Na Juma Mohamed, Mtwara.
WADAU wa
huduma za mawasiliano nchini ikiwamo Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA),
wametakiwa kufika vijijini kutoa elimu kwa wananchi juu ya namna ya kutambua
simu bandia ambazo zitafikia mwisho wa matumizi yake mwezi June mwaka huu.
Wito huo
ulitolewa juzi mkoani hapa na mkuu wa wilaya ya Mtwara, Fatma Ally, wakati wa
ufunguzi wa warsha kwa wanafunzi sekondari na wadau wengine wa huduma
zinazodhibitiwa, iliyoandaliwa na Jukwaa la watumiaji Tanzania (TCF), ikiwa ni
sehemu ya maandalizi ya maadhimisho ya siku ya kimataifa ya haki za mtumiaji
itakayofanyika kitaifa Machi 15 mwaka huu mkoani Mtwara.
Alisema
kutokana na maeneo mengi ya vijijini kuwa na miundombinu migumu kwa kuweza
kufikiwa na vyombo vya habari ambavyo vinatumika kutoa elimu hiyo, wananchi
wengi wanakosa kupata elimu na itawafanya waendelee kutumia na kununua simu
hizo ambazo ni bandia.
Wanafunzi wa shule za sekondari za Manispaa ya Mtwara Mikindani, waliohudhuria warsha ya kutoa elimu kwa watumiaji wa huduma zinazodhibitiwa, iliyoandaliwa na Jukwaa la Watumiaji Tanzania (TCF) |
“Kwahiyo
mtakapoweza kufikisha elimu hii kwao mtatusaidia wananchi kuweza kujua uwepo wa
hili naamini huko vijijini kuna simu ‘fake’ nyingi kuliko huku mjini..kutokana
na hofu ya kushindwa kuziuza simu hizi bandia, nimeharifiwa kwamba sasa hivi
zimeshushwa bei sana, na mnajua tumetoka kuuza korosho zetu kwahiyo wananchi
wana hela na wanafanya ‘shopping’ ya vitu mbalimbali..” alisema.
Aliongeza kuwa,
zoezi hilo litakapoanza wananchi wa vijijini ndio watakaoathirika zaidi
kwasababu hela zao wanazipata kwa misimu, na simu ni miongoni mwa mahitaji
muhimu kwa binadamu ambayo anakua na hamu ya kumiliki akipata hela.
Mkuu wa wilaya ya Mtwara, Fatma Ally. |
Kwa upande
wake, katibu mtendaji wa baraza la ushauri kutoka Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma
za Nishati na Maji (EWURA), Mhandisi Goodluck Mmari, alisema maadhimisho hayo
yanafanyika kwa kuandaliwa kwa pamoja na mabaraza ya ushauri ya watumiaji wa
taasisi za EWURA, Mamlaka ya Usimamizi wa Huduma za Usafiri wa Nchikavu na
Majini (SUMATRA), Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) pamoja na Mamlaka ya
Usafiri wa Anga Tanzania (TCAA).
Alisema,
taasisi hizo kwa pamoja zilifikia makubaliano ya kufanya maadhimisho hayo mwaka
huu mkoani Mtwara kwa kuzingatia sababu mbalimbali ikiwamo kuwapo kwa fursa
nyingi za kiuchumi zinazotokana na uwepo wa rasilimali za Mafuta na Gesi asilia
zilizopelekea kujengwa kwa kiwanda cha kuchakata gesi cha Madimba na kiwanda
cha Saruji cha Dangote.
“Mbali na
hivi vitu ambavyo nimevitaja na ambavyo vinaonekana Mhe. Mgeni rasmi (Mkuu wa
wilaya), kuna matarajio siku za usoni kwamba hapa Mtwara kitajengwa kiwanda cha
Mbolea, na kitajengwa hapa kwasababu malighafi ya kiwanda cha Mbolea yanatokana
na mabaki ya gesi..kuna matarajio ya siku za usoni kwamba itajengwa mitambo ya
kuzalisha umeme hapa ambao utaingizwa kwenye gredi ya Taifa..” alisema.
No comments:
Post a Comment