Monday, April 25, 2016

Masasi kutumia Bill. 11.3 kulipa mishahara 2016/2017.

Mwenyekiti wa Halmashauri ya mji wa Masasi, Sospeter Nachunga (mwenye kipaza sauti) akisoma dua kabla ya kuanza kwa kikao cha baraza la madiwani. Wapili kulia ni mkuu wa mkoa wa Mtwara, Halima Dendego akifuatiwa na mkuu wa wilaya ya Masasi, Benard Nduta.


Na Juma Mohamed, Masasi.

HALMASHAURI ya mji wa Masasi mkoani hapa imepanga kutumia kiasi cha sh. Bilioni 11.3 kwa ajili ya kulipa mishahara kwa watumishi wake ikiwa ni matumizi yanayotokana na kupitishwa kwa bajeti ya mwaka 2016/2017.

Taarifa iliyotolewa kwa vyombo vya habari na ofisa habari na mahusiano wa halmashauri hiyo, Clarence Chilumba, inaeleza kuwa matumizi hayo yanayotokana na bejeti nzima ya halmashauri hiyo iliyopitishwa ambayo ni sh. Bilioni 19.09 kwa mwaka wa fedha 2016/2017, ambapo ni sawa na asilimia 59.6 ya bajeti yote.

Taarifa hiyo ilieleza kuwa, matumizi mengine yanayotokana na bajeti hiyo ni fedha za utekelezaji wa miradi ya maendeleo kiasi cha bilioni 4.8 ambazo ni sawa na asilimia 25.19.
“Bajeti hii ya kiasi cha Tsh billion 19, 092,007,820.00 kwa mwaka wa fedha wa 2016/2017 imeongezeka kutoka  ile ya mwaka Jana ya Tsh. billioni 16,954,310,834.00 2015/2016 ambayo jumla ni sawa na ongezeko la asilimia 12.6.” ilieleza taarifa hiyo.
Aidha, kupitia bajeti hiyo, vipaumbele Saba vimepangwa kutekelezwa kwa mwaka wa fedha 2016/2017 ambavyo ni pamoja na kuwezesha upatikanaji wa elimu bora ya msingi na sekondari kwa kuzingatia usawa, kuongeza upatikanaji wa maji safi na salama katika maeneo ya pembezoni mwa halmashauri na kuboresha usafi wa mazingira hasa katika maeneo yenye msongamano kama Kituo cha mabasi na sokoni.

Vipaumbele vingine ni kuimarisha ukusanyaji wa Mapato ya ndani ya Halmashauri na kudhibiti matumizi ya fedha za Serikali za Mitaa na Serikali Kuu, kurasimisha makazi yasiyo rasmi na kuongeza kasi ya upimaji viwanja kwa ajili ya makazi,biashara,viwanda na maeneo ya kuabudia.

“Kuongeza wigo wa ajira  na kuboresha hali ya usalama wa kijamii (socio- Protection) hasa kwa wanawake , vijana, makundi maalumu, wazee na watu wanaoishi na virusi vya Ukimwi na Kukarabati miundombinu ya barabara za Halmashauri..” ilieleza.


Katika Makisio ya Mpango na Bajeti ya Mwaka 2016/17 Halmashauri hiyo imejikita katika  kutekeleza azma ya serikali ya kutoa elimu ya msingi na sekondari bila malipo kwa kufanya mambo kadhaa ikiwamo, kulipa likizo kwa walimu, Kugharamia Chakula mashuleni, Kulipa gharama za uhamisho kwa walimu, Uendeshaji wa ofisi na Gharama za mitihani.

2 comments:

Unknown said...

Safi sana kijana ubarikiwe ktk jina la Yesu

Juma Mohamed said...

Hongera sana Halmashauri ya mji wa Masasi..nadhani na wengine wataiga kutoka kwenu