Wednesday, June 13, 2012

BREAKING NEWS; AZAM WAJENGA MPYA WA KISASA KAMA TAIFA




Uwanja wa sasa wa Azam

KLABU ya Azam FC, imeanza ujenzi wa Uwanja mpya mkubwa na wa kisasa wenye hadhi sawa na Uwanja mpya wa Taifa wa Dar es Salaam, ambao ndio utakuwa ukitumika kwa mechi mbalimbali za timu hiyo, wakati Uwanja wa sasa utakuwa kwa ajili ya mazoezi tu.
Habari za ndani kutoka Azam zimesema kwamba tayari hatua za awali za ujenzi zimeanza katika eneo lile lile la Chamazi.
“Tunajenga Uwanja mwingine mkubwa, huo utakuwa kama Uwanja wa Taifa. Utakuwa unatumika kwa mechi zetu zote za kitaifa na kimataifa, huu Uwanja wa sasa utakuwa kwa ajili ya mazoezi tu na mechi za timu za vijana,”kilisema chanzo chetu kutoka Azam.
Azam FC wanaelekea kupiga hatua nyingine kubwa na kuzidi kuzipiga bao, timu kongwe nchini Simba na Yanga- kwani hadi sasa tayari hiyo ndio klabu pekee nchini yenye Uwanja wake wenye kukidhi vigezo.
Simba iliyoanzishwa zaidi ya miaka 70 iliyopita, bado haina Uwanja hata wa wachezaji wake japo kupigia danadana, wakati wapinzani wao wa jadi, timu kongwe zaidi nchini kwa sasa, Yanga ina Uwanja wa Kaunda, ambao umetelekezwa na upo katika hali isiyotazamika.
Ingawa historia inasema Yanga ilizaliwa mwaka 1935 na Simba mwaka 1936, lakini ukizama ndani utagundua kwamba, huo ndiyo ulikuwa mwanzo wa utani na upinzani wa jadi, baina ya miamba hiyo ya soka nchini.
Kulikuwa kuna timu inaitwa New Youngs, ambayo mwaka 1938 ilisambaratika na baadhi ya wachezaji wake wakaenda kuunda timu iliyokuwa ikiitwa Sunderland, ambayo hivi sasa inajulikana kama Simba.
Kabla ya kutokea vurugu zilizoisambaratisha New Youngs, vijana wa Dar es Salaam walikuwa wana desturi ya kukutana viwanja vya Jangwani kufanya mazoezi na baada ya muda wakaamua kuunda timu yao, waliyoipachika jina Jangwani.
Ndani ya kipindi kifupi tu, timu hiyo iliteka hisia za wengi, waliojitokeza kujiandikisha uanachama wa klabu hiyo. Miongoni mwa waliovutika na uanachama wa klabu hiyo ni Tarbu Mangara (sasa marehemu) na ilipofika mwaka 1926, walifanya mkutano wa kwanza katika eneo ambalo hivi kuna shule ya sekondari ya Tambaza.
Miongoni mwa yaliyojadiliwa kwenye mkutano huo ni kuiboresha timu hiyo, ambayo wachezaji wake wengi walikuwa wafanyakazi wa Bandarini na mashabiki wake wengi walikuwa wabeba mizigo wa bandarini.
Baada ya mkutano huo, timu hiyo ilibadilishwa jina na kuwa Navigation, iliyotokea kuwa moto wa kuotea mbali katika timu za Waafrika enzi hizo, kabla ya uhuru wa Tanganyika. Timu kama Kisutu, Kitumbini, Gerezani na Mtendeni zilikuwa hazifui dafu kwa wana Jangwani hao.
Ikiwa inatamba kwa jina la Navigation, wanachama wa timu hiyo walikuwa wakitembea kifua mbele na kuwatambia wapinzani, kwamba wao ndiyo zaidi. Kwa sababu katika kipindi hicho, Italia ilikuwa inatamba kwenye ulimwengu wa soka, wanachama wa timu hiyo nao waliamua kuibadilisha jina timu yao na kuiita Taliana.
Taliana ilipata mafanikio ya haraka na haikushangaza ilipopanda hadi Ligi Daraja la Pili Kanda ya Dar es Salaam, mwanzoni mwa miaka ya 1930. jina la Taliana waliamua kuachana nalo mapema, kabla ya kuingia kwenye ligi hiyo, hivyo wakaanza kujiita New Youngs.
Lakini kila ilipokuwa ikibadilisha jina, ilikuwa ikifanya vitu pia, kwani wakiwa na jina la New Youngs, waliweza kutwaa Kombe la Kassum, lililoshirikisha timu mbalimbali za Dar es Salaam.
Hatimaye ukawadia mwaka mbaya kwa New Youngs, 1938 wakati baadhi ya wachezaji walipojitoa na kwenda kuanzisha Sunderland. Kwa sababu hiyo, waliobaki wakaamua kubadili jina na kuwa Young Africans, jina ambalo mashabiki wake wengi walishindwa kulitamka vizuri hivyo kujikuta wakisema Yanga.
Azam FC, ilianzishwa mwaka 2004 tu na kikundi cha wafanyakazi wa kampuni ya Mzizima Flour Mill, kampuni tanzu ya Bakhresa, makao yake makuu yakiwa Barabara ya Nyerere, Dar es Salaam.
Lengo la wafanyakazi hao wa kampuni inayomilikiwa na Said Salim Bakhresa, awali ilikuwa ni kucheza kwa ajili ya kujiburudisha, baada ya kazi.
Lakini baada ya kuona wana timu nzuri, Oktoba 16, mwaka 2004, waliisajili rasmi kwa ajili ya kushiriki Ligi Daraja la Nne, wakitumia jina la Mzizima FC.
Baadaye Mkurugenzi Mkuu wa makampuni ya Bakhresa, Abubakar Bakhresa, aliona ni vyema timu hiyo ihusishe wafanyakazi wa kampuni zote za Bakhresa, na kutumia jina la moja ya bidhaa zao kubwa, Azam.
Kampuni nyingine za Bakhresa ni Food Products Ltd, Azam Bakeries Ltd, Omar Packaging Industries Ltd na kadhalika. Wazo lake lilikubaliwa na wafanyakazi wa kampuni hiyo, ndipo timu hiyo ikaanza kuitwa Azam SC, badala ya Mzizima. Lakini baadaye Juni 11, mwaka 2007, ilibadilishwa jina tena na kuwa Azam FC.
Azam ilikwenda kwa kasi nzuri kuanzia Daraja la Nne na hadi mwaka 2008, ilifanikiwa kucheza Ligi Kuu, na msimu uliopita pamoja na kutwaa Kombe la Mapinduzi mbele ya vigogo wa soka nchini Simba na Yanga, pia ilikaribia kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu- baada ya kuzidiwa na Simba waliobuka mabingwa, huku wao wakishika nafasi ya pili mbele ya waliokuwa mabingwa watetezi, Yanga.
Kwa mara ya kwanza, Azam mwakani itapeperusha bendera ya Tanzania kwenye michuano ya Afrika, ikicheza Kombe la Shirikisho

No comments: