Thursday, October 1, 2015
NHIF sasa kuwatibu wachezaji VPL
Shirikisho la Mpira wa Miguu nchini (TFF), limeingia mkataba wa mwaka mmoja na Mfuko wa Taifa wa Bima ya afya (NHIF) kwa ajili ya kutoa huduma kwa wachezaji wa Ligi Kuu pamoja na viongozi wa benchi la ufundi.
Hafla ya kusaini mkataba huo imefanyika katika hoteli ya Protea Courtyard iliyopo Upanga jijini Dar es salaam ambapo katibu mkuu wa TFF, Mwesigwa Selestine na Mkurugenzi wa Masoko na Utafiti wa NHIF Rehani Athumani walisaini kwa niaba ya pande hizo mbili.
Akiongea na waandishi wa habari wakati wa mkutano wa uwekaji sahihi mkataba huo, Mwesigwa amesema anaishukuru NHIF kwa kudhamini kutoa huduma ya afya kwa wachezaji na mabenchi ya ufundi kwa vilabu vyote 16 vinavyoshiriki Ligi kuu ya Vodacom.
Aidha Mwesigwa ameviomba vilabu vya Ligi Kuu nchini kutoa ushirikiano na watoa huduma ya afya kwa wachezaji na viongozi kutoka NHIF pindi watakapokuwa wanafika kwenye vilabu vyao kwa ajili ya shughuli mbalimbali.
Mkurugenzi wa Masoko na Utafiti wa mfuko huo Rehani Athumani alisema wako tayari kufanya kazi na kutoa huduma ya afya kwa ngazi zote ikiwemo kwa timu za madaraja ya chini pia.
TFF na NHIF zimeingia mkataba wa mwaka mmoja wa udhamini wa huduma ya afya kwa wachezaji kwa ligi kuu na viongozi wa benchi la ufundi, mkataba ambao unaweza kuongezwa kila unapomalizika.
TFF kwa kupitia bodi ya ligi inavitaka vilabu vyote vya Ligi Kuu vitoe ushirikiano kwa wafanyakazi wa NHIF katika kurahisiha shughuli za usajili ikiwa ni pamoja na kutoa taarifa na nyaraka sahihi zikiwemo picha za wahusika katika muda sahihi.
SOURCE: TFF
I'm a Blogger, and News Reporter at East Africa Radio and Nipashe-News Paper. Available in Mtwara.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment