Friday, May 6, 2016

Wananchi Mtwara watakiwa kutoa taarifa za viashiria vya rushwa Dangote.


Mkurugenzi wa kampuni ya uajiri katika kiwanda cha Saruji cha Dangote, ya Unique Consultant Company Ltd, Maulid Haule, akiongea katika kikao cha pamoja kati ya wenyeviti wa vijiji jirani na kiwanda hicho na viongozi wa kiwanda.


Mwenyekiti wa kijiji cha Naumbu Kusini, Rashid Abdelleman akiongea jambo katika kikao cha pamoja kati ya wenyeviti wa vijiji vya jirani na kiwanda cha Dangote na viongozi wa kiwanda hicho.



Na Juma Mohamed, Mtwara.

WANANCHI na viongozi wa vijiji vinavyozunguka kiwanda cha Saruji cha Dangote Industries Ltd mkoani hapa wametakiwa kutoa taarifa za vitendo na viashiria vya rushwa kwa mamlaka husika, iwapo itabainika kujitokeza katika michakato ya utoaji wa ajira kiwandani hapo.
Hayo yamezungumzwa na mkurugenzi wa kampuni ya uajiri katika kiwanda hicho ya Unique Consultant Company Ltd, Maulid Haule, wakati akijibu hoja za wenyeviti wa vijiji hivyo kufuatia malalamiko yao juu ya tuhuma za rushwa wakati wa utoaji wa ajira.
Alisema, alisema kama kutakuwa na uthibitisho juu ya kuwapo kwa watu ambao wameingia kazini kwa kutoa pesa, vipo vyombo vya kupeleka malalamiko ili wachukuliwe hatua za kisheria kwani kufanya hivyo ni kinyume na taratibu za kazi.
“Suala la kutoa pesa ni mwiko..mwiko kwa maana ya kikatiba, kwa sheria zetu za nchi na mwiko kwenye taratibu zetu hizi za uajiri kama kampuni, hiyo ni sehemu yoyote ya kazi ipo wazi anayetoa na anayepokea sheria imekataza kwa uwazi kabisa na uzuri wa siku hizi mambo yote yapo wazi..” alisema.
Aidha, aliwataka wananchi wawe wawazi iwapo baadhi yao watashindwa katika usaili kutokana na kutokidhi vigezo au kufeli katika mitihani ya majaribio ili kuhepusha kuupotosha umma na kuuaminisha kuwa wananchi wa Mtwara wanabaguliwa.
Naye, kaimu kamanda wa Polisi mkoa wa Mtwara, Mrakibu Mwandamizi wa Polisi, George Salala, aliwataka viongozi wa kiwanda hicho na kampuni ya uajiri kutekeleza makubaliano yao na wananchi ili kuhepuka kutokea kwa migogoro na mivutano itakayoyumbisha maendeleo ya kiwanda na wananchi kwa ujumla.

Kaimu Kamanda wa Polisi mkoa wa Mtwara, Mrakibu Mwandamizi wa Polisi, George Salala, akiongea katika kikao cha viongozi wa kiwanda cha Dangote na wenyeviti wa vijiji vya jirani na kiwanda hicho.


“Tutengeneze mazingira ya uwazi kila wakati, kama tunataka twende sawasawa uwazi iwe ni sehemu ya utendaji, konakona inajenga hisia mbaya hawa hapa wenyeviti leo tunaona ni wachache, tunaona wanaonung’unika ni wachache lakini wanaonung’unika ni wengi..” alisema.
Mwakilishi mkazi wa kampuni ya Dangote, Esther Baruti, aliwashukuru viongozi wa vijiji hivyo kwa kutoa kero zao ambazo alisema amezipokea na kuahidi kuzifanyia kazi na kuongeza kuwa kutakuwa na utaratibu wa kukutana nao kila tarehe Tatu ya kila mwezi kwa ajili ya kujadili maendeleo.

Mwakilishi Mkazi wa kiwanda cha Saruji cha Dangote Industries Ltd, Esther Baruti.


“Nitawasilisha maombi yenu kwa Mhe. Alhaj Dangote kuhusu ahadi zake alizowaahidi zitekelezwe awamu kwa awamu..kwahiyo mimi naomba ushirikiano wenu kwasababu bila nyinyi hiki kiwanda kisinge simama..kwahiyo naomba musamemehe yote yaliyotokea na tufungue ukurasa mpya..” alisema Esther.



No comments: