Monday, June 18, 2012

13 WAHUDHURIA MAZOEZI SIMBA SC

 


WACHEZAJI 13 wameripoti kwenye mazoezi ya Simba SC jioni hii, wakiwemo Kiggi Makassy aliyesajiliwa kutoka kwa mahasimu, Yanga ingawa mshambuliaji aliyesajiliwa kutoka Dong Tam Long An ya Vietnam, Danny Davis Mrwanda hakutokea.
Mashabiki wengi wa Simba walifika mapema Uwanja wa TCC Chang’ombe, Dar es Salaam jioni hii kuwashuhudia wachezaji wao, kiu zaidi ikiwa kumuona mpachika mabao wao wa zamani, aliyerejea kikosini Mrwanda, lakini Meneja wa Simba, Nico Nyagawa akaiambia BIN ZUBEIRY kwamba mchezaji huyo ni miongoni mwa waliotoa udhuru.
Waliohudhuria ni pamoja na Salim Kinje, Abdalllah Juma, William Mweta, Hamadi Waziri, Abuu Hashim, Haroun Athumani, Haruna Shamte, Amri Kiemba, Paul Ngalema, Uhuru Suleiman, Patrick Kanu Mbivayanga na Abdallah Seseme.
Mazoezi hayo yaliongozwa na Kocha wa Mazoezi ya Viungo, Mganda Hamatre Richard kwa sababu Kocha Mkuu, Mserbia Milovan Cirkovick bado anakula sikukuu kwao.
Simba itaendelea na program ya mazoezi kwa jioni tu wiki hii na Nyagawa amesema anatarajia idadi ya wachezaji itakuwa ikiongezeka taratibu wiki hii, wakiwemo wachezaji waliokuwa na timu ya taifa Msumbiji nao pia wanatarajiwa kuungana na wenzao wakirejea kutoka nchini humo.
Mrwanda ambaye amesaini mkataba wa mwaka mmoja wa kuichezea Simba, ambao hauna kipengele cha kumruhusu kuuvunja kabla haujamalizika naye anatarajiwa kuanza maozezi wakati wowote wiki hii.
Mrwanda, awali ilielezwa anataka kusaini mkataba ambao wakati wowote akipata timu nje, aondoke, lakini kwa mujibu wa mkataba aliosaini Simba ni kwamba akipata timu italazimika kumnunua kutoka kwa Wekundu wa Msimbazi, au isubiri hadi amalize mkataba.
Habari za uhakika, kutoka ndani ya Simba SC ambazo BIN ZUBEIRY imezipata, zimesema kwamba Mrwanda ameridhika na mkataba huo na ameahidi kufanya vitu baab kubwa Msimbazi.
Kwa upande mwingine, Simba SC imeamua kumtema kiungo Salum Machaku kwa makubaliano maalum ya pande zote mbili ya kuvunja mkataba. Simba ilitaka kumtoa kwa mkopo Machaku, lakini mwenyewe akasema bora aachwe moja kwa moja.
Tayari Simba imemsajili kiungo wa Yanga, Kiggi Makassy kuziba nafasi ya Machaku. Machaku sasa ameingia kwenye mazungumzo na Yanga.
Simba SC inajiandaa na michuano ya Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati, Kombe la Kagame inayotarajiwa kuanza Julai 14 hadi 29, mwaka huu mjini Dar es Salaam. Timu nyingine za Tanzania zitakazoshiriki michuano hiyo ni mabingwa watetezi, Yanga na washindi wa pili wa Ligi Kuu Azam FC.
Azam pia wameshaanza kujifua kwenye Uwanja wao wa Chamazi, wakati Yanga wanatarajiwa kuanza kesho Uwanja wao wa Kaunda, Jangwani, Dar es Salaam.
Kocha wa makipa, James Kisaka akiwanoa makipa wa timu hiyo, William Mweka anayemuelekeza na kulia ni kipa aliyepandishwa kutoka timu ya vijana Abuu Hashim wakati kulia Hamadi Waziri aliyesajiliwa kutoka JKT Oljoro

Uhuru kushoto anamtoka mtu

Kiggi baada ya kufumua shuti, kushoto kwake Hamatre

Wanatafuta upepo

Wananyoosha misuli

Kutoka kulia Kiggi Makassy, Amri Kiemba na Abdallah Juma

Kutoka kulia, Abdallah Juma, Haruna Shamte na Paul Ngalema

Baada ya mazoezi

Mazoezi yameisha
 

MAZOEZI SIMBA YAANZA KUCHANGANYA TCC CHANG'OMBE

Wachezaji wa Simba SC wakifanya mazoezi kwenye Uwanja wa TCC Chang'ombe Dar es Salaam jioni hii.Wa kwanza kabisa kushoto ni Kiggi Makasy na kulia kabisa ni Salim Kinje, ambao wamekuwa kivutio kwenye mazoezi hayo yanayoongozwa na Kocha wa mazoezi ya viungo, Mganda Hamatre Richard

Kocha wa Mazoezi ya Viungo wa Simba, Hamatre Richard (katikati) akiongoza mazoezi ya Simba jioni hii Uwanja wa TCC Chang'ombe, Dar es Salaam. Kulia kabisa ni mpachika mabao mpya wa timu hiyo, Abdallah Juma kutoka Ruvu Shooting

No comments: