Manji ajisalimisha Mahakama Kuu
MWENYEKITI wa Yanga, Yusuph Manji na Katibu wake, Laurence Mwalusako,
wamejisalimisha Mahakama Kuu Kitengo cha Kazi ili wajieleze kwa nini
wasifungwe jela kwa kukaidi amri ya mahakama.
Viongozi hao walijisalimisha jana, mbele ya Msajili wa mahakama
hiyo, Mohammed Gwaye, baada ya kutakiwa kufanya hivyo kwa sababu
walishindwa kuwasilisha mahakamani hapo dhamana ya Sh 106,300,000.
Gwaye
aliwaamuru kuwasilisha dhamana hiyo wakati wakisubiri hatima ya marejeo
ya uamuzi uliotolewa na Kamisheni ya Usuluhishi wa Migogoro,
iliyowataka Yanga kuwalipa wachezaji waliowafukuza jumla ya Sh
106,300,000 kwa kuvunja mikataba yao kinyume cha sheria.
Wachezaji
hao ni Steven Malashi na Wisdom Ndlovu kutoka Malawi, waliochukuliwa na
Yanga kwa mkataba wa miaka miwili wakati wakijiandaa kwa kipindi cha
Ligi Kuu.
Malashi na Ndlovu walikimbilia Kamisheni ya Usuluhishi,
mgogoro wao ulisikilizwa huku Yanga wakigoma, ambapo Mahakama iliamuru
Ndlovu alipwe Sh milioni 57, zikiwa ni mishahara ya miaka miwili, Sh
1,800,000 gharama za usafiri kutoka Malawi, Sh milioni 20 fidia, wakati
Malashi aliamuliwa kulipwa Sh milioni 18 za mshahara wa miaka miwili, Sh
milioni 10 fidia na Sh 500,000 fedha zake za usajili zilizobaki kwa
mwaka 2009 na 2010.
Msajili wa Mahakama Kuu Kitengo cha Kazi,
Mohammed Gwaye, alitoa uamuzi wa maombi hayo Februari 4 mwaka huu,
akiamuru Yanga kuwasilisha fedha hizo mahakamani wakati wakisubiri
hatima ya marejeo, lakini hawakufanya hivyo hadi ilipotolewa amri ya
kuitwa mahakamani kueleza kwa nini wasifungwe jela kwa kushindwa
kutekeleza amri ya mahakama.
Manji na Mwalusako walifika mbele ya
Msajili Gwaye kwa ajili ya kujieleza kwa nini wasifungwe, lakini
msajili hakuwapa nafasi ya kuwasikiliza wala kuhoji kwa sababu jalada
mama la kesi hiyo liko Mahakama ya Rufaa.
Katika kiapo
kilichoapwa na Mwalusaka, anadai kwamba msuluhishi wakati akitoa uamuzi
hakutilia maanani nafasi ya Yanga, kwani haina mali za kuiwezesha kulipa
fedha hizo, hivyo wanaomba uamuzi ubatilishwe.
SOURCE: MTANZANIA
No comments:
Post a Comment