Wednesday, October 5, 2016

Wakulima wa korosho Nanyumbu wapinga malipo kwa njia ya Benki.




Wazee wa vijiji vya Sengenya na Matimbeni, halmashauri ya wilaya ya Nanyumbu mkoani Mtwara, wakiwa katika mkutano wa hadhara kujadili masuala mbalimbali juu ya zao la korosho.


Juma Mohamed, Mtwara

Baadhi ya wakulima wa zao la korosho wa vijiji vya Sengenya na Matimbeni halmashauri ya wilaya ya Nanyumbu mkoani Mtwara wameonesha kutounga mkono agizo la serikali linalotaka malipo ya zao hilo yafanyike kupitia benki.
Wakizungumza katika mkutano wa hadhara katika kijiji cha Sengenya, walidai kuwa agizo hilo linawafaa wakulima wanaokusanya kiasi kikubwa cha korosho ambao fedha zao zinapaswa kulipwa kwa njia ya benki tofauti na wale wanaokusanya kiasi kidogo.
Diwani wa kata ya Sengenya, Fatma Chisanga, alishauri wanaopaswa kulipwa kwa njia ya benki ni wale wanaokusanya zaidi ya kilo 500 na kutoa tahadhari kwamba suala hilo linaweza kupelekea wakulima wadogo kushawishika kuuza kwa wanunuzi holela maarufu Kangomba.
"Mimi uchumi wangu unaishia kupata debe moja, debe moja hili nikiuza napata sh. 5,000..alafu nikafungue akaunti benki, napanda pikipiki kufika kule mpaka kurudi hapa hela ya dagaa yote imeisha debe moja ile.." alisema Chamila Mrekoni.
Afisa mtendaji wa kijiji hicho, Athuman Makochela, aliwaonya wakulima kutothubutu kuuza kwa wanunuzi wa Kangomba na kwamba watakaofanya hivyo serikali haitosita kuwachukulia hatua.

Baadhi ya wananchi wa vijiji vya Sengenya na Matimbeni, halmashauri ya wilaya ya Nanyumbu mkoani Mtwara wakiwa katika mkutano wa hadhara kueleza masuala mbalimbali juu ya zao la korosho.



Msimu mpya wa korosho ulizinduliwa Septemba Mosi mwaka huu katika mkutano mkuu wa wadau wa tasnia ya korosho uliofanyika wilayani Bagamoyo mkoani Pwani na kupanga bei dira kuwa ni shilingi 1,300.

No comments: