Saturday, August 22, 2015

Watu wasiojulikana wavamia na kubomoa nyumba ya mgombea ubunge, baada ya kuto rudisha fomu.


Nyumba ya mgombea ubunge wa jimbo la Nanyamba kupitia Chama cha Wananchi (CUF), Twahili Said, ikiwa imebomolewa vibaya na watu wasiojulikana usiku wa juzi kuamkia jana, baada ya mgombea huyo kuto rudisha fomu ya ugombea na kutokomea kusikojulikana na kutoa fursa kwa mgombea wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Abdallah Chikota kukosa mpinzani. 



Na Juma Mohamed, Mtwara.
KIKUNDI cha watu wasio julikana kimevamia na kubomoa nyumba ya mgombea ubunge wa jimbo la Nanyamba wilaya ya Mtwara vijijini, kupitia Chama cha Wananchi (CUF), Twahili Saidi, ambaye alishindwa kurudisha fomu ya ugombea na kutokomea kusikojulikana.
Tukio hio limetokea usiku wa juzi kuamkia jana katika kijiji cha Milangominne, halmashauri ya mji wa Nanyamba, na kwamba linahusishwa na kukerwa na kitendo cha mgombea huyo ambaye alipewa ridhaa na Umoja wa Katiba ya Wananchi (UKAWA) kuwakilisha jimbo hilo, kutorudisha fomu na badala yake kumfanya mgombea wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Abdallah Chikota kukosa mpinzani.
Baadhi ya wananchi wa jimbo hilo ambao walikuwa wanamuunga mkono mgombea huyo wametoa maoni yao huku wengine wakidai kuwa ameuza jimbo kwa mgombea wa CCM jambo ambalo limewasikitisha na kukosa imani naye.
“Tulimpa ile dhamana tukiwa na imani kwamba atatuwakilisha, lakini sasa ndio tumefehamu kabisa kwamba hakwenda kwa dhati kama mwakilishi wa wananchi.. alikuwa na mawazo binafsi ambayo yalipelekea vishawishi, tama ya maisaha na kipato cha haraka na kufikia hatua sasa ya kuuza haki za wananchi, kwasababu ile sio haki yake ni haki yetu sisi..” alisema Maspana Rashidi Maspana mkazi wa kata ya Dinyecha, Nanyamba.
Aliongeza kuwa, wakazi wa jimbo hilo wamenyanyasika kwa muda mrefu kwa kutopata mbunge wanaomuhitaji wa kutatua kero zao, hivyo alivyojitokeza walijua ni mtu sahihi kutokana na elimu yake na uzalendo aliokuwa ameuonyesha mwanzo.
Naye, Mohamed Yusufu Mnemo, alisema mgombea huyo alifika ofisi za msimamizi wa uchaguzi katika halmashauri ya Nanyamba, Oscar Ng’itu, juzi majira ya saa nne asubuhi akiwa na lengo la kurejesha fomu lakini baadae alikutana na kigogo mmoja wa CCM (Jina linahifadhiwa) ambaye alimrudisha.
“Na Yule mgombea wetu akashindwa kurudisha fomu kwa makubaliano yao..na huu mchezo mimi nimeshaujua siku nyingi toka wakati wa uchaguzi wa serikali za mitaa, walishaandaliwa hawa watu na waliitwa wasomi..walikutana Mikindani (Manispaa ya Mtwara) wakaongelea habari za uchaguzi ujao na kupanga timu ya kuja kuvuruga..na kuna baadhi ya wananchi tuliwaambia kwamba mgombea tutakaye msimamisha tumchunguze..” alisema.
Mwenyekiti wa jimbo la Nanyamba kupitia Chama cha Wananchi (CUF), Jamali Katende, alisema taarifa hizo walizipokea kwa masikitiko kama viongozi lakini pia na baadhi ya wanachama kiasi cha kutaka kufanya fujo lakini viongozi waliyumia busara na kuweza kuwatuliza kwa masilahi yao na chama kwa ujumla.
“Kwasababu lengo la chama cha siasa ni kama taasisi yenye kukusudia kushika dola, na kama chama tulifanya mchakato wa kuweza kumpata yeye ili aweze kusimama na kushika dola..kwahiyo tulipopata taarifa kwamba muda wa kurudisha fomu umepita na mgombea wetu hajarudisha kwakweli tulisikishwa sana..na hii itachangia mgogoro kwa kiasi cha kama asilimia 25 ya watu kutokuwa na imani na chama hiki kwa kuona wakisimamisha mgombea hawezi kufikia lengo.” Alisema.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa halmashauri hiyo, Oscar Ng’itu, alikiri kutokea kwa tukio hilo na kusema kwamba baada ya kupata taarifa aliamua kufika eneo la tukio na kushuhudia kubomolewa kwa nyumba hiyo ambayo ilizungukwa na nyumba za wakazi wengine.
Alisema baada ya kujiridhisha kuwa na uwezekano wa kufahamika kwa waliofanya tukio hilo, aliamua kufanya kikao na viongozi wa kijiji, kata na wa CUF na kuwaagiza kutafuta majina ya waliohusika mpaka kufikia jana saa 6 mchana yapatikane, na vinginevyo dola itachukuwa hatua.
“Nitasaidiana na viongozi wa wilaya ili waweze kuwasiliana na viongozi wa mkoa waone nini kinaweza kufanyika..lakini tu niwaombe wananchi, maswala ya siasa ni maswala ya kupita, na tunavyozungumzia uchaguzi ni jambo tu la muda Fulani linapita na maisha yanaendelea..sasa leo tunavyosababisha vurugu kama hizi, Napata picha ya tarehe 25 sehemu kama hii inapaswa kuiangalia, kitu ambacho so kizuri..” alisema.
Jumla ya wagombea watau walichukuwa fomu katika jimbo hilo ambao ni Twaha Saidi (CUF), Severin Simon ( CHADEMA) na Abdallah Chikota (CCM) na aliyerudisha ni Chikota pekeake huku Severin wa Chadema akimuachia mgombea wa CUF kutokana na makubaliano ya UKAWA.
 

No comments: