Na Juma
Mohamed, Mtwara.
WIZARA ya
afya na ustawi wa jamii imezindua kambi ya kufanyia upasuaji kwa watu wenye
matatizo ya Mabusha na Matende, katika hospitali ya rufaa ya Ligula, manispaa
ya Mtwara Mikindani.
Uzinduzi huo
umefanyika leo ambapo wagonjwa wasiopungua 100 wanatarajiwa kufanyiwa upasuaji
kupitia huduma zitakazotolewa na madaktari bingwa wa upasuaji kutoka hospitali
ya taifa ya Muhimbili.
Abdallaha
Namanga, mkazi wa Mbaye Mashariki, alisema fursa hiyo ni adimu ambayo
inapatikana mara moja kwa mwaka, na kwamba ilipojitokeza wamelazimika
kuichangamkia kwasababu ikipita gharama zinakuwa kubwa za kupata matibabu
tofauti na uwezo wao.
Alisema,
kutokana na kusumbuliwa na tatizo la busha, alikuwa anahisi kunyanyasika na
kukosa raha anapokuwa katika shughuli zake za kila siku huku baadhi wa watu
wakimtania jambo ambalo lilimlazimu avae nguo kubwa kwa ajili ya kuzuia watu
wasitambue kwa urahisi matatizo yake.
“Niliona
kama nanyanyasika kijinsia yani mtu anakutania kwamba una mpira..sasa inabidi
upate shati ‘over size’ ili kuzuia, sasa kwakweli kitu kama kile nilikua naumia
moyo sana..sasa jana nimekaa nyumbani majira ya saa mbili nikasikia gari la
matangazo, nikasema hapana nikamuaga mke wangu lakini sikumwambia naenda wapi..”
alisema.
Omari
Makongoro, mkazi wa kata ya Likombe, ambaye anasumbuliwa na busha na mlemavu wa
mguu, alienda mbali zaidi na kuwataka wasamalia wema kumsaidia kwa namna yoyote
ili aweze kuendesha maisha yake kutokana na kukosa ndugu wa kuweza kumsaidia.
Alisema
tatizo la busha limekuwa likimsumbua kwa kipindi kirefu na kwamba awali aliwahi
kufanyiwa upasuaji lakini limemrudia tena kwa mara ya pili kiasi cha
kumzidishia matatizo ukilinganisha na hali yake ya ulemavu na ukosefu wa kipato
alionao kwa sasa.
“Naomba
msaada kwa redio zote za mjini hapa na wasamalia wema, ninavyoishi nyumbani
huko hali ni mbaya sana..bora mwanzo nilikuwa na Baiskeli ambayo ilikuwa
ikinisaidia kuzunguka mitaani na kupata chochote lakini sasaivi Baiskeli
imekufa kwahiyo siwezi kutembea tena, sasa nafikiria nitaishi vipi..ndio naomba
waisilamu wenzangu na wakristo, maana mungu ni mmoja ..” alieleza.
Naye,
Mkurugenzi wa Taasisi ya Uchunguzi wa Magonjwa ya Binadamu (NIMR), Dkt. Mwele
Malecela, alisema wizara ya afya imeweka mkazo katika mkoa wa Mtwara kwasababu
umekuwa ni mkoa mmojawapo kati ya mine ya Tanzania ambayo inaongoza kwa kuwa na
wagonjwa wengi wa matatizo ya mabusha.
Alisema
kumekuwa na idadi kubwa ya wagonjwa wenye matatizo hayo hapa nchini na kwamba
ili kufikia malengo ya 2020, ni lazima zifanyike jitihada kubwa zaidi kuwafikia
wagonjwa wote wanaohitaji upasuaji kabla ya mwaka huo.
“Mkakati wa
kutokomeza matende una sura mbili kuu, ya kwanza ni kumaliza kabisa maambukizi
kati ya Mbu na Binadamu na pili ni kutoa huduma kwa ambao tayari wameathirika
kwa ugonjwa huu..na hii sababu ya pili ndio imetuleta hapa leo..” alisema.
Kwa upande
wake, Kaimu katibu tawala wa mkoa wa Mtwara, Johansen Bukwali, akizungumza kwa
niaba ya mkuu wa mkoa Halima Dendego, aliwataka viongozi wa halmashauri
kuhakikisha kwamba halmashauri zao zinatenga fedha kila mwaka kwa ajili ya
kufanya huduma za upasuaji wa Ngirimaji, na sio kuwategemea wafadhili pekeao.
“Tukumbuke
kwamba, wafadhili wanatusaidia, lakini wenye dhamana ya afya kwa wananchi wetu
ni sisi wenyewe viongozi wa mkoa na wilaya, na pia tuhakikishe tunajenga
mazingira mazuri ya kazi hii ili iwe endelevu.” Alisema.
Mwakilishi
wa kampuni ya Statoil inayoshughulika na utafiti na uchimbaji wa rasilimali za
mafuta na gesi mkoani hapa, ambao ndio wafadhili wa shughuli hiyo, Naomi
Makota, alisema kupitia mpango wao wa Maisha ni Ushirikiano, waliweza kuanza
kuungana na watu wa Mpango wa Magonjwa Yasiyopewa Kipaumbele (NTDs) ambao
waliwaomba wachangie katika kudhibiti magonjwa ya Ngirimaji.
Alisema,
ufadhili wao katika shughuli hiyo umegharimu kiasi cha dola za kimarekani 250, 88 ambapo walikabidhi mfano wa hundi yenye thamani hiyo kwa mkurugenzi wa
kinga wa NTDs, Dkt. Neema Rusibamayila.
No comments:
Post a Comment