Tuesday, March 22, 2016

Bodi ya Korosho yakiri wakulima kutopata pembejeo za kutosha.

Mkurugenzi wa Bodi ya Korosho, Mfaume Juma.


Na Juma Mohamed, Mtwara.

BODI ya Korosho Tanzania (CBT) imekiri kuwapo kwa changamoto ya upatikanaji wa pembejeo za kutosha za zao hilo kwa wakulima, huku wengi wao wakiamini kuwa upo uwezekano wa kupata pembejeo za ruzuku kwa asilimia 100.
Akizungumza mkoani hapa katika kiako cha Kamati ya Ushauri ya Mkoa (RCC), mkurugenzi wa bodi hiyo, Mfaume Juma, alisema bajeti ya pembejeo za ruzuku inapitishwa na wadau wa zao hilo katika mkutano wa wadau ambao unafanyika kabla ya kuanza kwa msimu mpya.
Alisema, katika msimu wa mwaka jana, mkutano wa wadau ulipitisha bajeti ya tani 8,000 kwa ajili ya pembejeo za ruzuku kwa nchi nzima ambapo baadae walibaini kuwa kiasi hicho bado hakitoshi na kuamua msimu wa mwaka huu kupitisha bajeti ya tani 10,000.
“Tena ikasisitizwa zaidi kwamba tani 10,000 hizo zinunuliwe kutoka kwa watengenezaji, baadala ya kutangaza tenda ikaongeza ghalama ya pembejeo tupunguze ghalama hizi kwa wakulima ili tuwasaidie kupata pembejeo kwa bei nafuu zaidi na mapema kadiri inavyowezekana..” alisema.
Alisema mkutano huo pia uliamua kuwapo kwa nyongeza ya pemebejeo za tani 5,000 ili zisambazwe kwa utaratibu wa bei nafuu huku akifafanua zaidi kwa kusema kuwa bei hizo hazifanani na bei za sokoni kwasababu zinakua ni nusu yake.
Aidha, alisema bodi itasimamia uuzwaji wa pembejeo hizo na kuhakikisha haziuzwi kwa bei ya soko ili mkulima aweze kunufaika na ruzuku ambapo kutakuwa na mpango rasmi wa kuhakikisha hilo linafanyika kikamilifu na kuwashinda walanguzi.
“Na zitasambazwa kwa utaratibu rasmi, upo mpango kabisa umetengenezwa wa namna gani pembejeo za mei nafuu zitasambazwa kwa wakulima, ili isiingie katika mikono ya watu ambao sio waaminifu wakawauzia wakulima kwa bei ya kuwalangua..” alisema Mfaume.




No comments: