Sunday, September 27, 2015

ACT waunguruma Mtwara, wagongana na CCM kufanya mikutano- waahidi rasilimali za taifa kumilikiwa na wananchi kikatiba.


Mgombea Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia chama cha ACT-Wazalendo, Anna Mngwira, akinadi sera za chama jana katika mkutano wa hadhara uliofanyika katika uwanja wa Mashujaa mjini Mtwara.



Anna Mngwira


Na Juma Mohamed.

MGOMBEA Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia chama cha ACT-Wazalendo, Anna Mngwira, amesema iwapo chama hicho kitapata ridhaa ya kuongoza nchi, kitahakikisha rasilimali za madini, gesi asilia na mafuta zinamilikiwa na wananchi kikatiba.
Akizungumza katika mkutano wa kunadi sera za chama hicho uliofanyika katika uwanja wa Mashujaa mkoani hapa, alisema swala hilo tayari lipo katika ilani ya chama hicho na kwamba, wananchi ndio watakuwa na hati miliki ya rasilimali hizo za taifa.

Anna Mngwira

 Alisema, mfumo wa uchimbaji wa rasilimali hizo utabadilika kutoka katika mfumo wa sasa wa kukusanya kodi na mirahaba, na kuingia katika mfumo mpya wa umiliki na ukandarasi ambao utampa mwanachi kibali cha kuwa na hati miliki ya rasilimali hizo.
“Maana yake atakaekuwa na hati miliki ya maliasili yoyote, iwe misitu, gesi na vingine ni mwananchi kupitia serikalio yake au shirika la umma, na mkandarasi au mwekezaji atafanya kazi ya ukandarasi tu..akimaliza kazi yake atahesabu mapato alafu tutagawana faida..” alisema.
Alisema, rasilimali ya gesi asilia iliyopo katika mkoa wa Mtwara, iwapo chama hicho kitapata ridhaa kitahakikisha inawanufaisha wananchi wa mkoa huo na kwamba kutakuwa na ndege ya Mtwara huku akitaja faida zingine kuwa ni kujenga barabara na wanafunzi kusoma bure.

Wananchi waliojitokeza katika uwanja wa Mashujaa mjini Mtwara jana kusikiliza sera za chama cha ACT-Wazalendo, katika mkutano wa hadhara uliofanywa na mgombea wa Urais wa chama hicho Anna Mngwira, aliyeambatana na mgombea mwenza, Hamad Yusuf.

 Aliwataka wananchi kuwa makini katika kusikiliza hoja za wagombea jambo litakalowawezesha kuchaguwa kiongozi makini, na kwamba wasibabaike na ‘mafuriko’ ya watu katika mikutano.
“na ninamuomba mungu sana kwa imani na kwa moyo wa dhati kabisa mbele yenu na mbele ya mungu kwamba mwaka huu tusikosee na tusidanganywe na mafuriko ya kubebwa, twende na mafuriko ya hoja..kama wana hoja za msingi tuwape, kama hawana hoja za msingi tuwakatae waziwazi hatakama ni ACT wazalendo tuwakatae, kwasababu hapa tulipofika hakuna tena kutazama mahali pakutazama nyuma, ni kutazama mbele tena kwa makini..” alisema.
Awali, mgombea mwenza wa chama hicho, Hamad Yusuf, alisema miradi mbalimbali ya uwekezaji iliypangwa kufanyika mjini Bagamoyo ikiwa ni pamoja na uwanja wa ndege na bandari, itafutwa na baadala yake uwekezaji huo utafanyika mkoani Mtwara.
“Rais Kikwete amaemaliza akapumzike, uwanja wa ndege wa kichina ambao anataka kujengwa Bagamoyo kwao, nchi haiendeshwi hivyo, ACT-Wazalendo mkituchaguwa uwanja ule unakuja Mtwara..biashara ya Kikwete imekwisha Tanzania, bandari ya Bagamoyo tunafuta mpango huo na tunakuja kuboresha bandari ya Mtwara..” alisema.
Alisema serikali ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) kimeufanya mkoa wa Mtwara kuwa nyuma kimaendeleo kutokana na kuwanyima elimu wananchi wake, ambapo wanashindwa kufaidika na uwekezaji wa viwanda unaofanyika sasa kwa kukosa ajira za kudumu, na kuwataka wananchi kutokipa nafasi tena chama hicho ya kuendelea kutawala.
Wakati huo huo, mgombea Ubunge wa jimbo la Mtwara mjini kupitia CCM, Hasnain Murji, naye alifanya mkutano wake wa uzinduzi wa kampeni katika viwanja vya Nkanaredi, mjini hapa.
Kitendo hicho kimepelekea kugongana kwa mikutano miwili ya kisiasa ya vyama viwili tofauti, huku mkutano mmoja ukiwa ni wa mgombea wa Urais, jambo ambalo viongozi wa ACT wamelilalamikia na kuahidi kulifanyia kazi kwa kulifikisha katika vyombo husika.
Mwenyekiti wa chama hicho Taifa, Shabani Mambo, alisema kitendo hicho kinaonesha udhaifu kwa wahusika, ambapo wameshindwa kufuata ratiba za mikutano na kwamba hakukuwa na uhalali wa kuwa na mkutano mwingine tofauti na wakwao.

No comments: