Friday, September 11, 2015

Serikali kupunguza idadi ya mizani barabarani.

Katibu Mkuu wa wizara ya viwanda na biashara, Uledi Mussa, akizungumza jambo katika semina ya kuboresha mazingira ya ufanyaji biashara na uwekezaji kwa maafisa biashara wa mikoa ya Lindi na Mtwara, iliyofanyika jana mkoani Mtwara


Maafisa biashara wa mikoa ya Lindi na Mtwara, wakiwa katika semina ya kuboresha mazingira ya ufanyaji biashara na uwekezaji, iliyoandaliwa na wizara ya viwanda na biashara na kufanyika jana mkoani Mtwara.

 

Na Juma Mohamed.

Katibu Mkuu wa Wizara ya Viwanda na Biashara, Uledi Mussa, amesema serikali ina mpango wa kupunguza vizuizi vya barabarani ambavyo vinawekwa kiholela, na kuchangia kuzorotesha maendeleo ya ukuaji wa chumi.
Akizungumza jana mkoani Mtwara katika semina ya kuboresha mazingira ya ufanyaji biashara na uwekezaji kwa maafisa biashara wa mikoa ya Lindi na Mtwara, amesema huo ni miongoni kwa mikakati iliyowekwa na serikali katika juhudi za kuondoa vikwazo kwa wafanya biashara.
Alisema, kumekuwa na usumbufu wanaoupata wafanya biashara katika maeneo mbalimbali hapa nchini kutokana na kudaiwa vibali katika biadhaa zingine ambazo hazistaili, jambo ambalo linarudisha nyuma ukuaji wa sekta hiyo.
“Polisi anakusimamisha ukiwa umepakia bati zako kwenye Canter anataka nini..alafu anauliza risiti inamuhusu nini, mtu kama ameibiwa bati zake si ataripoti huko na kesi itaanza..kwahiyo unakuta hata hapa mjini mtu akibeba matenga yake ya nyanya au nazi, basi kuna watu wanaulizia kibali..haiwezekani ndani ya wilaya hiyo hiyo bado kuwe na vikwazo..” alisema.

Uledi Mussa

Aliongeza kuwa, upo mpango wa kupunguza idadi ya mizani barabarani na kubakiza michache, huku akisema mizigo inayotolewa katika bandari ya Dar es Salaam kupelekwa nchi za Rwanda na Burundi inasimamishwa njiani katika vituo vitatu pekee.
“Kwahiyo tutapunguza hata idadi ya mizani barabarani, ili kusudi hata mzani upimwe tu pale patapohitajika kufanya hivyo..mtu utakuta anaweka ‘ka road block’ kake tu anavyotaka yeye, leo unaweza kukuta kuna ‘road block, kesho haipo alafu keshokutwa unaikuta tena..” aliongeza.
Kwa upande wake, Mkuu wa Kitengo cha Matokeo Makubwa Sasa (BRN) kutoka wizara hiyo, Sekela Mwaisela, alisema Tanzania imetajwa kuwa nyuma katika uanzishaji wa biashara ukilinganisha na nchi nyingine duniani.
Alisema, hali hiyo inayosababishwa na watu kutumia muda mwingi kufuatilia vitendea kazi vya biashara, imepelekea kuwa katika nafasi ya 119 kati ya nchi 189 baada ya utafiti uliofanywa mwaka jana na Benki ya Dunia (WB), huku ikipitwa na nchi ndogo kama Rwanda.
“Tanzania ili mtu aanze kufanya biashara anatumia karibu siku 26 wakati nchi kama New Zealand inatumia siku moja..vilevile katika gharama za kufuatilia vitendea kazi kama vile leseni, kusajili kampuni na mambo mengine utakuta kwamba Tanzania tunachukuwa muda mrefu sana na gharama nyingi kwasababu ya utendaji wetu ulivyo.” Alisema.
 



Alisema, kutokana na changamoto hizo, wizara imekuja na mikakati ya kuweza kubadilisha utendaji wa serikali ili kuweza kufupisha muda unaotumika katika mchakato wa kusajili kampuni, kwa kuanzisha mifumo ambayo inamuwezesha mfanya biashara kutumia siku moja.
Alisema utekelezaji wa mikakati hiyo umeanza ambapo sasa Wakala wa Usajili wa Kampuni Nchini (BRELA) inatumia muda wa nusu saa (Dakika 30) katika zoezi la kusajili jina la kampuni na kwamba mtu anaweza kusajili maali popote alipo.
“Na mkakati mwingine ni kwamba wizara tumeanza kutoa hizi semina kwa watendaji kwasababu utendaji mwingi upo chini ya serikali za mitaa, ambao ndio watendaji wakubwa na wako karibu zaidi na wananchi..kwahiyo hii elimu tumeanza kuishusha huko ili waweze kuwaelimisha wananchi..” alisema.
Naye, kaimu katibu tawala wa mkoa wa Mtwara, Johansen Bukwali, aliwataka maafisa biashara hao kuyatumia vizuri mafunzo hayo wanayoyapata , kwasababu hali ya uchumi wa mkoa huo inaelekea kukuwa kwa kasi na kwamba viwanda zaidi ya 40 vinatarajiwa kujengwa kutokana na kuwepo kwa rasilimali za gesi na mafuta.
 
   
 

No comments: