Wednesday, June 20, 2012

BREAKING NEWS; ALLY MAYAY AENGULIWA UCHAGUZI YANGA


Ally Mayay Tembele

Na Prince Akbar
KAMATI ya Uchaguzi ya klabu ya Yanga ya Dar es Salaam, imemuengua mgombea nafasi ya Makamu Mwenyekiti, Ally Mayay Temebele kwa sababu mbili; kwanza pingamizi alilowekewa na pili kuidharau Kamati hiyo kwa kutofika kwenye usikilizwaji wa pingamizi lake bila ya taarifa yoyote.
Katibu wa Kamati hiyo, Francis Kaswahili ameambia BIN ZUBEIRY jioni hii kwamba pingamizi alilowekewa Mayay lilistahili majibu yake, lakini kwa kuwa hakutokea Kamati imeona mambo mawili, mtoa pingamizi ana hoja na pili Mayay ameidharau Kamati hiyo kwa kutofika bila taarifa.
Kaswahili alisema pingamizi dhidi ya ‘Meja’ Mayay, Nahodha wa zamani wa Yanga lilikuwa kuhusu kushindwa kutekeleza majukumu yake awali, akiwa kiongozi wa klabu hiyo na ndani ya muda mfupi anaomba tena uongozi.
“Wagombea wengine wote wamepitishwa kuendelea na usajili kwa ajili ya uchaguzi, isipokuwa Ally Mayay pekee,”alisema Kasawahili.
Kuenguliwa kwa Mayay, kunafanya nafasi ya Makamu Mwenyekiti ibakiwe na watu watatu, ambao ni Ayoub Nyenzi, Yono Kevela na Clement Sanga, wakati wagombea Uenyekiti ni Yussuf Mehboob Manj, John Jambele, Edgar Chibura na Sarah Ramadhani.
Katika nafasi za Ujumbe ni Lameck Nyambaya, Ramadhani Mzimba ‘Kampira’, Mohamed Mbaraka, Ramadhani Said, Edgar Fongo, Beda Simba, Ahmad Gao, Mussa Katabaro, George Manyama, Aaron Nyanda, Abdallah Bin Kleb, Omary Ndula, Shaaban Katwila, Jumanne Mohamed Mwammenywa, Abdallah Mbaraka, Peter Haule, Justin Baruti na Abdallah Sharia.
Awali, Mkuu wa Wilaya ya Handeni, Muhingo Rweyemamu, Mfanyabiashara Muzamil Katunzi na Katibu Mkuu wa Wizara ya Madini, Eliakhim Masu walichukua fomu za kugombea Ujumbe lakini wakashindwa kurudisha, wakati Isaac Chanzi pia hakurudisha fomu ya Makamu Mwenyekiti hivyo moja kwa moja hao hawamo katika kinyang’anyiro.
Uchaguzi huo, unaokuja baada ya Wajumbe wengi wa Kamati ya Utendaji katika uongozi uliokuwa madarakani, akiwemo Mwenyekiti Wakili Lloyd Baharagu Nchunga na Makamu wake, Davis David Mosha kujiuzulu utafanyika Julai 15, mwaka huu Dar es Salaam.
Mapema jana, Mwenyekiti wa Kamati ya Uchaguzi ya klabu hiyo, walipokea pingamizi dhidi ya wagombea Uenyekiti, Manji na Sarah Ramadhani, Makamu Mwenyekiti, Yono Kevella, Clement Sanga na Ally Mayay.
Lakini Jaji Mkwawa amesema Kamati yake inaweza kusikiliza na kuamua kuhusu mapingamizi hayo bila ya kuwepo waliowekewa au walioweka, ila tu amesistiza ni vema wakawepo ili watetee hoja zao.
Aidha, kuhusu tamko la mwanachama Abeid Abeid ‘Falcon’ kutaka ufafanuzi wa Katiba ipi itatumika katika uchaguzi huo, Jaji Mkwawa alisema itatumika Katiba ya mwaka 2010 iliyowasilishwa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) Juni 17, mwaka huo.
Amemtoa wasiwasi Abeid kwamba katiba ya 2011 iliyokuwa na matatizo kiasi cha kupingwa mahakamani na wanachama wa klabu hiyo haitatumika.
Lakini pia, Mkwawa amesema pamoja na kwamba uchaguzi huu unakuja baada ya Wajumbe wengi wa Kamati ya Utendaji, wakiwemo Mwenyekiti na Makamu wake kujiuzulu, Wajumbe waliojiuzulu kutoka kwenye uongozi huo wanaruhusiwa kugombea.
Aidha, kuhusu wagombea kusaidia klabu katika masuala yanayohusu fedha katika kipindi hiki kigumu, Jaji Mkwawa amesema hayana matatizo yakifanyika katika taratibu zinazoeleweka.
Baada ya kusikiliza pingamizi kesho, Jaji Mkwawa amesema usaili utafanyika Juni 22 na Uchaguzi wa Yanga utafanyika Julai 15 kama ilivyopangwa, siku moja baada ya kuanza kwa Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati, Kombe la Kagame, michuano ambayo, Yanga ni bingwa wake mtetezi.

AZAM WAENDELEA KUKAMUA HADI UFUKWENI


Wachezaji walioipa Azam Medali ya Fedha Ligi Kuu msimu uliopita


Na Prince Akbar
KLABU ya Azam FC inaendelea vema na maandalizi yake ya Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati, CECAFA Kagame na leo asubuhi walifanya mazoezi katika ufukwe wa Coco Beach, Dar es Salaam.
Azam ilianza mazoezi ya viungo na kusaka pumzi na stamina wiki mbili zilizopita, Beach na Gym na wiki wanatarajiwa kuanza kuuchezea mpira.
Tayari Azam, washindi wa pili wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara wamekwishamalisha usajili wa wachezaji wao hata kabla ya kwenda likizo.
Programu ya maandalizi ya Kombe la Kagame, inayoendelea hivi sasa itamalizika siku moja kabla ya kuanza mashindano hayo, Juni 28 na yatakapomalizika, wachezaji watapewa mapumziko ya siku chache kabla ya kuanza maandalizi kwa ajili ya msimu ujao wa Ligi Kuu.
Maandalizi kwa ajili ya VPL yatahusisha pia ziara ya nje ya nchi ya kujiandaa na msimu mpya, ingawa amesema nchi hiyo itatajwa baadaye.
Wachezaji wapya kikosini Azam msimu huu ni kiungo Mkenya George ‘Blackberry’ Odhiambo na kipa Deogratius Munishi kutoka Mtibwa Sugar, wakati Aishi Salum, Jackson Wandwi, Dizana, Ibrahim Rajab Jeba na Joseph Kimwaga, wamepandishwa kutoka akademi ya Azam.
Kikosi kamili cha Azam FC kinaundwa; na makipa, Mwadini Ally, Deo Munishi ‘Dida’ Aishi Salum na Jackson Wandwi, mabeki wa Ibrahim Shikanda, Erasto Nyoni, Waziri Salum, Samir Haji Nuhu, Luckson Kakolaki, Said Mourad, Joseph Owino na Aggrey Morris.
Viongo ni Kipre Bolou, Abdulhalim Humud, Himid Mao, Salum Abubakar, Abdi Kassim Sadalla, Ramadhani Suleiman Chombo, Abdulghani Ghullam, Ibrahim Rajab Jeba, Jabir Aziz Stima, Ibrahim Joel Mwaipopo, Kipre Tchetche, Mrisho Ngassa, Zahoro Pazi, Khamis Mcha na George Odhiambo ‘Blackberry’ wakati washambuliaji ni Gaudence Mwaikimba, John Bocco ‘Adebayor’.
Hii ni mara ya kwanza kwa Azam FC kucheza Kombe la Kagame, baada ya kushika nafasi ya pili katika msimu uliopita wa Ligi Kuu. Katika Kombe la Kagame mwaka huu, wenyeji Bara wataingiza timu tatu, Yanga ambao ni mabingwa watetezi, wakati Simba na Azam wanaingia kwa nafasi za uwakilishi.

KONGAMANO LA MICHEZO NA AMANI KESHO UBUNGO


Thadeo, Mkurugenzi wa Michezo

Na Princess Asia
KONGAMANO linalohusu michezo na amani (National forum on sport for development and peace) linatarajiwa kufanyika kesho mjini Dar es Salaam, BIN ZUBEIRY imeiapta hiyo.
Kongamano hilo limeandaliwa na Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo kwa kushirikiana na Taasisi ya Right to Play na British Council litafanyika kwa siku mbili kesho na keshokutwa, katika hoteli ya Blue Pearl, Ubungo, Dar es Salaam .
Mkurugenzi wa Idara ya Michezo nchini, Leonard Thadeo amesema kongamano hilo litawashirika wadau mbalimbali wa michezo kutoka ndani na nje ya nchi.
Amesema lengo la kongamano hilo ni kutoa fursa kwa wadau kubadilishana mawazo na kuelezana changamoto zinazoikabili sekta hiyo. Mbali na kubadilishana mawazo, wadau hao pia wataangalia sera ya michezo nchini na kutoa ushauri wa nini kifanyike ili kufikia malengo yaliyomo.

MAZOEZI YA SIMBA YASUASUA, WACHEZAJI ZAIDI BADO KUJITOKEZA


Wachezaji wa Simba waliokuwa mazoezini juzi
Na Prince Akbar
HADI sasa kwenye Uwanja wa TCC Chango’ombe, Dar es Salaam ambako mabingwa wa Ligi Kuu ya Tanzania Bara, Simba SC wanaendelea na mazoezi kujiandaa na Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati, hakuna mchezaji aliyeongozeka kutoka idadi ya juzi, wachezaji 13.
Kwa mujibu wa Daktari wa Simba SC, Cossmas Kapinga ambaye muda huu tayari yuko maezoini TCC, wachezaji waliokuwa na timu ya taifa nchini Msumbiji na wengine wapya, akiwemo Danny Mrwanda bado hawajafika.
Kwa maana hiyo, Kiggi Makassy aliyesajiliwa kutoka Yanga ndiye anaendelea kuwa mchezaji ‘lulu’ kwenye mazoezi hayo.
Juzi BIN ZUBEIRY ilitembelea mazoezi ya Simba TCC na kukuta wachezaji 13 wakijifua chini ya Kocha Msaidizi, Mganda Hamatre Richard, akiwemo Kiggi Makassy ingawa mshambuliaji aliyesajiliwa kutoka Dong Tam Long An ya Vietnam, Danny Davis Mrwanda hakutokea.
Mashabiki wengi wa Simba walifika mapema Uwanja wa TCC Chang’ombe, Dar es Salaam kuwashuhudia wachezaji wao, kiu zaidi ikiwa kumuona mpachika mabao wao wa zamani, aliyerejea kikosini Mrwanda, lakini Meneja wa Simba, Nico Nyagawa akaiambia BIN ZUBEIRY kwamba mchezaji huyo ni miongoni mwa waliotoa udhuru.
Waliohudhuria ni pamoja na Salim Kinje, Abdalllah Juma, William Mweta, Hamadi Waziri, Abuu Hashim, Haroun Athumani, Haruna Shamte, Amri Kiemba, Paul Ngalema, Uhuru Suleiman, Patrick Kanu Mbivayanga na Abdallah Seseme.
Mazoezi hayo yaliongozwa na Richard kwa sababu Kocha Mkuu, Mserbia Milovan Cirkovick bado anakula sikukuu kwao.
Simba itaendelea na program ya mazoezi kwa jioni tu wiki hii na Nyagawa amesema anatarajia idadi ya wachezaji itakuwa ikiongezeka taratibu wiki hii, wakiwemo wachezaji waliokuwa na timu ya taifa Msumbiji nao pia wanatarajiwa kuungana na wenzao wakirejea kutoka nchini humo.
Mrwanda ambaye amesaini mkataba wa mwaka mmoja wa kuichezea Simba, ambao hauna kipengele cha kumruhusu kuuvunja kabla haujamalizika naye anatarajiwa kuanza maozezi wakati wowote wiki hii.
Mrwanda, awali ilielezwa anataka kusaini mkataba ambao wakati wowote akipata timu nje, aondoke, lakini kwa mujibu wa mkataba aliosaini Simba ni kwamba akipata timu italazimika kumnunua kutoka kwa Wekundu wa Msimbazi, au isubiri hadi amalize mkataba.
Habari za uhakika, kutoka ndani ya Simba SC ambazo BIN ZUBEIRY imezipata, zimesema kwamba Mrwanda ameridhika na mkataba huo na ameahidi kufanya vitu baab kubwa Msimbazi.
Kwa upande mwingine, Simba SC imeamua kumtema kiungo Salum Machaku kwa makubaliano maalum ya pande zote mbili ya kuvunja mkataba. Simba ilitaka kumtoa kwa mkopo Machaku, lakini mwenyewe akasema bora aachwe moja kwa moja.
Tayari Simba imemsajili kiungo wa Yanga, Kiggi Makassy kuziba nafasi ya Machaku. Machaku sasa ameingia kwenye mazungumzo na Yanga.

BARTHEZ AANZA MAZOEZI RASMI YANGA JIONI HII


Barthez

Na Prince Akbar
KIPA wa Simba, Ally Mustafa ‘Barthez’ ameanza mazaoezi jioni hii katika klabu yake mpya, Yanga SC kwenye Uwanja wa Kaunda, Dar es Salaam.
Barthez ni miongoni mwa wachezaji 17 ambao hadi sasa tayari wapo Uwanja Kaunda wakijifua chini ya kocha Freddy Felix Minziro.
Wengine ni Said Bahanuzi na Juma Abdul, wote kutoka Mtibwa Sugar ya Morogoro na Nizar Khalfan aliyekuwa akichezea Philadelphia Union ya Marekani- hao ni kwa upande wa wachezaji wapya.
Nizar
Wachezaji wa zamani ambao hadi sasa wamekwishafika Jangwani ni Juma Seif ‘Kijiko’, ambaye kulikuwa kuna tetesi anakwenda Simba, Hamisi Kiiza, Kenneth Asamoah, Yaw Berko, Shamte Ally, Jerry Tegete, Stefano Mwasyika, Godfrey Taita, Athumani Iddi ‘Chuji’, Oscar Joshua, Nadir Haroub ‘Cannavaro’, Idrisa Senga, Omega Seme na Ibrahim Job.
Yanga imeanza mazoezi jana kujiandaa na michuano ya Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati, Kombe la Kagame, inayotarajiwa kuanza Julai 14 hadi 29, ikishirikisha na timu nyingine mbili za Tanzania, Simba SC mabingwa wa Ligi Kuu na Azam FC washindi wa pili.
Yanga ndio mabingwa watetezi wa Kombe la Kagame, baada ya mwaka jana kuifunga Simba SC kwenye fainali bao 1-0, mfungaji Kenneth Asamoah.

MAMIA WAUAGA MWILI WA MPIGANAJI WILLY EDWARD OGUNDE DAR


Mwenyekiti wa Chama cha Wananchi (CUF),Prof. Ibrahim Lipumba akitoa heshima zake za mwisho kwa Mwili wa Marehemu Willy Edward ambaye alikuwa Mhariri wa Gazeti la Jambo Leo aliefariki ghafla huko mkoani Morogoro mwishoni mwa wiki.Hafla hii ya kuaga imefanyika mchana huu katika viwanja vya Mnazi Mmoja,Jijini Dar es Salaam. PICHA NA FATHER KIDEVU BLOG.

MJUE ABDALLAH SALIM JUMA, MTAMBO MPYA WA MABAO MSIMBAZI KUTOKA JESHINI



Na Dorris Maliyaga
FURAHA hukamilika kwa mchezaji yeyote anayetoka katika timu ndogo za Ligi Kuu Tanzania Bara na kujiunga na moja ya klabu kubwa kama Simba, Yanga na Azam.
Mshambuliaji Abdallah Salim Juma ni kati ya wachezaji wenye furaha msimu huu kwa sababu ataanza kuonekana katika jezi za rangi nyekundu na nyeupe.
Hii ni baada ya kujiunga na Simba kwa mkataba wa miaka miwili akitokea Ruvu Shooting na ataanza kuonekana katika klabu yake hiyo mpya kwenye michuano ya Kombe la Kagame.
Abdallah, ambaye ni mrefu kwa umbo na ana nguvu, sifa ambazo humfanya awe kikwazo kwa mabeki wasumbufu ambao huambulia patupu wanapojaribu kumdhibiti na ndicho kilichowashawishi mabingwa hao wa Ligi Kuu Bara kumsajili.
Kutokana na mafanikio hayo, Mwanaspoti ilimtafuta nyota huyo na kufanya naye mahojiano ya kina na yeye anaeleza sababu ya kutua hapo na malengo yake kwa ujumla.

Sababu ya kujiunga Simba
Abdallah aling'ara akiwa na Ruvu Shooting msimu wa Ligi Kuu Bara uliomalizika kutokana na mchango wake hadi kuibakiza klabu hiyo katika ligi na ndiyo sababu iliyowavutia Simba wakamsajili.
Anasema amejiunga hapo kwa sababu yalikuwa malengo yake ya muda mrefu; "Nilikuwa na mipango ya kucheza klabu kubwa nisiishie hizi ndogo, ikiwa ni njia ya kufanikiwa mipango yangu kucheza soka la ushindani nje ya nchi.
"Hata hivyo, Simba naipenda, lakini pamoja na mapenzi yangu maslahi pia yamechangia, mimi ni mchezaji na kipaji changu cha soka ndiyo ajira yangu, kipato nitakachokipata hapa si sawa na nilichokuwa nakipata nikiwa na Ruvu,"anasema Abdallah, ambaye anaishabikia Arsenal ya England.
Anaeleza kuwa kutua kwake Simba ni hatua ya mafanikio makubwa kwake.
Abdallah amezungumzia pia changamoto na ushindani wa namba atakaokutana nao klabuni hapo; "Ushindani upo kila mahali na hasa katika klabu kubwa kama Simba, nimejipanga kuhakikisha nakabiliana nazo ili kuipa mafanikio klabu yangu,"anasema Abdallah, anayependa soka ya Fernando Torres wa Chelsea.
"Ninachowaahidi mashabiki wa Simba watulie na wanipe ushirikiano kwani nitajituma kadri niwezavyo nikishirikiana na wenzangu kuhakikisha tunaipa mafanikio Simba," anaongeza Athumani.

Fundi wa magari Abdallah anasema mbali na kipaji cha soka yeye ni fundi mzuri wa magari.
"Kabla sijaingia rasmi kwenye soka, nilipomaliza shule nyumbani Shinyanga, nilienda kwa dada yangu Sheila ambaye anaishi Simanjiro, Manyara, nilipokuwa huko alinisomesha Chuo cha Veta ambako nilisoma ufundi wa magari.
"Nilipata elimu hiyo na mara nyingine huwa nafanya kazi hiyo kwani naimudu vizuri,"anasema Abdallah ambaye anaweka wazi aliifanya kazi hiyo, alipokuwa anaichezea AFC Arusha.
"Nilikuwa nafanya shughuli ya ufundi magari kipindi cha mapumziko ya ligi au baada ya mechi, wakati huo nilikiwa naichezea AFC Arusha.
"Kuna gereji moja iko Ngaramtoni, Arusha ndiko nilikuwa naenda kufanya shughuli zangu huko,"anaeleza Abdallah.
Amefafanua kuwa tangu alipoondoka Arusha na kuja Dar es Salaam alipojiunga na Ruvu Shooting hakuweza kufanya tena shughuli hizo kutokana na kukosa muda.

Nje ya soka "Ninapokuwa sina majukumu ya soka, huwa napenda kutulia nyumbani kuangalia picha za Kihindi na msanii ninayempenda ni Akshey,"anasema Abdallah.
Ameweka wazi kuwa husikiliza pia muziki wa Bongo Fleva na msanii anayempenda ni Juma Nature.

Alikotokea Abdallah anasema, kipaji chake cha soka tangu alipokuwa mtoto mdogo akiwa shule ya msingi Buhangila alikosoma hadi la tatu kabla ya kuhamishiwa Salawe alikomaliza darasa la saba na zote ziko Shinyanga.
Alipata umaarufu zaidi alipokuwa akiichezea klabu yake ya mtaa ya Vijana Sejese, Kahama, Shinyanga na kushiriki michuano mbalimbali.
"Hapo niling'ara na ndio Polisi Shinyanga waliniona na kunisajili kabla ya kujiunga na Mwanza United," anaeleza Abdalah ambaye hata hivyo hakudumu na Mwanza United na kusajiliwa na AFC Arusha mwaka 2007.
Anasema aliichezea AFC kwa msimu mmoja akaenda Kagera Sugar na kuichezea misimu miwili, baada ya hapo alirudi tena AFC Arusha mwaka 2010 wakaipandisha Ligi Kuu na mwaka 2011 alitua Ruvu Shooting na sasa Simba.

Historia Abdallah anasema katika familia yao walizaliwa watatu, lakini mkubwa wao, Sadi ni marehemu na yeye ni wa mwisho yupo na kaka yake, Juma.
Alisoma na Shule ya Msingi ya Buhangija, Shinyanga na kumalizia darasa la saba Salawe kabla ya kujiunga na Chuo cha Veta huko Simanjiro.
Upande wake, yeye ni baba wa mtoto mmoja anayeitwa, Salum (2) na mke mmoja anaitwa, Amina Yusuph.

SOURCE: GAZETI LA MWANASPOTI


HUYU NDIYE IBRAHIM RAJAB JEBA ANAYEZIGOMBANISHA SIMBA NA AZAM



Na Dorris Maliyaga
KIUNGO Ibrahim Rajab Juma Jeba amesisitiza kwa sasa ndoto yake ni kujiunga na Simba licha ya kuwekewa zengwe na timu yake ya Azam.
"Ndoto yangu katika msimu ujao wa Ligi Kuu Bara ni kuvaa jezi za rangi nyeupe na nyekundu," anasema Jeba.
Ndoto ya Jeba huenda ikayeyuka kwani Azam imewasilisha malalamiko Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) kupinga usajili wake.
Jeba, ambaye amejazia kwa mazoezi anasifika kwa kujituma na kuwa msumbufu uwanjani.
Ni miongoni mwa wachezaji waliosajiliwa na Simba kwa ajili ya msimu ujao. Amesaini mkataba wa miaka miwili.
Sakata hilo la kuzuiwa na Azam linamnyima raha mchezaji huyo.
Kutokana na mkasa huo, Mwanaspoti ilizungumza na Jeba kwa kirefu juu ya mkasa huo na yeye anaeleza pamoja na malengo yake.

Mvutano wake na Azam
Jeba anaizungumzia Azam kuwa ni klabu bora kwake, lakini hakuwa na bahati nayo kwa sababu licha ya kucheza kikosi cha timu ya vijana wenye umri chini ya miaka 20 kwa mafanikio katika michuano mbalimbali, lakini ilishindwa kumwamini na kumjumuisha katika timu ya wakubwa.
"Azam ni bora kwangu kutoka waliponitoa hadi hapa nilipo ni juhudi zao,"anaeleza Jeba anayeishabikia klabu ya Chelsea ya England na anavutiwa na soka ya Mbrazili Ricardo Kaka wa Real Madrid.
Akizungumzia mkasa wake wa usajili, Jeba anasimulia kuwa walikubaliana na Azam wamwache na walitekeleza hilo kwani kwa muda mrefu walikuwa hawamlipi mshahara.
"Ninachowaambia Azam nawaomba waniache kama tulivyokubaliana, wasiniwekee vikwazo kwa sababu mimi ni kijana natafuta maisha, waniache nijaribu bahati lakini si kuniwekea pingamizi,"anaeleza kwa masikitiko.
Meneja wa klabu hiyo, Patrick Kahemele anasema, Jeba ni mchezaji wao na kudai kuwa Simba wamempora mchezaji wao.
Kahemele alifananisha kitendo kile na kitendo cha Chelsea kumnyakua Gael Kukuta wa Lens ya Ufaransa.
"Jeba ni mchezaji wa timu ya yosso ya Azam hata bila mkataba anafungwa, lakini pia ana mkataba na Azam uliosainiwa Novemba 2011 na ikamtoa mkopo kwenda Villa Squad. Huko hakwenda kwani alikuwa anaumwa mguu.
"Kitendo cha Simba kufanya naye mazungumzo, kumhamisha kinyemela na kufanya nao mazoezi ni uvunjifu wa kanuni za soka kama si kuleta vurugu tulizoanza kuzisahau."

Sababu ya kujiunga Simba
"Nimejiunga Simba kutokana na mpango wao wa kuendeleza vijana kwani idadi ya wengi walioko hapo wamefanikiwa kutokana na kuaminiwa na kupewa nafasi ya kucheza,"anasema na kutolea mifano kwa Shomari Kapombe, Edward Christopher, Abdallah Seseme, Ramadhan Singano Messi na Jonas Mkude.
"Lakini pia, Simba ninaipenda tangu nilipokuwa mdogo, nilitamani siku moja niichezee na sasa nimekamilisha ndoto zangu.
"Kingine ni maslahi kwa sababu mpira ndiyo ajira yangu na pia nilitaka kubadilisha mazingira kuona kama naweza kutimiza ndoto zangu,"anaeleza Jeba na kudokeza, mmoja wa viongozi wa Simba alichangia huduma ya matibabu, alipokuwa amevunjika mguu na kuwekwa bandeji ngumu (P.O.P).
Aliumia katika mechi ya fainali ya Kombe la Uhai mwaka jana kati ya Azam na Simba.
Anaongeza na kusema kutokana na mapenzi pamoja na kujituma, anaamini atafanikiwa kwani atajibidiisha na kufuata maelekezo ya kocha wa Simba, Milovan Cirkovic kwa ufasaha na kuahidi hawatajutia usajili wake.
Jeba anazungumzia pia ushindani wa namba, kwani katika kikosi cha Simba, anafahamu atakuwa na kibarua cha kugombea namba na wakali kama Haruna Moshi Boban, Mwinyi Kazimoto na Mzambia Felix Sunzu.
"Wale ni wakubwa wangu na wananizidi ujuzi lakini nafahamu utafika wakati wangu nami nitapata nafasi."

Chanzo cha kutungiwa jina Jeba
Jeba anasema jina hilo lilitungwa na watu wa karibu yake na lilikuwa zaidi kutokana na kucheza kwake soka.
"Nilipewa jina hili na watu wa karibu yangu na wao walikuwa na maana kuwa, pamoja na umri wangu mdogo niliokuwa nao, nilionekana kama na umri mkubwa ndio wakaniita jina la Jeba.
"Licha ya muonekano wangu, lakini niliweza kupambana na walio wakubwa zaidi yangu, ndipo likaendelea kukua, likazoeleka mpaka sasa,"anaeleza Jeba na kuongeza analifurahia jina hilo.

Alivyopenya katika soka
Jeba anasema kipaji chake kilianza kuonekana tangu alipokuwa mdogo na aliyechangia sehemu kubwa ya mafanikio yake ni baba yake mzazi, Mzee Ibrahim Rajab.
"Kipaji changu kilianza kujionyesha tangu nikiwa mdogo nilipoanza Shule ya Msingi ya Mwanakwerekwe huko Zanzibar na nilishiriki mashindano mbalimbali.
"Soka la ushindani nilianza katika timu yangu ya mtaa, Simba Kids ambayo pia niliihama 2005 na kujiunga na Lebanon.
"Nilipokuwa Lebanon mwaka 2007, klabu ya Ras El Khalima ilinichukua kwa ajili ya michuano ya Ligi Daraja la Kwanza la Zanzibar ambayo pia sikukaa nayo sana nikajiunga na Ochu Boys yenyewe ilikuwa Ligi Daraja la Pili,"anasema Jena na kuweka wazi sababu zilizomsababishia kuhamahama kwa ajili ya kutafuta njia ya kutoka na maslahi.
Hali hiyo ndiyo ilimsaidia pia, kwani mwaka 2010 alivyokuja na timu ya Mkoa wa Mjini Magharibi ya Zanzibar katika michuano ya Copa Coca Cola, Azam ilimwona na kumjumuisha katika kikosi chao cha vijana wenye umri chini ya miaka 20 kabla ya kujiunga na Simba, msimu huu.
Alizichezea pia timu za taifa za vijana Tanzania, chini ya miaka 17, chini ya miaka 20 na chini ya miaka 23, lakini pia alikuwa katika kikosi cha timu ya taifa ya Zanzibar 'Zanzibar Heroes' kilipokuwa kikijiandaa na mashindano ya Kombe la Chalenji mwaka jana na kwenda nayo kambini Misri.


SOURCE: GAZETI LA MWANASPOTI:

FIRST ELEVEN YA MAGARASA HATUA YA MAKUNDI EURO 2012


Mario Balotelli - Italy
Getty Images
ANALYSIS
By Andrew Kennedy

BAADA ya siku 12 mfululizo za hatua ya makundi ya michuano ya Euro 2012, BIN ZUBEIRY kwa msaada wa Goal.com inakuletea kikosi cha kwanza cha wachezaji walioboronga kutoka vikosi vyote katika fainali hizo zinazoendelea Poland na Ukraine.
CHALKIAS
UGIRIKI

MAGGIO RAMI PAPADOPOULOS LIMBERSKY
ITALIA UFARANSA UGIRIKI JAMHURI YA CZECH

MILNER KOLAR KARAGOUNIS MALOUDA
ENGLAND JAMHURI YA CZECH UGIRIKI UFARANSA


BALOTELLI BAROS



ITALIA JAMHURI YA CZECH

No comments: