Wednesday, September 5, 2012

SAINTFIET ASIFU UKUTA WA YANGA,ASEMA OKWI KAZI ANAE 0KTOBA 3


 http://www.mwanaspoti.co.tz/edittext/image/13749.
KOCHA Mkuu wa Yanga, Tom Saintfiet amesema amemsoma nyota wa Simba, Emmanuel Okwi na kujigamba kuwa hatafurukuta wakati timu hizo zenye upinzani wa jadi zitakapokabiliana Oktoba 3, kwenye mechi ya Ligi Kuu Tanzania Bara.

Mechi hiyo itapigwa kwenye Uwanja wa Taifa Dar es Salaam.

Akizungumza na Mwanaspoti, Saintfiet, ambaye amejizolea sifa baada ya kuifanya beki ya Yanga kutopitika kirahisi, alisema amewapa mbinu nyingi mabeki wake ili kuwadhibiti washambuliaji wakali wa Ligi Kuu akiwamo Okwi.

Alitolea mfano wa umahiri wa beki yake kwenye Kombe la Kagame wakati Yanga ilipotwaa taji hilo baada ya kuruhusu mabao manne tu kiasi cha kufananishwa na 'Ukuta wa Berlin' na gazeti hili.

Fomesheni ya kumdhibiti Okwi
Okwi anayesifika kwa kuwa machachari uwanjani atapaswa kutuliza kichwa na kutafuta ujanja wa kuvunja ukuta wa Yanga kama atataka kurudia alichofanya Mei 6, mwaka huu dhidi ya timu hiyo.

Mganda huyo alifunga mabao mawili na kusababisha penalti tatu wakati timu hizo zilipokutana kwenye mechi ya mwisho ya kumalizia msimu uliopita wa Ligi Kuu Tanzania Bara na Yanga ikacharazwa 5-0.

Baada ya kichapo hicho, kocha wa muda wa Yanga wakati huo, Fred Felix 'Minziro' alilia na mabeki wake kwa kumwachia Okwi kufanya anavyotaka.

Minziro ambaye ni beki wa zamani wa kushoto wa Yanga, amesema safari hii itakuwa mambo mengine kwani wana beki imara.

Okwi ambaye alifunga mabao 12 kwenye Ligi Kuu msimu uliopita, atakuwa chini ya ulinzi wa mabeki watano wa Yanga.
Ngome ya Yanga imeimarika zaidi siku hizi kufuatia fomesheni mpya ya Saintfiet.

Saintfiet anatazamiwa kutumia mfumo wa 5-1-2-2 akiwapanga mabeki, Juma Abdul, Oscar Joshua, Kelvin Yondani, Mbuyu Twite na Nadir Haroub 'Cannavaro' ili kumdhibiti Mganda huyo.

"Okwi nimemfuatilia sana katika mechi za klabu yake na timu ya taifa ya Uganda na ninafahamu uwezo wake vizuri.

"Ni mchezaji mzuri na msumbufu uwanjani lakini pamoja na ubora wake mbele ya ukuta wangu hataambulia chochote, ninaamini beki yangu kwa asilimia 100. Wanaweza kumzuia mtu yeyote," alisema Saintfiet.

Okwi anaweza kuwa katika wakati mgumu kama ilivyotokea kwa mshambuliaji wa hatari wa zamani wa Simba, Zamoyoni Mogella 'Golden Boy'.

Ilikuwa mwaka 1983 wakati Mogella akiwa na Simba iliyokuwa imeshuka kutoka Brazil na fomesheni ya 'Diagnol Samba', alidhibitiwa na mabeki watano wa Yanga kwenye Ligi Kuu mwaka 1983.

Yanga ikinolewa na Mjerumani Rudi Gutendorf aliyesuka beki hiyo na kuasisi jina la utani la 'Ukuta wa Berlin', iliwatumia Yussuf Bana, Ahmed Masha, Athumani Juma 'Chama', Allan Shomari na Charles Boniface ili kumdhibiti Mogella na katika mchezo huo Yanga ilishinda 3-1.

Simba nayo si ya kuchezea
Tofauti na Simba iliyoboronga Kombe la Kagame, timu hiyo imefanya kazi kubwa katika kuimarisha kikosi chake.

Ujio wa mshambuliaji Daniel Akuffo umeleta uhai mpya katika timu hiyo yenye makao yake makuu katika Mtaa wa Msimbazi jijini Dar es Salaam.

Raia huyo wa Ghana ametua kwa kishindo kwani amefunga mabao katika mechi zote alizoichezea Simba kambini mjini Arusha.

Mghana huyo ambaye ni mrefu na mwenye nguvu, alizamisha mabao katika mechi za dhidi ya JKT Oljoro ya Tanzania, Mathare United na Sony Sugar za Kenya.

Kutokana na hali hiyo, lazima Yanga waumize kichwa kwani Akuffo, Mzambia Felix Sunzu na Mtanzania Abdalla Juma wanaifanya Simba kuimarika zaidi.

Yanga wakifanya kosa la kumchunga Okwi pekee, watakuwa wanajichimbia kaburi kwani Akuffo, Sunzu na Abdallah nao wanaweza kuleta madhara makubwa.

Saintifiet akiizungumzia Simba, alisema ni timu nzuri ila dawa yao inaiva jikoni.

"Mechi ya Simba itakuwa ngumu na nzuri, siogopi na sina wasiwasi nao, hata hivyo sitaki kuwazungumzia sana, tusubiri muda ufike.
"Unajua nataka kushinda kila mechi na hizi za kwanza ndizo zinachanganya kutokana na ratiba walivyopanga ingawa sina wasiwasi."
SOURCE:MWANA SPOTI 

No comments: