Tuesday, September 29, 2015

MTPC kuwa mwanachama mpya wa NHIF.


Baadhi ya waandishi na wanachama wa Chama cha Waandishi wa Habari Mkoa wa Mtwara (MTPC), wakiwa katika semina ya siku moja juu ya mpango wa Kikoa wa Mfuko wa Taifa wa Bima ya Ayfa (NHIF), iliyofanyika jana mjini Mtwara.


Waaandishi na wanachama wa MTPC

Na Juma Mohamed.

MFUKO wa Taifa wa Bima ya Ayfa (NHIF) kanda ya kusini, umeingia makubaliano ya awali na Chama cha Waandishi wa Habari Mkoa wa Mtwara (MTPC), kwa ajili ya kuwa mwanachama wa mfuko huo kupitia mpango wa Kikoa.
Akizungumza jana mkoani hapa katika semina ya siku moja kwa wanachama wa MTPC, meneja wa mfuko huo kanda ya kusini, Joyce Sungwe, alisema, mpango wa Kikoa ni utaratibu wa utoaji huduma za afya kwa kadi kwa vikundi/ushirika vilivyo katika sekta isiyo rasmi, ambapo miongoni mwa sekta hizo ni pamoja na wajasiriamali, VIBINDO, VICOBA na AMCOS.

Meneja wa Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF) kanda ya kusini, Joyce Sungwe, akifafanua jambo katika semina ya siku moja juu ya mpango wa Kikoa wa mfuko huo, iliyofanyika jana mjini Mtwara.

Alisema, mpango huo ni miongoni mwa mikakati ya NHIF ya kuwaunganisha wanachama wengi zaidi kuweza kupata huduma za matibabu zinazogharamiwa na mfuko, ambapo gharama kwa kila mwanachama wa MTPC atakaye hitaji kadi ya uanachama itakuwa ni sh. 76,800 kwa mwaka.
“Mfuko umekuwa na mipango ya aina mbalimbali kwa makundi mbalimbali ili kuhakikisha watanzania wengi wanapata matibabu kupitia mfuko huu..ndio maana leo ni rasmi kwa ajili ya wanachama wa Press Club, kwasababu kama ukiwa Press Club unapata bima ya afya kwanini wanahabari wengine ambao sio wanachama wasijiunge na uanachama..” alisema
Aidha, alitoa angalizo kwa kuzitaja huduma maalumu ambazo mwanachama wa mfuko hatoweza kuzipata katika mwaka wake wa kwanza wa kujiunga, ambazo ni vipimo vya MRI na CT Scan, huduma za kusafisha damu (haemodialysis), dawa za saratani (chemotherapy) na dawa kwa waliopandikizwa figo (immunosuppressant).

Waaandishi na wananchama wa MTPC

Alisema, utaratibu wa huduma hizo upo sio tu kwa wanachama wa mpango wa Kikoa, bali ni kwa wanachama wote wa NHIF na kwamba huduma za mwanacha wa Kikoa ni sawa na anazopata mwanachama mwingine anaengia kupitia utaratibu mwingine.
Kwa upande wake, katibu mtendaji wa MTPC, Bryson Mshana, alisema kutokana na waandishi wengi kufanya kazi katika mazingira magumu na huku baadhi yao wakiwa hawana mikataba ya kudumu katika vyombo vyao, mpango huo utasaidia sana hivyo kama chama, kimeona kuna umuhimu mkubwa wa kupatiwa kadi za bima ya afya wanachama wake ili kuweza kuwarahisihia katika kupata huduma za matibabu wanapopatwa na matatizo ya kiafya.
“Kwa kupitia mpango huu ambao ni kwa kuchangia kiasi cha sh. 76,800 unamfanya mwanahabari kujiunga na bima afya na kuwa na sifa kama mwanachama mwingine aliejiunga kupitia mfumo mwingine, ni dhahiri kwamba wanahabari wa mkoa wa Mtwara watanufaika na hili..” alisema.
Na kuongeza “niwashawishi tu sasa wale ambao hawajajiunga na Mtwara Press Club, waendelee kujiunga kwa wingi kwa ajili ya kuhakikisha wananufaika na utaratibu huu ambao bima ya afya umeamua kuja nao kwasababu ni njia pekee ya kumkomboa mwanahabari katika swala la afya yake..” aliongeza.

No comments: