Monday, June 25, 2012

MASHALI SASA AWATAKA CHEKA, KASEBA

 

Mashali akivalishwa mkanda wake wa ubingwa baada ya kuutetea jana kwa kumtwanga TKO raundi ya tano Maisha


Na Prince Akbar
BAADA ya kumtwanga kwa Technical Knockout (TKO) raundi ya tano Samson Maisha wa Mbeya, bingwa wa Taifa wa TPBO, Thomas Mashali 'Simba wa Teranga' amesema anamtaka mshindi wa pambano kati ya Japhet Kaseba na Francis Cheka apande naye ulingoni, ili adhihirishe yeye ndiye ‘king’ wa ndondi Tanzania.
Mashali akiwa amemdondosha Maisha jana
Akizungumza na BIN ZUBEIRY kwenye ukumbi wa Friends Corner, Manzese jana baada ya ushindi wake huo, Mashali alisema kwamba anaamini kwa sasa katika nchi hii hana mpinzani na ameomba yeyote atakayeshinda kati ya Kaseba na Cheka asikwepe kupanda naye ulingoni.
“Huyu mtoto (Maisha), si saizi yangu, wamempakazia tu, baada ya kuona mabondia wote wa Dar es Salaam sasa hivi wananiogopa, nilikuwa nampiga huku namhurumia, na bado amefia katikati ya safari (raundi ya tano). Namtaka mshindi kati ya Kaseba na Cheka,”alisema Mashali.
Katika pambano hilo la jana la uzito wa Middle, Mashali alimzidi uwezo mpinzani wake kuanzia raundi ya kwanza na katika raundi ya tano alimkalisha chini kwa ngumi kali ya mkono wa kulia.
Maisha alijitutumua kuinuka ili aendelee na pambano, lakini alionekana dhahiri hajiwezi na ndipo Kocha wake, Bagaza Mambane akarusha taulo ulingoni. Hata hivyo, Maisha anaonekana ni bondia mzuri akipata mazoezi zaidi na ujanja wa mjini.

NGASSA AJISALIMISHA AZAM FC, BOCCO 'HASOMEKI'


Ngassa mazoezini Azam FC

Na Prince Akbar
WACHEZAJI wa Azam FC waliokuwa na timu ya taifa ya Tanzania, Taifa Stars akiwemo Mrisho Khalfan Ngassa anayevumishiwa kuwa katika mpango wa kurejea klabu ya zamani, Yanga leo wameanza mazoezi rasmi na timu hiyo, kwa maandalizi ya klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati, Kombe la Kagame.
Kutoka Azam, BIN ZUBEIRY imeelezwa kwamba, wachezaji wanne hawakufanya mazoezi leo asubuhi, kwa sababu ambazo hazikuweza kufahamika mara moja, hao ni makipa Deo Munishi ‘Dida’ na Mwadini Ally na viungo Waziri Salum na Jabir Aziz na mshambuliaji John Bocco ‘Adebayor’.
Waziri aliripoti kambini wiki iliyopita na kutoa taarifa ya kuuguliwa na baba yake akarejea Zanzibar na Stima alikuwepo tangu mazoezi yanaanza, wakati Bocco alikuwa Taifa Stars.
Wachezaji wengine waliokuwa na timu ya taifa ya Zanzibar, Zanzibar Heroes kwenye michunao ya Kombe la Dunia ya nchi zisizo wanachama wa FIFA, Abdi Kassim ‘Babbi’, Abdulhalim Humud ‘Gaucho’, Abdulghani Gullam na Hamisi Mcha tayari wameripoti na wameendelea na mazoezi leo Chamazi.
Kiungo Salum Abubakar ‘Sure Boy Jr.’ aliyeumia kabla ya Stars kwenda Msumbiji, yeye anaendelea na programu maalum ya daktari wa timu hiyo na tayari ameripoti.
John Bocco 'Adenayor'
Tayari Azam, washindi wa pili wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara wamekwishamalisha usajili wa wachezaji wao hata kabla ya kwenda likizo.
Programu ya maandalizi ya Kombe la Kagame, inayoendelea hivi sasa itamalizika siku moja kabla ya kuanza mashindano hayo, Juni 28 na yatakapomalizika, wachezaji watapewa mapumziko ya siku chache kabla ya kuanza maandalizi kwa ajili ya msimu ujao wa Ligi Kuu.
Maandalizi kwa ajili ya VPL yatahusisha pia ziara ya nje ya nchi ya kujiandaa na msimu mpya, ingawa amesema nchi hiyo itatajwa baadaye.
Wachezaji wapya kikosini Azam msimu huu ni kiungo Mkenya George ‘Blackberry’ Odhiambo na kipa Deogratius Munishi kutoka Mtibwa Sugar, wakati Aishi Salum, Jackson Wandwi, Dizana, Ibrahim Rajab Jeba na Joseph Kimwaga, wamepandishwa kutoka akademi ya Azam.
Kikosi kamili cha Azam FC kinaundwa; na makipa, Mwadini Ally, Deo Munishi ‘Dida’ Aishi Salum na Jackson Wandwi, mabeki wa Ibrahim Shikanda, Erasto Nyoni, Waziri Salum, Samir Haji Nuhu, Luckson Kakolaki, Said Mourad, Joseph Owino na Aggrey Morris.
Viongo ni Kipre Bolou, Abdulhalim Humud, Himid Mao, Salum Abubakar, Abdi Kassim Sadalla, Ramadhani Suleiman Chombo, Abdulghani Ghullam, Ibrahim Rajab Jeba, Jabir Aziz Stima, Ibrahim Joel Mwaipopo, Kipre Tchetche, Mrisho Ngassa, Zahoro Pazi, Khamis Mcha na George Odhiambo ‘Blackberry’ wakati washambuliaji ni Gaudence Mwaikimba, John Bocco ‘Adebayor’.
Hii ni mara ya kwanza kwa Azam FC kucheza Kombe la Kagame, baada ya kushika nafasi ya pili katika msimu uliopita wa Ligi Kuu. Katika Kombe la Kagame mwaka huu, wenyeji Bara wataingiza timu tatu, Yanga ambao ni mabingwa watetezi, wakati Simba na Azam wanaingia kwa nafasi za uwakilishi.

MILOVAN AWASILI USIKU WA MANANE, KIKOSI SIMBA CHAREJEA DAR USIKU WA LEO


Milovan Cirkovick

Na Princess Asia
WAKATI Kocha Mkuu wa Simba SC, Milovan Cirkovick amewasili alfajiri ya leo kutoka kwa Srebia alipokuwa kwa mapumziko, kikosi cha mabingwa hao wa Ligi Kuu kinapanda ndege ya ATC saa1:00 usiku wa leo mjini Mwanza, kurejea Dar es Salaam kuungana na mwalimu hiyo kwa maandalizi ya Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati, Kombe la Kagame.
Ofisa Habari wa Simba SC, Ezekiel Kamwaga ‘Mr. Liverpool’ ameiambia BIN ZUBEIRY asubuhi hii kwa simu kutoka Mwanza kwamba timu ikifika itaendelea na mzoezi Uwanja wa TCC, Chang’ombe, Dar es Salaam chini ya Profesa Milovan, aliyetua kwa ndege ya shirika la ndege la Uturuki saa 8:45 usiku wa jana.
Simba, mabingwa mara sita wa Kombe la Kagame, 1975, 1991, 1992, 1995, 1996 na 2002, walikuwa Kanda ya Ziwa kwa ziara ya mechi mbili za kirafiki sambamba na kutambulisha Kombe lao la ubingwa wa Ligi Kuu kwa mashabiki wao wa huko.
Katika ziara yao hiyo, Simba ilicheza mechi ya mwisho jana Uwanja wa Kambarage Shinyanga na mabingwa wa Uganda, Express ‘Tai Mwekundu’ na kutoka sare ya 1-1, baada ya juzi, kuifunga Toto Africa Uwanja wa CCM Kirumba mabao 2-0.
Katika mchezo wa jana, kiungo mpya wa Simba SC, Kiggi Makassy aliifungia bao lake kwanza klabu hiyo, tangu ajiunge nayo mwezi huu kutoka kwa mahasimu, Yanga.
Hata hivyo, bao hilo la Kiggi lilidumu kwa dakika 20 tu, kwani dakika ya 40, Joseph Kaira aliwasawazishia Tai Wekundu na hadi kipyenga cha mwisho, timu hizo zilitoka 1-1.
Michuano ya Kombe la Kagame inatarajiwa kuanza Julai 14 hadi 29 mwaka huu, Tanzania ikiwakilishwa na timu tatu, mbali na Simba watakuwepo mabingwa watetezi wa michuano hiyo, Yanga SC na washindi wa pili wa Ligi Kuu, Azam FC.

PETER SHILTON: Aliyefungwa bao la ‘Mkono wa Mungu’ na Maradona


Shilton alivyo sasa

PETER Shilton ni mlinda mlango wa zamani wa timu ya taifa ya England aliyezaliwa Septemba 18, mwaka 1949 Mjini Leicester, England.
Anashikilia rekodi ya kucheza mechi nyingi katika timu ya taifa ya England, zaidi ya wachezaji wengine, amecheza jumla ya mechi 125.
Katika miaka 30 aliyocheza soka, ameweza kucheza klabu tofauti 11, pamoja na fainali tatu za Kombe la Dunia na michuano miwili ya Mataifa ya Ulaya na zaidi ya mechi 1,000 za michuano.
Shilton hakucheza fainali za Kombe la Dunia hadi alipofika umri wa miaka 32, lakini amecheza jumla ya mechi 17 na kuweka rekodi ya kutofungwa mechi 10 katika fainali hizo za Kombe la Dunia, rekodi ambayo pia imewekwa na mlinda mlango wa Ufaransa, Fabien Barthez.
Alipokuwa Nottingham Forest alishinda mataji mawili ya UEFA Super Cup, ubingwa Ligi Daraja la Kwanza na Kombe la Ligi na mataji mengine mengi.
Shilton alikuwa ni mwanafunzi wa umri wa miaka 13 katika shule ya King Richard III Boys School, iliyopo Leicester, wakati alipoanza kufanya mazoezi na klabu ya Leicester City mwaka 1963.
Mei mwaka 1966, akiwa na umri wa miaka 16, Shilton alianza kucheza kwa mara ya kwanza katika klabu ya Leicester dhidi ya Everton, kuanzia hapo alikuwa akipangwa kwenye kikosi cha kwanza cha timu hiyo.
Pamoja na kuwa na msimu mbaya wakiwa katika hatari ya kushuka daraja, lakini walifanikiwa kuingia fainali ya Kombe iliyochezwa Wembley, akiwa na umri wa mika 19. Shilton alikuwa ni mchezaji mdogo katika mechi hiyo, lakini walifungwa kwa bao 1-0 na Manchester City.
Timu yake ilishuka daraja, lakini aliamua kubaki nayo, pamoja na kucheza timu ya daraja la chini, lakini alimshawishi kocha wa timu ya taifa ya England wakati huo, Alf Ramsey, kumpa nafasi ambapo alicheza dhidi ya Ujerumani Mashariki Novemba mwaka 1970. England ilishinda mabao 3–1.
Baadaye aliisaidia Leicester kupanda daraja na kupata nafasi nyingine ya kuichezea timu ya taifa katika mchezo uliomalizika bila ya kufungana dhidi ya Wales katika Uwanja wa Wembley.
Na mechi yake ya tatu, huku ikiwa ni ya kwanza ya ushindani alicheza dhidi ya Uswisi, ambapo walitoka sare 1–1, katika mchezo wa kufuzu michuano ya Mataifa ya Ulaya.
Aliendelea kuichezea England mechi ya nne na ya tano, wakati huo Shilton akiwa mlinda mlango namba mbili na Oktoba mwaka 1972, mlinda mlango namba moja Gordon Banks, alipata ajali na kupoteza uwezo wa kuona na kukatiza soka lake, ambapo nafasi yake ilichukuliwa na Ray Clemence wa Liverpool.
Shilton aliondoka Leicester na kujiunga na Stoke City kwa ada ya pauni 325,000, wakati huo wakiendelea kugombea namba kwenye kikosi cha England na Clemence, ambaye alionekana kumzidi Shilton kwa kucheza mechi nane kati ya tisa.
Shilton alicheza mara moja tu mwaka 1975 kwenye kikosi cha England, hakucheza kabisa mwaka 1976 na 1977 alicheza mara mbili.
Msimu wa mwaka 1976 Manchester United walimtaka Shilton na Stoke walikubali kumtoa kwa pauni 275,000, lakini walishindwa juu ya mshahara alioutaka kipa huyo na kuamua kuachana naye.
Shilton enzi zake
Aliendelea kubaki kwenye kikosi hicho cha Stoke, ingawa kilishuka daraja mwaka 1977, Nottingham Forest walitoa ofa ya pauni 250,000 na Shilton alikubali kusaini msimu mpya na timu hiyo ya Forest kupanda daraja.
Walishinda Kombe la Ligi katika mchezo wa marudiano baada ya kutoka sare dhidi ya Liverpool, katika mchezo ambao Shilton alionyesha uwezo wake, akiokoa michomo na vichwa vya Mick Ferguson. Shilton alishinda tuzo ya mchezaji bora wa mwaka ya PFA, kocha mpya wa England, Ron Greenwood, alimchagua Shilton na kumuacha Clemence na mashabiki na wachambuzi wengi wa soka kukosoa jambo hilo.
Shilton, alisaidia England kwa ajili ya kufuzu michuano ya Mataifa ya Ulaya mwaka 1980 nchini Italia, ushindi dhidi ya Hispania, ulimfanya ashinde mechi 30.
Mlinda mlango huyo, aliwahi kushtakiwa kwa kosa la kuendesha gari akiwa amelewa na kupigwa faini ya pauni 350, huku tetesi za kutaka kuondoka Nottingham mwaka 1982, zilianza kuzagaa.
Shilton, aliondoka Forest na pamoja na kutakiwa na Arsenal, alikwenda kucheza Southampton na kukutana na wachezaji wenzake wa timu ya taifa kwenye klabu hiyo kama vile, Kevin Keegan, Alan Ball na Bobby Robson, aliivunja rekodi ya Bank kwa kucheza mechi 188, wakati mwenzake alicheza 73.
Wakati wa fainali za Kombe la Dunia mwaka 1986, England walianza taratibu kwa kupoteza mechi ya kwanza ya makundi dhidi ya Ureno, wakatoka sare na Morocco, wakati huo Robson akiwa majeruhi na Wilkins alipewa kadi nyekundu.
Kutokana na kukosekana kwao wote, Shilton alipata nafasi ya kucheza mechi na kuwa nahodha wa England na kuichapa Poland 3–0 kwenye mechi ya mwisho ya kundi lao, mabao yote yakifungwa na Gary Lineker.
Walikutana na Paraguay katika hatua iliyofuata na Shilton kufanya kazi kubwa ya kuokoa mipira ya hatari katika kipindi cha kwanza, England walishinda 3-0 mabao yakifungwa na Lineker mawili na moja Peter Beardsley.
Hatua ya robo fainali walikutana na Argentina, mechi iliyoonyesha uwezo wa Shilton katika kipindi chake chote cha soka.
Nahodha wa Argentina, Diego Maradona, alikuwa nyota wa michuano hiyo, lakini katika mchezo wao, England walimudu kumbana katika kipindi cha kwanza, kazi ilikuwa pale kipindi cha pili, Maradona alipobadili uchezaji wake na kumchanganya sana Shilton.
Maradona alianza kushambulia na kuingia kila wakati kwenye eneo la hatari England, beki wa England alifanya madudu na Maradona, akawahi mpira kwenye eneo la hatari, lakini Shilton aliokoa mpira uliopigwa na mshambuliaji huyo wakiwa wamebaki wawili.
Baadaye Maradona alitumia mbinu nyingine ya kumfunga mlinda mlango huyo baada ya kushindwa kufanya hivyo hapo mwanzo.
Ulipigwa mpira na Maradona akaruka na kuangalia ule mpira wakati Shilton akiunyemelea hewani, Maradona alinyoosha mkono wake na kuugonga mpira na ukaingia nyavuni.
Wachezaji wa England pamoja na mlinda mlango wao walilalamika kwamba Maradona ameshika, lakini mwamuzi kutoka Tunisia, Ali Bin Nasser, alikubali bao hilo.
Baadaye Maradona alipoulizwa alisema ni bao la mkono wa Mungu, na mwamuzi Nasser hakupewa nafasi nyingine tena ya kuchezesha michuano mikubwa kama hiyo.
Hivyo Shilton, aliepuka kukosolewa kutokana na vyombo vya habari vya England kuona tukio zima lilivyokuwa.
Lakini baadaye Maradona alifunga bao jingine la kawaida, baada ya kuwakusanya mabeki wote wa England pamoja na Shilton na kupasia nyavu zikiwa tupu. Lineker alifunga bao moja na kukaribia kusawazisha lakini bahati haikuwa yao, walitolewa katika hatua hiyo ya robo fainali.
Shilton aliendelea kuichezea England kwenye michuano ya Mataifa ya Ulaya mwaka 1988, iliyofanyika Ujerumani Mashariki.
Juni mwaka 1989, Shilton alivunja rekodi ya Bobby Moore, aliyecheza mechi 108, wakati yeye akicheza 109, alicheza mechi tatu bila kufungwa katika kampeni za kushiriki fainali ya Kombe la Dunia mwaka 1990 na wakafanikiwa kufuzu.
Baada ya kustaafu kuichezea timu ya Taifa mwaka mwaka 1991, alikataa kuwa kocha kuchukua nafasi ya Stan Ternent kwa ajili ya kuinoa Hull City.
Yeye na mkewe Sue, walioana mwaka 1970 na wana watoto wawili, Michael na Sam.
Sam anacheza soka katika nafasi ya kiungo, amecheza klabu kubwa mbalimbali kama Plymouth Argyle na Coventry City.
Desemba 18 mwaka 2011, ilitangazwa kwamba ametengana na mkewe baada ya kuishi wote miaka 40 ya ndoa yao.
WASIFU WAKE
JINA: Peter Leslie Shilton
KUZALIWA: Septemba18, 1949 (62)
ALIPOZALIWA: Leicester, England
UREFU: Futi 6 inchi 1
NAFASI: Mlinda mlango

TIMU ZA VIJANA
1963–1966 Leicester City

TIMU ZA WAKUBWA
1966–1974 Leicester City, (mechi 286, bao 1)
1974–1977 Stoke City, (mechi 110)
1977–1982 Nottingham Forest, (mechi 202)
1982–1987 Southampton, (mechi 188)
1987–1992 Derby County, (mechi 175)
1992–1995 Plymouth Argyle, (mechi 34)
1995 Wimbledon, (hakucheza)
1995 Bolton Wanderers, (mechi 1)
1995–1996 Coventry City, (hakucheza)
1996 West Ham United, (hakucheza)
1996–1997 Leyton Orient, (mechi 9)
Jumla amecheza mechi 1,005 na bao 1
(Tangu 1970 hadi 1990, aliichezea England mechi 125)
UKOCHA: 1992–1995 Plymouth Argyle

No comments: