Na Juma
Mohamed, Mtwara.
MGOMBEA
Ubunge wa jimbo la Mtwara mjini kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM) Hasnain
Murji, amesema atawafikisha mahakami wananchi watakaothubutu kuwazomea
wanachama wa CCM wanaovaa sare za chama na kutembea mitaani.
Hatua hiyo
imekuja baada ya malalamiko yaliyotolewa na baadhi ya wanachama wa chama hicho
katika mkutano wa uzinduzi wa kampeni kwa mgombea huyo, uliofanyika jana katika
ukumbi wa Chuo Kikuu Kishiriki cha Mtakatifu Augustine (SAUT) tawi la Mtwara,
ambapo walisema hali hiyo inawapa shida na kuwakosesha raha kiasi cha kuhofia
kutembea wakiwa wamevaa sare.
Murji
aliwataka wana-CCM kutokuwa na wasiwasi juu ya kuvaa sare na kutembea nazo, na
kwamba atakaewazomea jukumu la kumkamata na kumfikisha mahakamani litakuwa
chini yake.
“Mimi nataka
sasa wana-CCM tuvae sare, na ninawahakikishia kuwa mtu yeyote atakaekuja
kutuzomea mimi nitakufa nae mpaka mahakamani..safari hii tumejipanga vizuri na
tuna wanasheria watatu, mtu yeyote atakaemchezea mwanachama wa CCM hatumuachi
tunampeleka mahakamani na wanasheria wapo na gharama hiyo nitailipia mimi.” Alisema.
Aidha, aliwataka
wanachama kutomuangusha katika uchaguzi mkuu ujao kutokana na ahadi ambayo
aliitoa mbele ya Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Jakaya
Kikwete alipotembelea mkoani hapa kuzindua miradi mbalimbali, kwamba Mtwara
ndio mkoa ambao utampa kura nyingi mgombea wa Urais wa chama hicho Dkt. John
Magufuli.
“Nilisimama
nikajitia kitanzi mbele ya Magufuli, nikamwambia ndugu yangu Kikwete unamaliza,
nikamwambia mgombea wa Urais nakuhakikishia utapata kura nyingi Mtwara kuliko
mkoa au wilaya nyingine yoyote nadhani mnakumbuka..kile kitanzi naomba mnitoe
aibu ile na tumpe kura nyingi Magufuli..na niwaambie tu kwamba siku ile
wana-Mtwara mlinitoa kimasomaso kwa mlivyonishangilia..” alisema.
Alisema
Umoja wa Katiba ya Wananchi (UKAWA) wakosa demokrasia kutokana na kila mtu
kutaka uongozi na kwamba mtu ukitaka kununua uongozi unaweza huku akidai kwamba
viongozi wa UKAWA walikuwa wanamtamani ajiunge kwao lakini hawajafanikiwa.
Aliongeza kuwa,
siku ya kurudisha fomu ya ugombea aliongea na wanahabari na kuwaeleza kwamba wagombea
wa upinzani wanaogombea katika jimbo la Mtwara mjini wote wanataka ajira na sio
ubunge kutokana na kutokuwa na makazi ya kudumu.
“Leo mgombea
yeyote wa ubunge aliyekuja kugombea kupitia chama chako kigezo cha kwanza ili
wana-Mtwara tumpe kura, atuonyeshe nyumba anayolala ili tukipata shida twende..wengine
wapo ‘guest’ (Nyumba za wageni), wengine wanalala kwa ndugu zao wakifukuzwa
kesho tutawapata wapi..”aliongeza Murji.
No comments:
Post a Comment