Mbunge wa Tandahimba (CUF), Katan Ahmad, akizungumza na waandishi wa habari baada ya kumalizika kikao cha bodi ya barabara. |
Na Juma Mohamed, Mtwara.
WABUNGE
mkoani hapa wameitaka serikali kutekeleza ahadi zake inazozipanga ikiwamo ahadi
ya ujenzi wa barabara ya Mtwara-Nanyamba-Tandahimba-Newala na Masasi, ambayo
imekuwa kero kubwa kwa wananchi wa Mtwara.
Wakizungumza
mara baada ya kikao cha bodi ya barabara, walisema ahadi za ujenzi wa barabara
hiyo zimekua zikitolewa muda mrefu kuanzia serikali ya awamu ya Nne ambayo
mpaka inamaliza muda wake hakuna chochote kilichofanyika.
Walisema,
wakati wa kampeni za kuelekea uchaguzi mkuu wa mwaka jana, Rais wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania, Mhe. John Magufuli, aliwaahidi wananchi juu ya ujenzi wa
barabara hiyo yenye urefu wa Km 210, na kuwaambia kuwa tayari ilishatengewa
pesa zaidi ya sh. Bilioni 60.
“Lakini
jambo la ajabu leo tunakuja kwenye kikao tunapewa sanaa tu ya Bilioni 3.5
ambazo haziwezi kufanya jambo lolote..sasa hili ni jambo la ajabu sana na huu
wakati tuliokuwa nao sio wakati wa siasa, na muda wote huwezi kuwafanya
Watanzania kuwa watoto unazungumza jambo la Km 210 alafu kwenye bajeti unatoa
ahadi ya Km 50 lakini kwenye bajeti hakuna hata Km 5, sasa hii ni sanaa..”
alisema Katani Ahmad, Mbunge wa Tandahimba (CUF).
Aliwataka
wabunge wenzie wa mkoa wa Mtwara kulivalia njuga suala la ujenzi wa barabara
hiyo kwa kwenda kuonana na waziri husika kwa ajili ya kutoa msukumo na ikibidi
hata kwenda kuonana na Rais ili ahadi yake ianze kutekelezwa.
Naye,
mbuunge wa viti maalum (Chadema), Tunza Malapo, alisema changamoto kubwa
inayoyumbisha ujenzi wa barabara ni uchache wa fedha zinazotengwa na serikali
na wakati mwingine kutopatikana kabisa.
Mbunge wa viti maalum (CHADEMA), Tunza Malapo, akizungumza na waandishi wa habari juu ya kero za barabara Mtwara. |
“Ingawa
tumepewa matumaini kwamba watafuatilia na kutekeleza wale ambao wanahusika moja
kwa moja lakini na sisi kama wabunge tuna nafasi yetu ya kufuatilia na pia
kusisitiza kwa wale mawaziri wenye dhamana watusikie na kujali hasa barabara
yetu hii ya uchumi yenye Km 210..tumeambiwa kwa mpango wa awali itajengwa kwa
kiwango cha lami kwa Km 50 ingawa bado pesa ni tatizo lakini tutaendelea
kufuatilia na kusisitiza..” alisema.
Kwa upande
wake, mkuu wa mkoa wa Mtwara, Halima Dendego, alikiri kuwepo kwa changamoto za
upatikanaji wa fedha na kusema kuwa ndio inakwamisha kumalizwa kwa kero hiyo ya
muda mrefu kwa wakazi wa Mtwara na wilaya zake.
Alisema,
fedha inapochelewa kupatikana ndipo miradi inachelewa kuanza na kwamba kadri
barabara zinapokaa kwa muda mrefu bila kutengenezwa ndipo zinazidi kuharibika
hivyo mahitaji ya fedha yanakuwa makubwa mwaka hadi mwaka.
Mkuu wa mkoa wa Mtwara, Halima Dendego, akizungumza na waandishi wa habari baada ya kumalizika kikao cha bodi ya barabara. |
“Miradi ya
2015/2016 pesa yake hata senti moja bado hatujaipata, kwahiyo unapochelewa
kupata fedha hata utekelezaji wa miradi ambayo tumejipangia kuitekeleza inakua
inachelewa, inapochelewa basi changamoto inaongezeka kama eneo lenye uharibifu
lilikua dogo basi unaweza ukakuta limepanuka tena hata wakati wa utekelezaji
zile bajeti zinaweza kuwa sio halisia..” alisema.
Alisema
serikali ya mkoa bado inaendelea kuwasiliana na wizara ili kuhakikisha fedha
zinapatikana kwa wakati kwa ajili ya kuikamilisha miradi hiyo na kuzifanya
barabara ziweze kupitika vizuri kwa wakati wote wa mvua na jua.
No comments:
Post a Comment