Baadhi ya wanakikundi cha Jipange Cashewnut cha mjini Mtwara wakiwa katika shughuli yao ya uuzaji wa korosho. |
Na Juma Mohamed, Mtwara
Wabanguaji
wadogo wa korosho wa kikundi cha kina mama cha Jipange Cashewnut Group mkoani
Mtwara wako hatarini kusitisha shughuli hiyo inayowaingizia kipato kutokana na
serikali mkoani humo kupiga marufuku ununuzi holela wa zao hilo maarufu
Kangomba.
Wakizungumza
na Juma News, walidai kuwa korosho
wanazobangua sasa na kuziuza walizinunua msimu uliopita kwa njia ya Kangomba,
lakini kutokana na marufuku ya serikali, na kutokuwa na uwezo wa kwenda
minadani kushindana na wanunuzi wakubwa, hawajui watumie njia gani ili wapate
korosho msimu huu.
“Yani sasa
hivi Kangomba wamepiga marufuku je, sisi serikali inatusaidiaje?..na tusipofanya
hivyo sisi mitaji tutapata wapi wenye biashara ndogondogo, maana sisi wengine
tuna mitaji midogo hatuna mitaji mikubwa..sisi tunachoomba serikali itusaidie
sisi wenye mitaji midogo.” Alisema Zuhura Mfaume.
Bodi ya
Korosho Tanzania CBT kupitia kwa makamu mwenyekiti wake Mudhihiri Mudhihiri,
ilieendelea kusisitiza kukomeshwa kwa ununuzi wa Kangomba na kwamba yeyote
atakayekutwa ananunua kwa njia hiyo akamatwe na kuchukuliwa hatua za kisheria.
Aidha,
Mudhihiri alisema Bodi itawasaidia wabanguaji wadogo na tayari wapo katika
hatua nzuri ya kuwasajili ili iwe rahisi kuwasaidia kupitia chama chao sambamba
na kuwapatia elimu mbalimbali juu ya ubanguaji.
Makamu mwenyekiti wa Bodi ya Korosho Tanzania CBT-Mudhihiri Mudhihiri |
“Kwahiyo
sisi tumeamua kwenda kwa wabanguaji wadogo hao kuwasaidia shida zao lakini
tuliona tukienda kwa mojamoja tutakuwa tunatumbukiza hela mtoni, ndiomana
tunawasajili wawe na umoja wao tuweze kutoa elimu kwa urahisi na kuweza
kuwafikia kwa misaada kwa urahisi..” alisema Mudhihiri.
Bodi hiyo
imetangaza rasmi kuanza kwa minada ya ununuzi wa korosho ambapo kwa mkoa wa Mtwara
mnada wa kwanza umefanyika leo Oktoba 14 wilaya za Masasi na Newala, huku jumla
ya kampuni 66 zikiwa zimepata leseni za ununuzi ikiwa ni sawa na ongezeko la
asilimia 22 kutoka kampuni 54 za msimu uliopita.
No comments:
Post a Comment