Redondo’ kwenda Simba kwa maelezo bado ina mkataba naye unaomalizika Juni 11 mwakani na inaelezwa tayari klabu hizo zimekwishamalizana juu ya kiungo huyo.
Yanga inapinga Simba kuwaacha wachezaji Dan Mrwanda, Haruna Shamte, Kanu Mbiyavanga na Lino Masombo kwa maelezo walishapatiwa leseni za kucheza Ligi ya Tanzania walizozitumia kwenye mashindano ya Kombe la Kagame. Pia inapinga Ramadhan Chombo ‘Redondo’ kujiunga Simba kwa vile ana leseni ya kuchezea Azam kwa msimu wa 2012/2013.
Pingamizi lingine la Yanga kwa Simba ni kuwa imezidisha idadi ya wachezaji wa kigeni wanaotakiwa kusajiliwa kwa maelezo inao wanane wakati wanaoruhusiwa ni watano. Imewataja wachezaji hao kuwa ni Lino Masombo, Felix Sunzu, Emmanuel Okwi, Mussa Mude, Kanu Mbiyavanga, Pascal Ochieng, Komalmbil Keita na Daniel Akuffor.
Pingamizi nyingine ambazo jumla zinahusu wachezaji 17 walioombewa usajili katika timu za Ligi Kuu ni Toto Africans ya Mwanza imewawekea pingamizi wachezaji Enyinna Darlington aliyeombewa usajili Kagera Sugar, na Mohamed Soud anayekwenda Coastal Union kwa maelezo kuwa bado ina mikataba na wachezaji hao.
Pia Flamingo ya Arusha inapinga usajili wa wachezaji wake Kelvin Friday Iddy katika timu za Azam na Salim Walii (Polisi Mara) kwa vile taratibu za kuwahamisha bado hazijafanywa. Nayo Kagera Sugar inapinga usajili wa beki David Charles Luhende kwenda Yanga kwa vile ada ya uhamisho haijalipwa.
Super Falcon ya Chanjamjawiri, Chakechake, Pemba inapinga wachezaji wake wanne; Edward Christopher Shija, Samir Said Luhava (Simba), Robert Joseph Mkhotya (African Lyon) na Sultan Juma Shija (Coastal Union) kusajiliwa katika timu hizo kwa maelezo taratibu halali za uhamisho hazikufuatwa.
Mchezaji Othman Hassan aliyeombewa usajili Coastal Union anapingwa na Oljoro JKT kwa vile bado ana mkataba na timu hiyo unaomalizika Mei 24, 2013. Nayo Rollingstone Multipurpose Ateclass Foundation ya Arusha inapinga usajili wa Kigi Makassy kutoka Yanga kwenda Simba hadi itakapolipwa fidia ya kumlea mchezaji huyo kwa vile bado hajafikisha umri wa miaka 23.
 
SOURCE:BIN ZUBEIRY

No comments: