Sunday, May 8, 2016

Ndanda Fc waahidiwa Milioni 15 za usajili.

Mohamed Kiluwa wakwanza kushoto akikabidhiwa jezi ya Ndanda Fc na mashabiki wa timu hiyo baada ya kumtembelea nyumbani kwake, Mikocheni jijini Dar es Salaam.


Mohamed Kiluwa, akieleza jambo mbele ya mashabiki wa Ndanda Fc



Mohamed Kiluwa, akipeana mikono na meneja wa Ndanda Fc, Martin Mwesiga






Mashabiki wa Ndanda Fc wakiporomosha burudani ya Ngoma nyumbani kwa mdau wa timu hiyo Mohamed Kiluwa.


Burudani



Na Juma Mohamed, Mtwara.

MFANYABIASHARA na mmiliki wa Kiwanda cha Chuma cha Kiluwa Still, Mohamed Kiluwa, ameahidi kutoa fedha kiasi cha sh. Milioni 15 kuipatia timu ya Ndanda Fc ya mkoani hapa kwa ajili ya kusaidia katika usajili wa wachezaji kwa maandalizi ya msimu mpya wa Ligi.
Akizungumza na Nipashe nyumbani kwake jijini Dar es Salaam baada ya kutembelewa na mashabiki wa timu hiyo, Kiluwa alisema atatoa fedha wiki ijayo ambazo zitasaidia kuwasajili wachezaji huku akiahidi kuendelea kuisaidia timu hiyo ambayo mpaka sasa bado inahaha kutafuta wadhamini.
Alisema, timu ya Ndanda inatoka mkoani Mtwara ambako yeye ndio nyumbani kwake, hivyo haoni sababu ya kushindwa kuisaidia kwani hata yeye anaguswa inapotokea timu inalalamika kuwa na hali ngumu ya kifedha kwasababu ni mwanamichezo mwenye kupenda maendeleo.

Mohamed Kiluwa akipeana mikono na mmoja wa mashabiki wa Ndanda Fc, kushoto ni msemaji wa mashabiki hao, Hamisi Chichi.


“Nadhani hilo halina tatizo kwasababu wameamua kuja kwangu na wameamua kunishirikisha na mimi nitashiriki labda walichoniambia kingine wanahitaji Milioni 15 kwa kusajili wachezaji, nimewaambia hilo halina tatizo nitawapatia vilevile..na sio kwenye hilo tu hata kwenye jambo lingine la aina yoyote kwasababu mimi mwenyewe ni mwanamichezo..” alisema Kilua ambaye pia ni mlezi kikundi cha wasanii wa muziki wa kizazi kipya cha Makomando.
Alisema, suala lolote wanalohitaji msaada wanatakiwa kueleza ili kwa pamoja waangalie namna ya kulitatua huku akidai kuwa timu hiyo kupitia viongozi wao walichelewa kumfuata na kumshirikisha katika utatuzi wa changamoto za kifedha wanazokabiliana nazo.
Mbali na ahadi hiyo ya fedha za usajili, aliwakabidhi mashabiki wa timu hiyo ambao walimtembelea nyumbani kwake wakiwa safarini kwenda Mlandizi mkoani Pwani kuishangilia timu yao ilikabiliana na JKT Ruvu katika mchezo wa ligi kuu, kiasi cha sh. Milioni 3.2 kwa ajili ya kuwawezesha katika safari yao ya kwenda jijini Mbeaya kuishangilia Ndanda itakapochuana na Mbeya City. 

Mwenyekiti wa Umoja wa mashabiki wa Ndanda, Karimu Achiso akibadilishana namba za simu na Mohamed Kiluwa


Kwa upande wake, mwenyekiti wa umoja wa mashabiki hao, Karimu Achiso, alisema licha ya kukabidhiwa Milioni 3 kwa ajili ya safari pia walipatiwa sh. Milioni 1 kwa ajili ya kujikimu watapouwa safarini.
Alisema, kupatikana kwa sh. Milioni 15 ambazo zimeahidiwa kutolewa wiki ijayo kwa viongozi wa timu ni mchango wa mashabiki kwa timu yao kwasababu walitumia nafasi ya kukutana naye kumuomba mchango huo wa safari ya Mbeya, kuiombea timu fedha za usajili hasa kwa wachezaji ambao wengi wao mikataba yao inamalizika baada ya msimu kumalizika.
“Tumesababisha kuiombea timu Milioni 15 ambazo ameahidi atatoa..ni mchango mkubwa kupitia mashabiki waliopitia nyumbani kwake na kuahidi kiasi kama hicho kinaweza kupatikana..lakini pia kwa mashabiki baada ya kupata Milioni 3 kutoka kwa Kiluwa na wao wametoa 500,000 kuipa timu..” alisema Achiso.
Mchezo wa JKT Ruvu na Ndanda ambao ulichezwa uwanja wa Mabatini mkoani Pwani ulimalizika kwa Ndanda kukubali kufungwa magoli 2-0.



No comments: