Na Juma Mohamed, Mtwara.
Adha ya
uhaba wa maji safi na salama ni moja ya changamoto kubwa wanayokabiliana nayo wananchi
wa kijiji cha Hiayari, halmashauri ya wilaya ya Mtwara hali ambayo inawalazimu
kununua Ndoo moja kwa shilingi Miatano.
Wakizungumza
na Juma News kijijini hapo, wananchi hao
wameiomba serikali kufanya jitihada za dhati kutatua tatizo hilo ambalo
linawafanya washindwe kuoga na kufanya shughuli zingine zinazo hitaji huduma
hiyo.
“Hapa sisi
tuna shida ya maji ndoo moja sh. 500, tunashindwa kuoga na unaweza ukakaa kutwa
maji hayajaletwa, maji tunanunua kwenye maboza kwahiyo unaweza ukakaa mpaka
yaje maboza ndio tupate maji..” alisema Mariam Hemed.
Naye, Matonya
Peater, alionesha kushangazwa na kijiji hicho kukosa maji wakati kuna kiwanda
kikubwa cha Saruji cha Dangote Industries Limited jambo ambalo lingesaidia
kuondoa kero mbalimbali za kijamii kwa wananchi wake.
Miongoni mwa wazee wanaokabiliwa na uhaba wa maji katika kijiji cha Hiyari. |
Mwenyekiti
wa kijiji hicho, Mohamed Namkopa amesema kuwa tatizo hilo linatokana na
uchakavu wa mitambo ya mradi wa Maji wa Mbuo-Mkunwa ambao awali ulikuwa
unahudumia vijiji vichache kabla ya kufikia kutoa huduma kwenye vijiji 14.
“Sasa hivi
kuna changamoto ambazo zipo, changamoto ya kwanza ni huu mradi wa muda mrefu, una
muda mrefu haujafanyiwa matengenezo..changamoto ya pili ni ongezeko la watu
wapo wengi..” alisema Namkopa.
Naye afisa habari wa halmashauri ya wilaya
hiyo Isack Bilali alisema kuwa halmashauri imeshatambua changamoto hiyo na
kwamba bado inaendelea na mikakati ya kutatua tatizo hilo.
“Sisi kama
halmashauri tumeliona hilo na katika mipango yetu tunaendelea kuhakikisha
tunaimarisha upatikanaji huo wa maji na unaendelea kuwa bora kama ilivyokuwa
zamani.” Alisema.
Kijiji hicho
kimezunguka kiwanda cha Saruji cha Dangote Industries Limited ambacho kuwapo
kwake kimetoa matumaini makubwa kwa wananchi juu ya kupata ajira pamoja na
kuondokana na kero mbalimbali za huduma za kijamii.
No comments:
Post a Comment