Wednesday, July 22, 2015

Chadema Mtwara mjini washindwa kumpata mbunge..mkutano wavurugika..viongozi wapigwa 'stop'



Wajumbe wa mkutano wa uchaguzi wa wagombea ubunge wa Chadema wakiwa nje ya ukumbi baada ya zoezi la uchaguzi kuvurugika na kuahirishwa.






Wagombea ubunge wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kwa jimbo la Mtwara mjini, wakwanza kushoto ni Mohamed Hassan Hanga akifuatiwa na Ibrahim Mandoa, Joel Nanauka na mwakilishi wa Mlokozi ambae ni mke wake.




Mwenyekiti wa mkutano wa uchaguzi wa wagombea ubunge jimbo la Mtwara mjini, Kasto Mmuni akifafanua jambo kuhusu utata ulijitokeza katika mkutano huo



Wajumbe wa mkutano wa uchaguzi wa wagombea ubunge wa Chadema mtwara mjini wakiwa ndani ya ukumbi kwa ajili ya kufanya uchaguzi.

Na Juma Mohamed, Mtwara.



CHAMA cha Dekrasia na Maendeleo (CHADEMA) wilaya ya Mtwra kimeshindwa kupata wagombea ubunge katika jimbo la Mtwara mjini na wa viti maalum kutokana na kuvurugika kwa mkutano baada ya kutokea  mkanganyiko juu ya idadi ya kata zilizofanya uchaguzi na kuwa na uhalali wa kupiga kura za kuchaguwa wagombea.

Wagombea waliokuwa wanachuana ili apatikane mmoja wa kuwania ubunge katika jimbo hilo walikuwa wane ambao ni Joel Nanauka, Mohamed Hassan Hanga, Ibrahim Mandoa na Dastani Mulokozi ambaye hakuwepo mkutanoni na kuwakishwa na mke wake.

Hatua hiyo ilitokana na hoja iliyotolewa na mjumbe wa mkutano huo ambaye ni mwenyekiti wa mawasiliano, takwimu na Biometric Voters Registration (BVR), Karim Salum Ally, ambaye alihoji utofauti wa idadi ya kata hizo kwamba taarifa alizokuwanazo yeye ni kata 15 huku zile za katibu wa Chadema mkoa Willy Mkapa zilisema ni kata 17.

Alisema taarifa za kujaza nafasi ambazo zilikuwa wazi kwa kuto pata viongozi katika uchaguzi uliopita wa serikali za mitaa ambazo zilifanya uchaguzi baadae, yeye ndiye alisaini na kwamba zilikuwa ni kata 15 na sio zaidi ya hapo.
“Taarifa ya kujaza mapengo ilivyokuja nimeijaza mimi, nilivyoijaza nimejaza kata 15 na mitaa yake..nikamkabidhi katibu wa sheria na haki za binadamu, yeye ndiye aliyenipa nikamuambia azipeleke..sasa kama taarifa zinafika makao makuu na mimi ndiye niliyoijaza alafu leo naongopwa hapa basi ni shida, kuna kila sababu ya kujitofautisha sisi na ccm (Chama Cha Mapinduzi)..alisema Karim.

Kata ambazo zinatajwa kuwa taarifa zake hazikufika kwa viongozi wa mkoa baada ya kukamilika kwa oparesheni jaza mapengo ambayo ndio ilikuwa ya kukamilisha kata zilizokuwa zimesalia zilikuwa ni kata ya Vigaeni na kata ya Tandika.

Naye mwenyekiti wa wilaya ya Mtwara mjini ambaye pia ni mgombea ubunge katika jimbo hilo, Ibrahim Mandoa, alisema tatizo lililojitokeza ni kutokana na uongozi wa wilaya kuwapa haki sawa wagombea ili wakazungumze na wanachama wao ambapo wagombea wengine walipewa taarifa za kata 15 na wengine kata 17.
Mandoa alionekana kuishutumu kamati ya wilaya ambayo iko chini yake akilaumu zaidi kitendo cha katibu na katibu mwenezi kushindwa kuwapa taarifa sawa wagombea.

“Siku ya tarehe 21, kulikuwa na kikao lakini hakikumalizika vizuri kwasababu katibu mwenezi ana taarifa ya kata 17 lakini kuna baadhi ya wagombea hawana hizo taarifa..hapo ndipo penye mkanganyiko, kama tunataka jawabu la humu humu ndani tukubaliane hapo..” alisema.
Katibu mwenezi wa wilaya, Hamisi Bakari, alisema kuwa kata zote yeye ndiye alizisimamia na anatambuwa idadi ya kata 17 ikiwa ni pamoja na Tandika na Vigaeni ambazo ndizo zinazolalamikiwa, na kwamba baada ya kukamilika kwa uchaguzi katika kata hizo taarifa alizifikisha kwa katibu wa mkoa.

Alisema utata uliojitokeza ni kutokana na baadhi ya viongozi kuwa na lengo la kutaka kuuvuruga uchaguzi, huku akimshutumu mwenyekiti wake Ibrahim Mandoa kuwa na dhamira ya kukivuruga chama na kwamba aliwahi kuandika barua ya kulalamikia matumizi mabaya ya madaraka yanayofanywa na mwenyekiti huyo.

Baada ya mvutano wa muda mrefu baina ya wajumbe wanaounga mkono upande wa mwenyekiti wa wilaya na wafuasi wake ikiwa ni pamoja na wagomea ubunge wawili ambao ni Mohamed Hassan Hanga na Dastan Mlokozi ambaye aliwakilishwa, na wanaounga mkono idadi ya kata 17 ambayo pia inaungwa mkono na mgombea mmoja Joel Nanauka, ndipo mwenyekiti wa mkutano huo Kasto Mmuni akaamua kuhoji wagombea wanaoridhia kata mbili zinazolalamikiwa zisishiriki mchakato huo au zisishiriki.
Wagombea watatu ambao ni Ibrahim Mandoa, Mohamed Hassan Hanga na mwakilishi wa Dastan Mlokozi walisema zisishiriki kwa kuwa wao hawakufika kwenda kujinadi huku Joel Nanauka akitaka zishiriki kwakuwa alikwenda kujinadi na anaimani zinawapiga kura wake wengi, hivyo zikiondolewa idadi ya kura itapungua.
Kutokana na kupishana kwa wagombea hao licha ya baadae Nanauka kukubali ziondolewe, mwenyekiti aliamuru kuahirisha zoezi la uchaguzi huo na kusema kwamba ataandika ripoti ya kilichotokea na kuituma makao makuu ili kamati kuu iamue kama kurudia uchaguzi au kuteuwa mgombea wanaomtaka wao ili agombee jimbo la Mtwara mjini.
Hali ilivyokuwa nje ya ukumbi
Baada ya wajumbe kutoka ndani ya ukumbi wengi wao walionekana kuwa na jaziba kiasi cha kuzungumza lugha za kukata tama na uwezekano wa Chadema kulipokonya jimbo hilo kutoka CCM, kutokana na kutumia muda mwingi bila ya kufikia lengo ambalo lilikuwa ni kumpata mgombea wa jimbo la Mtwara mjini na wale wa viti maalum ambao majina yao yangepelekwa katika ngazi za juu pamoja na Ukawa kwa ajili ya kuchagua nani anafaa kugombea katika jimbo hilo.
Nanauka atoa chozi
Joel Nanauka ambaye alionekana kuwa na wafuasi wengi wanaomuunga mkono miongoni mwa wajumbe wa mkutano huo, alitoka ndani ya ukumbi akiwa anatoa machozi kutokana na kusikitishwa na hoja zilizotolewa na baadhi ya viongozi wa wilaya na kuungwa mkono na wagombea wengine, jambo ambalo lilionekana kama amependelewa kwa kupewa taarifa za kata 17.
“Kwanza niseme mimi nasikitika sana, kwasababu wanachama ndio waamuzi..na ndio maana ikafika hatua nikasema kama tatizo ni kata mbili ambazo wanahisi mimi naungwa mkono basi tuendelee na uchaguzi..lakini imenisikitisha sana..” alizungumza Nanauka kwa ufupi sana na kuamua kuingia ndani ya gari yake na kuondoka.
Mohamed Hassan Hanga
Alionekana kuushutumu uongozi wa wilaya ambao kwa kuto tenda haki katika kutoa taarifa kwa wagombea juu ya uhalali wa kata mbili ambapo alisema hata aliyeweka uongozi hajulikani na hivyo kuonekana kutoa upendeleo kwa mgombea mmoja ambaye alizifikia kwenda kujinadi.
“Na wenyewe wamekiri kwamba hizo kata mbili hata aliyetoa uongozi hajulikani..na katika hizo kaonyeshwa mgombea mmoja tu ambaye alikwenda kujinadi na mwenyewe amesema kuwa ana mtaji mkubwa kwenye kata hizo mbili za Vigaeni na Tandika..kwahiyo sisi ambao hatujaenda tuna mtaji sifuri..” alisema.
Aliongeza kuwa “viongozi wa wilaya yani katibu mwenezi na katibu, hawafai na waondoke na nimesema mbele yao..inawezekana na Mandoa (Mwenyekiti wa wilaya) ana mambo yake lakini mvutano mkubwa ni kwa wagombea wawili Mandoa na Joel sio sisi..” aliongeza.
NEWS ROOM ilimtafuta mwenyekiti wa wilaya Ibrahim Mandoa lakini hakuweza kupatikana kuweza kutolea ufafanuzi juu ya shutuma zinazoelekezwa katika uongozi wake.
Viongozi wa wilaya wasimamishwa kwa miaka mitano
Uongozi wa kanda ulichukuwa hatua ya kuwapa barua za kuwasimamisha kujihusisha na shughuli za chama kwa muda wa miaka mitano viongozi watatu wa wilaya ambao ni Ibrahim Mandoa (mwenyekiti), Hamis Bakari (katibu mwenezi) na Stanslaus Sumi (katibu).
Akizungumzia maamuzi hayo, kiongozi wa Chadema kanda ya kusini, Abdallah Binnyaru, alisema viongozi hao wote ndio chanzo cha matatizo yote yaliyojitokeza na kwamba waliweza kufahamu mapungufu yao kupitia kikao cha kamati ya utendaji ambacho walikaa siku moja kabla ya mkutano huo.
“Tukaona ni bora sasa sheria ichukuwe mkondo wake baadala ya kukiona chama kinaingia porini..na ndio maana tukawapa barua, na tulishindwa kuwakabidhi mapema kwasababu tulitaka wote watimie.” Alisema.

Kwa upande wake, katibu wa Chadema mkoa, Willy Mkapa alisema hali hiyo ilijitokeza ni kuonesha ni jinsi gani chama hicho kimekomaa kidemokrasia na kwamba haiwezi kuathiri chama kwa nanmna yoyote kwasababu bado wanachama wanaimani na chama chao na wanakipenda.
Alisema maamuzi yaliyofanywa ya kutokubaliana na upande wowote na kuamua kuahirisha mkutano ni maamuzi ya busara zaidi kwasababu imesaidia kuhepusha mvutano baia ya pande hizo.
Mwenyekiti wa wagombea kanda ya kusini ambaye ndio alikuwa mwenyekiti wa mkutano huo, Kasto Mmuni, alisema sababu iliyopelekea kuvunjwa kwa mkutano huo ni kutokana na wagombea wenyewe hawakuwa tayari uchaguzi uendelee kutokana na watatu miongoni mwao hawakuwa na taarifa ya kata mbili zilizoongezwa huku mgombea mmoja ndio mwenye taarifa.
“Kwa namna moja au nyingine ilikuwa ni ngumu kuendelea na shughuli za uchaguzi kwasababu hizi kata mbili zilikuwa ni msingi mkubwa kwa huyu mgombea mmoja, kwahiyo ukiziondoa utakuwa hujamtendea haki..na ndio maana nikawahoji wote wane kujua kama wako tayari ziondolewe zile kata mbili ili uchaguzi uendelee..wagombea watatu walikubali lakini mmoja akasema hapana.” Alisema Mmuni.

Alisema baada ya kuona hakuna usawa baina yao licha ya kwamba baadae Yule mgombea mmoja ambaye ni Joel Nanauka kukubali ziondolewe ili uchaguzi uendelee, aliamua kuahirisha mkutano mpaka utakapoitishwa tena pamoja na kwamba mwisho wa mchakato huo wa kuchagua wagombea ni Julai 25 mwaka huu.

…………………………………………..mwisho……………………………………………………..

 

No comments: